Ma-RC, Ma-DC zingatieni haya utumbuaji wa majipu

19May 2016
Mhariri
Dar
Nipashe
Ma-RC, Ma-DC zingatieni haya utumbuaji wa majipu

MAKAMU wa Rais, Samia Suluhu Hassan, ametoa angalizo kwa wakuu wa mikoa na wilaya, akiwataka kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za utumishi wa umma, wakati wanapotaka kuwafukuza kazi watumishi hao.

Akizungumza mkoani Arusha juzi, Makamu wa Rais alisema kuwa angalizo lake halina maana kuwa ni kupinga kauli ya Rais John Magufuli ya kutumbua majipu, lakini wakuu wa mikoa na wilaya wanapaswa kuhakikisha wanapotaka kuwawajibisha watumishi wa umma wanafuata sheria, kanuni na taratibu za utumishi wa umma na sio vinginevyo.

Aliwakumbusha viongozi hao kuwa mwenye mamlaka ya kutumbua majipu ni Rais pekee kwa kuwa sheria za nchi zinampa mamlaka ya kuteua, kuajiri na kufukuza, hivyo viongozi wengine wakiwamo wakuu wa mikoa na wa wilaya wanapaswa kufuata taratibu za utumishi wa umma.

Kimsingi, Samia ametoa maelekezo ya msingi kwa viongozi hao wakati huu ambao Serikali ya Awamu ya Tano imejielekeza pamoja na malengo mengine, kurejesha nidhamu katika utumishi wa umma ikiwamo kuwachukulia hatua watumishi wote ambao wanakiuka taratibu, sheria, kanuni na misingi ya utumishi wa umma.

Katika kutekeleza hatua hizo, baadhi ya watumishi wa umma wamesimamishwa kazi kusubiri hatua zaidi baada ya kukamilika kwa uchunguzi na wengine wameshafikishwa kwenye mahakama wakisubiri maamuzi ya mhimili huo.

Ushauri wa Makamu wa Rais umetolewa wakati mwafaka kwa sababu tangu Rais Magufuli alipoanza kuwachukulia hatua baadhi ya watumishi wa umma, viongozi wengine wa umma wakiwamo wakuu wa wilaya na mikoa walianza kuunga mkono jitihada zake kwa kuwachukulia hatua watumishi walioko katika maeneo yao, lakini baadhi wakionekana kutofuata sheria, kanuni na taratibu.

Tumewasikia baadhi yao wakitangaza kuwachukulia hatua watushishi walioko kwenye maeneo hao hususan katika halmashauri, lakini mazingira ya kuwasimamisha kazi yamekuwa yakiacha shaka kama kweli wamefuata sheria, kanuni na taratibu za utumishi wa umma.

Hatupingani na hatua wanazozichukua wakuu wa mikoa na wilaya katika dhana nzima ya utumbuaji wa majipu kwa lengo la kumuunga mkono Rais Magufuli kutokana na kasi ya mmomonyoko wa maadili katika utumishi wa umma, isipokuwa tunataka sheria, kanuni na taratibu za utumishi wa umma zizingatiwe.

Hatusemi kuwa wakuu wa wilaya na mikoa hawana mamlaka ya kuwasimamisha kazi watumishi wa umma wakiwamo wa halmashauri, lakini wanatakiwa kufanya hivyo baada ya kuwasiliana na wizara ambazo watumishi hao wameajiriwa.

Watumishi wote waandamizi walioko katika halmashauri wameazimwa kwani ajira zao ziko kwenye wizara, hivyo kama mtumishi wa aina hiyo amefanya makosa yanayohitaji hatua za kinidhamu, ni lazima wizara yake pamoja na Utumishi watoe baraka kwa mkuu wa wilaya au mkuu wa mkoa kutangaza kumsimamisha kazi wakati hatua nyingine zikisubiri.

Kama alivyosema Makamu wa Rais kwamba mwenye mamlaka ya kuteua, kuajiri na kufukuza watumishi wa umma ni Rais pekee, ni vizuri kwa viongozi wa umma kulijua hilo na kuhakikisha kwamba wanafuata sheria, kanuni na taratibu za utumishi wa umma ili kuepukana na uwezekano wa baadhi ya viongozi wa umma kufanya maamuzi ya kuwaonea watumishi ambayo hatimaye yanaigharimu serikali.

Tunaunga mkono utumbuaji wa majipu kwa watumishi wa umma wavivu, wazembe na wasiofuata maadili ya utumishi wa umma, lakini tunawashauri viongozi katika utumishi wa umma kufuata sheria, kanuni na taratibu wakati wa kuwashughulikia kama alivyotoa angalizo Makamu wa Rais.

Habari Kubwa