Maandalizi mazuri ni muhimu kwa Mahakama ya Mafisadi

29Jun 2016
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Maandalizi mazuri ni muhimu kwa Mahakama ya Mafisadi

VYOMBO vya dola kupitia Jukwaa la Haki Jinai, vilikutana kwa siku mbili mjini Dodoma juzi na jana kwa ajili ya kupanga mikakati ya kuanzisha Mahakama Maalum ya Mafisadi.

Serikali ilishaahidi kwamba mahakama hiyo itaanzishwa rasmi mwezi ujao, kwa lengo la kushughulikia kesi zote za rushwa na zinazohusiana na mambo ya ufisadi.

Kuanzishwa kwa mahakama hiyo kunatokana na ahadi iliyotolewa na Rais John Magufuli wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana na katika hotuba yake ya kulizindua Bunge la 11.

Mkutano huo wa vyombo vya dola wa kupanga mikakati ya kuanzisha chombo hicho ni ishara sasa kwamba maandalizi yameanza rasmi. Na hilo limefanyika baada ya Bunge la Jamhuri ya Muungano kupitisha sheria ya uanzishwaji wa mahakama hiyo.

Waziri wa Katiba na Sheria, Dk. Harrison Mwakyembe, alisema mkutano huo iliitishwa ili kuandaa mpango wa kuhakikisha mahakama hiyo inafanya kazi kwa ufanisi na washiriki walikuwa ni viongozi wa taasisi ambazo ziko kwenye mfumo wa haki jinai ambazo ni Jeshi la Polisi, Usalama wa Taifa, Mahakama, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) na ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP).

Kufanyika kwa mkutano huo ni hatua nzuri na inaonyesha kwamba Serikali iko makini na inatekeleza ahadi yake ya kuanzisha mahakama hiyo kwa ajili ya kushughulikia vitendo vya ufisadi, ambavyo vimechangia kwa kiasi kikubwa kukwamisha maendeleo ya nchi yetu.

Baada ya kupata Uhuru, nchi yetu ilitaja maadui watatu wa maendeleo kuwa ni ujinga, umaskini na maradhi. Hata hivyo, jitihada kadhaa zilizofanyika kuwaangamiza maadui hao zilikwama kutokana na kuibuka adui mpya na mbaya zaidi ambaye ni ufisadi.

Tunaunga mkono juhudi zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano za kupambana na kansa ya ufisadi ikiwamo ya kuanzishwa kwa Mahakama ya Mafisadi, ambayo tunaamini kuwa itapunguza ukubwa wa tatizo hilo na kuiwezesha nchi yetu kupaa kimaendeleo.

Tunachoshauri ni kwamba kabla ya kuanzishwa kwa mahakama hiyo, yanahitajika maadalizi mazuri yatakayoiwezesha kutekeleza majukumu yake kwa tija na ufanisi mkubwa.

Kuzikutanisha taasisi za dola ni moja ya hatua nzuri ya maandalizi kwa kuwa taasisi hizo zitatakiwa kufanya kazi kwa pamoja ili kuharakisha na kufanikisha mashauri yote ya ufisadi.

Maandalizi mengine ambayo Serikali hainabudi kuyazingatia ni kutengwa fedha za kutosha kwa ajili ya uendeshaji wa mahakama hiyo. Kama haitatengewa fedha za kutosha itakuwa vigumu kuendesha mashauri na kuyamaliza kwa wakati mwafaka.

Mahakama hiyo pia itahitaji watumishi wa kutosha wakiwamo majaji kwa kuwa zitakuwapo kesi nyingi ambazo zitahitaji kumalizwa haraka. Kwa kuwa kesi nyingi za ufisadi zina mvuto kwa watu wengi, itakuwa vizuri kama mahakama hiyo itawekwa katika eneo kubwa na tulivu.

Aidha, kuna haja ya kuhakikisha bila kuacha shaka yoyote kwamba watumishi watakaopewa fursa ya kufanya kazi katika mahakama hiyo wakiwamo majaji, waendesha mashtaka na wapelelezi ni watu waadilifu wasiokuwa na chembe yoyote ya ufisadi kwani kinyume chake mahakama hiyo itapoteza lengo la kuanzishwa kwake.

Tunashauri pia kwamba litakuwa jambo la busara kama Serikali itatoa fursa kwa wananchi au asasi kadhaa kutoa maoni, ushauri na mapendekezo yao kuhusiana na namna bora ya kuianzisha na kuiendesha mahakama hiyo. Njia hiyo shirikishi itasaidia kupata mawazo mapana na mazuri yatakayowezesha kunzishwa kwa chombo kizuri.

www.guardian.co.tz/circulation

Habari Kubwa