Lugha za kuwanyanyapaa wenye ualbino ziepukwe

04Jun 2019
Mhariri
DAR
Nipashe
Lugha za kuwanyanyapaa wenye ualbino ziepukwe

KATI ya mambo ambayo yanawatia simamzi wenzetu wenye ualbino na kuwakosesha amani ya kuishi kama watu wengine hapa duniani ni lugha zinazotumika kuwaita na vitendo vya ukatili wanavyofanyiwa.

Mara kwa mara tumesikia kundi la watu wenye ualbino likifanyiwa vitendo hivyo vikiwamo vya kukatwa viungo vyao na kuuawa kwa sababu ya imani za kishirikina.

Vitendo hivyo vilishamiri sana mwanzoni mwa miaka ya 2006, 2007, 2008 mpaka 2015 na kufanya nchi kuingia doa ndani na nje kwenye jumuiya za kimataifa kutokana na baadhi ya Watanzania kufanya ukatili huo dhidi ya watu wenye ualbino.

Vitendo hivyo ni pamoja na kukatwa viungo, kuwaua, ufukuaji wa makaburi na mambo ya kishirikina.

Shirika la Under The Same Sun (UTSS), ambalo liliundwa nchini Canada mwaka 2008 na kusajiliwa kisheria hapa nchini mwaka 2009 kwa dhumuni la kuunga mkono juhudi za serikali katika kulinda na kutetea haki za kibinadamu za kundi hilo, linafanya juhudi za kuelimisha umma ili kuelewa chanzo cha ualbino, changamoto wanazokabiliana nazo, wajibu wa jamii katika kutatua changamoto hizo ili kuhakikisha usalama wa kila raia nchini.

Kupitia vyombo vya habari elimu inayotolewa na Shirika hilo itawafikia watu wengi zaidi na vitendo hivyo vinaweza kukomeshwa, na wenzetu wakaishi maisha ya amani kama wanavyoishi watu wengine.

Elimu kwa umma kuhusu ualbino inayotolewa na UTSS ni matokeo ya ugunduzi usio na shaka kwamba, Watanzania wengi hawana taarifa sahihi kuhusu ualbino na jamii nyingi zimejiundia imani potofu dhidi ya kundi hilo na hivyo kuliweka katika hatari ya kudhulumiwa haki zao.

Kazi kubwa ya wanahabari ni kuhakikisha wanatumia lugha sahihi wakati wa kuporipoti habari za kundi hilo ili hata jamii inaposoma, kusikilia au kuangalia kwenye vyombo hivyo inajifunza na kupata maneno sahihi ya kutamka, badala ya kutumia maneno ya kuudhi au ya kunyanyapaa.

Lugha isiyo sahihi kuwaita watu wa kundi hilo ni zeruzeru, albino, watu wenye ulemavu wa ngozi na maalbino.

UTSS imetoa lugha sahihi inayopaswa kuliita kundi hilo kuwa ni ‘Watu wenye ualbino’.

Lugha zisizo sahihi zinapotumika kwa kundi fulani huonyesha unyanyapaa. Kwa mfano kumuita mtu kipofu, kiziwi, bubu au kiwete haipendezi na kumfanya mwenye ulemavu huo kujiona anatengwa kwenye jamii.  

UTSS imeona umuhimu wa kutafuta fursa ya kufikisha elimu hii kupitia vyombo vya habari kupeleka kwa jamii kwasababu vyombo hivi ni kama mhimili wa nne wa dola. Vyombo vya habari vinapotoa ujumbe unakuwa umefikia takribani nchi nzima na kwa muda mfupi.

Vyombo vya habari kupitia kalamu zao vinaweza kuleta amani au kusababisha machafuko kama ujumbe hautafikishwa sahihi. Vyombo hivi vinaaminika na jamii na vinapotoa habari sahihi ni rahisi kwa Watanzania kujifunza kwa urahisi na uharaka.

Vyombo vya habari vina jukumu kubwa la kuheshimu na kutekeleza ombi la UTSS la kuhakikisha lugha potofu dhidi ya kundi hilo inaepukwa na kutumia lugha sahihi ili jamii nayo ielimike na kuacha kuita majina yanayonyanyapaa kundi hilo.

Habari Kubwa