Maandalizi mashindano CHAN yasiwe zimamoto

06Jul 2019
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Maandalizi mashindano CHAN yasiwe zimamoto

SOKA ni moja ya mchezo ambao unachezwa kwa kalenda inayozunguka, ambapo wadau na familia ya mchezo huo unaopendwa zaidi duniani huita msimu.

 

Kumalizika kwa msimu mmoja, ni mwanzo wa maandalizi ya msimu unaofuata, iwe ni wa mashindano ya ngazi ya wilaya, kitaifa au kimataifa.

Wakati kiuhalisia, msimu au kalenda ya Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon 2019), bado inaendelea huko nchini Misri, timu ya Tanzania maarufu Taifa Stars yenyewe imeshatolewa katika mashindano hayo.

Fainali hizo sasa zimeingia katika hatua ya 16 Bora, na katika Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati (Cecafa), ni timu moja tu ambayo ni  Uganda (The Cranes), ndiyo ilifanikiwa kutinga hatua hiyo.

Vigogo hao wa Cecafa, jana usiku walikuwa wakivaana na wenyeji, Misri na endapo watafanikiwa kusonga mbele, watakuwa wamejiweka kwenye nafasi nzuri zaidi, baada ya kufanya vibaya katika fainali mbili zilizopita.

Tukirudi hapa nyumbani, Taifa Stars imesharejea nchini na sasa inatakiwa kujiandaa kusaka tiketi ya kushiriki Fainali za Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN), ambapo nchi zitakazokuwa zimefuzu, zitachuana hapo mwakani.

Taifa Stars ambayo haitakuwa na nyota wake wanaocheza soka la kulipwa katika nchi mbalimbali hapa ulimwenguni, akiwamo nahodha, Mbwana Samatta, ambaye anaichezea KRC Genk ya Ubelgiji.

Katika kampeni ya kuwania tiketi ya mashindano hayo, Taifa Stars ambayo iko chini ya Kocha Mkuu Mnigeria Emmanuel Amunike, imepangwa kuanza na Sudan, na itaanzia nyumbani huku mchezo wa marudiano ukitarajiwa kuchezwa mjini Khartoum.

Ili Taifa Stars iweze kupeperusha vema bendera ya Tanzania, zinahitajika juhudi za kweli katika kuwandaa wachezaji wa timu hiyo kimwili na kifikra. Hii inatokana na wachezaji hao kutoka kusikia maneno ya kukatishwa tamaa baada ya kupata matokeo mabaya katika mechi za Afcon.

Wachezaji wa Taifa Stars wanatakiwa kupewa muda unaofaa kujiandaa na mchezo huo wa kwanza dhidi ya Sudan, lakini pia wakizingatia muda wa kupumzika baada ya kumaliza msimu uliopita.

Benchi la ufundi linatakiwa kutoa programu zake ambazo zitasaidia kuwainua wachezaji hao, katika kupambana kuwania nafasi hiyo muhimu.

Nipashe inaamini kwamba, kalenda ya mashindano haya haikuwa kwa kushtukiza, TFF na Idara yake ya Ufundi, iliyafahamu na sasa wanachotakiwa kukifanya ni kuendeleza pale walipoanza kabla ya kikosi kamili kwenda Misri kushiriki Afcon.

Gazeti hili linapenda kuwakumbusha wadau kwamba, soka ni mchezo wenye matokeo ya aina tatu ambayo ni kushinda, kutoka sare au kufungwa kama mnacheza mechi za ligi, au kushinda pamoja na kushindwa kwenye michezo ya mtoano.

Hivyo basi, pamoja na maandalizi yote hayo, ni lazima tukubali kuwa sisi ni wanamichezo, pale tunaposhuhudia timu yetu imepoteza mchezo, na mpinzani akisonga mbele.

Ni vema kwa kila mmoja kukubali kuheshimu matokeo na vile vile kukubali mapendekezo ambayo yanatolewa na walimu wa timu husika, kwa sababu mwisho wa siku, Nipashe inaamini kwamba hakuna kocha ambaye anapenda kuona kikosi chake kinafungwa kwa sababu, matokeo hayo huhatarisha ajira yake.

Naamini kupata nafasi ya kushiriki Fainali za CHAN, kutatoa fursa nyingine kwa wachezaji wa Tanzania kutangaza vipaji vyao kwa mawakala mbalimbali kutoka ndani na nje ya bara la Afrika.

Tayari, Taifa Stars imekaa miaka 11, tangu iliposhiriki kwa mara ya kwanza Fainali za CHAN mwaka 2008, tunaamini safari hii itapambana ili kurejea mapema na si kusubiri hadi miaka 39 kama ilivyorejea kwa mara nyingine kwenye Fainali za Afcon.

 

Habari Kubwa