Maandalizi michuano ya chalenji Kilimanjaro Boys, Queens yalingane

04Nov 2017
Mhariri
Nipashe
Maandalizi michuano ya chalenji Kilimanjaro Boys, Queens yalingane

ALHAMISI wiki hii Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), lilitangaza limethibitisha kwa timu zake mbili zitashiriki katika mashindano ya kuwania Kombe la Chalenji kwa nchi za Afrika Mashariki ambayo yatafanyika mwaka huu baada ya kusimama kwa miaka miwili.

Michuano hiyo ambayo itashirikisha nchi wanachama 12 na wageni wawili ambao ni Zimbabwe na Libya walioalikwa inatarajiwa kufanyika kuanzia Novemba 25 hadi Desemba 9 mwaka huu jijini Nairobi, Kenya.

Nchi wanachama wa Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki (CECAFA) ni pamoja na Tanzania Bara, Zanzibar, Burundi, Ethiopia, Rwanda, Sudan, Sudan Kusini, Eritrea, Somalia , Djibouti, Uganda na wenyeji Kenya.

Katika mashindano hayo ambayo hushirikisha timu za wakubwa, Tanzania Bara itawakilishwa na timu ya Kilimanjaro Herouse kwa upande wa wanaume na Kilimanjaro Queens kwa wanawake. Kilimanjaro Queens ndio mabingwa watetezi.

Ili wawakilishi hao waweze kufanya vizuri na kurejea nyumbani na vikombe, wanahitaji kupata maandalizi bora na yanayofanana kwa sababu wachezaji wote wanakwenda kufanya jukumu linalofanana la kupeperusha bendera ya nchi.

Kama ni kuingia kambini kuanza kujifua zinatakiwa zote zipate maandalizi bora na TFF inatakiwa kutekeleza mapendekezo ya programu za makocha bila ya kuwapo na upendeleo wa aina yoyote kwa sababu mwisho wa michuano Watanzania wanataka kuona vikombe vya ubingwa vinatua kwenye ardhi yao.

Tayari kikosi cha Taifa Stars ambacho ndio hicho hicho kitakachogeuka na kuwa Kilimanjaro Queens kwa sababu hakina wachezaji wa Zanzibar, kinatarajia kuingia kambini kujiandaa na mchezo wa kirafiki dhidi ya Benin ambao utafanyika Novemba 11 mwaka huu.

Mchezo huo utachezwa zikiwa zimesalia wiki mbili kabla ya kuanza kwa mashindano ya Chalenji, lakini pia Kilimanjaro Herouse inaundwa na wachezaji wengi wanaocheza Ligi Kuu Tanzania Bara ambayo sasa imeingia raundi ya tisa. 

Hii inamaana kuwa nyota hayo wataingia katika michuano hiyo ya CECAFA wakiwa imara na tayari kukabiliana na ushindani kutoka katika timu pinzani.

Hali iko tofauti na kwa upande wa wanawake ambao wao hawana mchezo wowote wa kirafiki wa kimataifa au wa hapa ndani, lakini wanatarajiwa kuibeba Tanzania kwenye michuano hiyo itakayofanyika kwa mara ya pili.

Vile vile inategemea wachezaji ambao bado wanasubiri msimu wa 2017/18 uanze, Ligi Kuu ya Wanawake Tanzania imepangwa kufanyika kuanzia Novemba 26 mwaka huu na itaanza kwa hatua ya makundi na baadaye itachezwa Nane Bora.

Mwaka jana Kilimanjaro Queens ilisafiri kwa kusuasua kutoka Dar es Salaam mpaka Bukoba, mkoani Kagera na baadaye kuelekea mjini Jinja, Uganda kupambana na hatimaye wakaibuka kidedea wakifanya vizuri na kuzishinda nchi nyingine sita zilizokuwa zinawania kikombe hicho.

Uongozi mpya wa TFF ulioingia madarakani Agosti 12 mwaka huu chini ya Rais, Wallace Karia kama ambavyo imedhamiria kuleta maendeleo katika soka la vijana na wanawake, huu ndio wakati wa kuonyesha kwa vitendo yale uliyokuwa unayanadi wakati wa unatambulisha sera zako 11 wakati wa kampeni.

Ni vyema mabadiliko ya kuandaa timu za wanawake yakaonekana kwa vitendo na kusahau kuiandaa Kilimanjaro Queens au Twiga Stars kwa mazoea au zimamoto.

Ni wazi kuwa Twiga Stars na Ligi ya Wanawake haina wadhamini, kinachofanyika sasa ni jitihada za hali na mali ili kuitunza timu hiyo, msichoke, kama uwekezaji ulioko kwa wanaume ukiwekwa japo robo kwa wanawake, hakika tutarajie kuona mazuri zaidi ya haya yanayoonekana sasa.

Nipashe inaamini kuwa hakuna mafanikio yanayoweza kupatikana kwa njia ya miujiza, soka linahitaji maandalizi na kamwe halina njia ya mkato ili kufikia zilizo nchi zilizoendelea kama Nigeria, Misri au jirani zetu Uganda ambao timu yao ya Taifa ya wanaume imekuwa katika kiwango cha juu hivi karibuni.

Gazeti hili linawatakia kila la kheri katika kufikia malengo katika utawala uliopo ili baada ya miaka minne itakapomalizika warudi kwa wapiga kura wakiwa wanacho cha kujisifia.

Habari Kubwa