Ligi Kuu Bara irejee na ubora, burudani

21Nov 2020
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Ligi Kuu Bara irejee na ubora, burudani

TIMU zinazoshiriki Ligi Kuu Bara zimerejea tena katika vita ya kuwania ubingwa wa ligi hiyo baada ya kumalizika kwa kalenda ya kimataifa ambapo kwa Tanzania (Taifa Stars), ilikuwa inakabiliwa na mchezo miwili ya ugenini na nyumbani dhidi ya Tunisia.

Mechi hizo mbili zilikuwa ni kwa ajili ya kusaka tiketi ya kushiriki fainali zijazo za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon 2022), ambazo zitafanyika nchini Cameroon.

Ligi Kuu Tanzania Bara ambayo inashirikisha timu 18 kutoka mikoa mbaliambali, imerejea kuanzia jana kwa timu sita kushuka kwenye viwanja vitatu tofauti ili kusaka pointi tatu muhimu zitakazowapeleka kwenye malengo yao ya msimu huu.

Timu nyingine nane zitashuka dimbani leo wakiwamo mabingwa watetezi, Simba ambayo imewafuata Coastal Union jijini Arusha, wakati raundi ya 11 itakamilika kesho kwa Yanga kuwakaribisha Namungo FC kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam, huku Mwadui FC ikiwafuata Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Kaitaba, Mjini Bukoba.

Ili ligi hiyo ya ngazi ya juu kwa upande wa Tanzania Bara ionekane kuwa bora na ya thamani ni vyema timu zote zikaingia uwanjani kuonyesha soka la kiwango cha juu.

Timu itakayoonyesha ubora katika mechi zake zote, itajiweka kwenye mazingira mazuri ya kupata ushindi au kuambulia sare dhidi ya mpinzani wake.

Mbali na kupata pointi, ambalo ndio lengo kuu kwa kila timu, lakini wachezaji husika hujiweka sokoni kwa kuzivutia klabu nyingine ambazo zinahitaji kujiimarisha kwa kusajili nyota wapya mara baada ya dirisha dogo la usajili litakapofunguliwa mwezi ujao.

Mpira wa miguu ni mchezo wa hadharani, hivyo kila ambaye ataitumia vyema nafasi ya kujituma, kucheza kwa kiwango cha juu na kudumisha nidhamu ndani na nje ya uwanja, atakuwa amejiweka jirani au amejifungulia njia ya mafanikio.

Nipashe inaamini wakati ligi imesimama kupisha timu za taifa mbalimbali kuendelea na majukumu yake, makocha wametumia nafasi ya kurekebisha makosa waliyoyaona kwenye mechi 10 zilizotangulia, na sasa wako tayari kuwapa mashabiki na wanachama wao burudani.

Ni wazi timu ambayo itarejea uwanjani ikiwa na mipango ya kucheza kandanda safi, itajipatia ushindi lakini pia itawaweka wachezaji wake 'sokoni' kutokana na burudani ambayo wataionyesha katika kila mchezo.

Tunaamini Kamati ya Waamuzi iliyoko chini ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), pamoja na Bodi ya Ligi Kuu imetumia pia muda huo wa mapumziko kuwajengea uwezo zaidi waamuzi wake kwa ajili ya kufanya vyema kazi yao.

Kufanya vizuri kwa waamuzi, ni sehemu mojawapo inayotegemewa katika kuwajenga wachezaji wetu na hatimaye kupata wawakilishi wa mashindano ya kimataifa ambao wameiva na hawakupatikana kwa njia ya 'kubebwa'.

Kwa waamuzi kufanya kazi yao kwa weledi, itamsaidia pia Kocha Mkuu wa Timu ya Taifa (Taifa Stars), Etienne Ndayiragije katika maandalizi ya kikosi chake kitakachoshiriki kwenye fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN), ambazo zitafanyika Januari, mwakani huko Cameroon.

Ligi hiyo ndiyo pekee itakayotoa wachezaji wengi watakaounda kikosi kitakachokwenda kupeperusha bendera ya nchi kwenye fainali hizo za CHAN, hivyo wanahitaji kupata misingi imara kuanzia kwenye mazoezi hadi wanapokuwa uwanjani.

Haipendezi kuona waamuzi wanaendelea kufungiwa, huku timu iliyonyimwa haki yake ikiendelea kuumia kwa sababu matokeo ya uwanjani hubaki vile vile.

Nipashe inawakumbusha pia mashabiki wa soka kufahamu mipaka ya majukumu yao na kuacha kuingia mambo ya kiufundi yanayofanywa na makocha.

Habari Kubwa