Lugola usishangae, chukua hatua sasa

25Jun 2019
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Lugola usishangae, chukua hatua sasa

TANGU Mbunge wa Mwibara, Kangi Lugola, ateuliwe kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, amekuwa akitoa maagizo mbalimbali kwa Jeshi la Polisi, lakini mara kadhaa baadaye amekuwa akibaini kuwa hayatekelezwi.

Maagizo yake mengi amekuwa akiyatoa kwa lengo la kumaliza kero mbalimbali za muda mrefu ambazo zinalalamikiwa na wananchi katika maeneo mengi.

Ni jambo la kumpongeza sana Waziri Lugola kwa kujitahidi kufuatilia kwa lengo la kubaini matatizo na kero za muda mrefu ambazo zimekuwa zikiwakabili wananchi.

Waziri huyo amekuwa akitumia ziara zake katika maeneo mbalimbali kwa kuandaa mikutano na kuzungumza na wananchi, huku akiwapa fursa ya kueleza kero mbalimbali, ambazo wamekuwa wakikabiliwa nazo.

Pale anapoelezwa, huwa hasiti kuwauliza maswali mbele ya wananchi wale wote wanaoshindwa kuwajibika na kuwabababisha wananchi kupata usumbufu, hivyo kutoa maagizo ili zimalizwe.

Sio hivyo tu, bali wakati mwingine Lugola amekuwa akifanya maamuzi yakiwamo ya kuwaaadhibu baadhi ya askari na maofisa wa polisi ambao wanasababisha matatizo kadhaa.

Pia amekuwa akieleza kuwa anafanya hivyo kwa kutekeleza kwa vitendo ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2015-2020, ambayo pamoja na mambo mengine, inaeleza kuwa serikali itahakikisha inalinda usalama wa raia na mali zao.

Kimsingi, Lugola ametoa maagizo mengi, lakini kubwa ambalo amekuwa akilisisitiza ni polisi kutowanyanyasa wananchi, ikiwamo kuwabambikia kesi na kuwaweka katika vituo bila kuwafikisha mahakamani.

Waziri huyo, juzi alieleza kushangazwa na kuona mahabusi 11 waliofutiwa kesi mahakamani kuwekwa katika Kituo cha Polisi Gogoni, Wilaya ya Kipolisi Kimara jijini Dar es Salaam kwa zaidi ya miezi sita kinyume cha sheria.

Lugola alieleza hayo alipofanya ziara ya kushtukiza katika kituo hicho kwa ajili ya kufuatilia utekelezaji wa maagizo aliyoyatoa.

Alisema kumekuwa na malalamiko ya kuwapo kwa baadhi ya vituo vya polisi vinavyokaa na watuhumiwa kwa muda mrefu bila kuwafikisha mahakamani.

Alisema katika kituo hiki cha Gogoni taarifa nilizokuwa nazo kinaongoza kwa kuwashikilia watuhumiwa na kukaa nao kwa muda mrefu bila kuwafungulia mashtaka mahakamani.

Kwamba baada ya kufika katika kituo hicho, alikutana na mahabusi 32, na kuwahoji mmoja baada ya mwingine kisha mahabusi 11 waliofutiwa kesi zao.

Lugola alisema watuhumiwa hao 11 wanakabiliwa na kesi za mauaji, na kuwa miongoni mwa alivyowahoji wengine wamekaa gerezani miaka saba na baada ya muda huo sasa mahakama imewarudisha katika vituo vya polisi kufuata kesi zao.

Alisema wana miezi sita katika kituo hiki, hivyo, kama waziri, hiyo sio sawa.

Tunaona kuwa hii siyo sawa, na pengine ndio maana wakati mwingine mahabusi wanateseka na kuamua kugoma, kutokana na kuona wamenyimwa haki yao ya msingi ya kufikishwa mahakamani.

Tunamshauri Waziri Lugola asiwe analalamika anapobaini maagizo yake yamepuuzwa, bali aanzishe utaratibu mzuri wa kufuatilia utekelezaji wa maagizo anayoyatoa.

Pia aweke utaratibu wa kuwasiliana na ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka kuhakikisha kesi za jinai zinapelekwa mahakamani kwa wakati mwafaka.

Ili kumaliza matukio haya, itakuwa vizuri jukumu la kufuatilia utekelezaji wa maagizo ya waziri likakabidhiwa kwa wakuu wa polisi wa wilaya na mikoa, ili wawe wa kwanza kuwajibika ikiwa mambo yatakuwa kinyume chake.

Habari Kubwa