Maandalizi makubwa yanahitajika Simba CAF

07Feb 2022
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Maandalizi makubwa yanahitajika Simba CAF

NI klabu ya Simba pekee kwa sasa inayobeba dhamana ya nchi kwenye michuano ya kimataifa wakati huu Watanzania wakitamani kuona msimu ujao Tanzania inaingiza tena timu nne kwenye michuano inayoandaliwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF); mbili Ligi ya Mabingwa na idadi kama hiyo Kombe la Shirikisho

Ikumbukwe tayari wawakilishi wengine wa Tanzania Yanga, Azam FC na Biashara United walishaaga michuano hiyo na Simba pekee ndiyo imetinga hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika, ambapo itaanza kurusha karata yake ya kwanza Jumapili wiki hii dhidi ya Asec Mimosas ya Ivory Coast kwenye mechi itakayopigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa.

Kwa mantiki hiyo, hadi sasa matarajio ya Tanzania kutetea kuingiza tena timu nne msimu ujao, yapo mikononi mwa Simba pekee, na katika hilo hakuna njia ya mkato zaidi ya timu hiyo kufanya maandalizi ya kutosha ili kuweza kufika mbali kwenye michuano hiyo hatua ambayo itaiongezea nchini pointi na kuwa miongoni mwa timu 12 zitakazoingiza timu nne msimu ujao kwenye michuano hiyo ya CAF.

Simba ambayo ipo kundi moja na Asec Mimosas, usgn ya Niger pamoja na RS Berkane ya Morocco, itaanza mechi hizo za hatua ya makundi Jumapili katika Uwanja wa Benjamin Mkapa dhidi ya Wamorocco hao, huku lengo lao likiwa ni kutinga hatua ya nusu fainali.

Hatuna hofu kwa Simba katika jukumu hilo na malengo yao ya kufika hatua hiyo ya nusu fainali hasa tukizingatia uzoefu wao katika michuano ya kimataifa na ubora wa kikosi chao pamoja na benchi la ufundi.

Jambo la muhimu kwa sasa, ni Simba kujiandaa vema kuelekea mchezo huo ili kuhakikisha inapata ushindi wa kishindo nyumbani kabla ya kwenda kucheza mechi mbili ugenini mfululizo dhidi ya usgn na RS Berkane.

Tunaamini kama Simba itaanza kwa ushindi nyumbani, kutajenga ari kubwa kwa wachezaji kuelekea mechi zinazofuata na hata kwa mashabiki katika kuipa hamasa timu yao, ili kuweza kufikia malengo yao waliojiwekea msimu huu, lakini kupigania nafasi hizo nne kwa Tanzania.

Ikumbukwe nafasi moja inayopambaniwa ya kuingiza timu nne kwenye michuano hiyo ya CAF, hadi sasa tayari Libya imefikia pointi za kuingiza timu nne msimu ujao huku ikiwa na timu mbili ambazo bado zipo kwenye michuano hiyo ya CAF, hivyo kama Simba ikishindwa kutinga robo fainali na hata nusu huku zenyewe zikifanya vizuri, ni dhahiri Tanzania itapoteza nafasi ya timu nne msimu ujao.

Hivyo, kinachotakiwa kwa sasa, wakati Simba ikiendelea na maandalizi yake ambayo tunaamini yatakuwa makubwa, Watanzania kwa ujumla tunapaswa kuwa kitu kimoja kwa kuanza kuiombea katika maandalizi yake na hadi siku itakapocheza mechi hiyo nyumbani na zile za ugenini, tukitambua kwamba inalipigania taifa, hivyo kuisapoti mwanzo mwisho.

Tunatamani kuona Watanzania tukiweka pembeni itikadi zetu za kiklabu na kuwa kitu kimoja, na Nipashe tukiwa kama wadau namba moja wa michezo nchini, tunatambua ili kuwa na matarajio makubwa ya timu zetu kufanya vizuri hatuna budi kupigania kuingiza nne kwenye michuano hiyo inayoongoza kwa utajiri mkubwa kwa ngazi ya klabu barani Afrika.

Nipashe tunatamani kuona Watanzania wote tukiwa kitu kimoja Jumapili kuisapoti Simba hasa kwa kuingiza mashabiki wote 35,000 walioruhusiwa na CAF kuingia uwanjani kipindi hiki ambacho dunia inapambana na janga kubwa la maambukizo ya virusi vya corona.

Hata hivyo, ili CAF kuendelea kuruhusu mashabiki kuingia uwanjani kwa idadi kama hiyo ama zaidi, kila mmoja anapaswa kufuata masharti yalitolewa ya kutakasa mikono kabla ya kuingia uwanjani, kuacha nafasi moja ya kiti uwanjani kwa kukaa kinachofuata na kuvaa barakoa uwanjani hapo.

Lakini kubwa zaidi ni mashabiki sasa kubadili utamaduni wao wakupenda kushangilia pale timu yao inapopata bao ama mchezaji anapopiga chenga na badala yake kushangilia mwanzo mwisho jambo ambalo litawaongezea ari ya kupambana mwanzo mwisho wa mchezo.

Habari Kubwa