Maandalizi safari ya AFCON 2019 yaanze sasa

12Sep 2016
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Maandalizi safari ya AFCON 2019 yaanze sasa

SOKA ni mchezo ambao mafanikio yake hayapatikani kwa njia ya mkato zaidi ya wahusika kuwekeza kikamilifu.

Mapema mwezi huu, mataifa ya Afrika yalishuka dimbani kusaka tiketi ya kushiriki fainali zijazo za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) Januari mwakani nchini Gabon.

Wababe 16 walipatikana, hivyo kuanza maandalizi ya kushiriki fainali hizo zinazoandaliwa kila baada ya miaka miwili na Shirikisho la Soka Afrika (CAF).

Lakini wakati timu nyingine zikishuka dimbani kuamua hatima yao katika ushiriki wa fainali hizo, timu ya Tanzania (Taifa Stars) yenyewe ilikuwa ugenini Nigeria ikiwavaa wenyeji Super Eagles, mechi hiyo kwa pande zote mbili ilikuwa ni ya kukamilisha ratiba.

Hiyo ilitokana na kinara wa Kundi G Misri (Mafarao) kuwa na pointi 10 wakati Super Eagles ikishuka dimbani kuikaribisha Taifa Stars ikiwa na pointi mbili. Taifa Stars yenyewe ilikuwa na pointi moja.

Kwa maana hiyo, timu hizo mbili zilikuwa zinakamilisha ratiba kutokana na matokeo yoyote kutoathiri msimamo wa kundi hilo lililobakia na timu tatu kutokana na Chad kujitoa kwenye michuano.

Hayo yamepita, lakini Nipashe tunaamini kuna mahali Tanzania ilikosea na kupitia ripoti ya benchi la kiufundi la timu hiyo iliyoko chini ya Boniface Mkwasa, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) itaanza kuifanyia kazi mapema.

Huku Tanzania ikiwa na ndoto za kuandaa na kushiriki fainali za vijana za Afrika mwaka 2019, pia maandalizi ya michuano ya fainali za AFCON 2019 yanatakiwa yaanze sasa.

Moja ya jambo la msingi ambalo TFF inatakiwa kulifanyia kazi ili kufanya vizuri kwenye michuano hiyo ni kuhakikisha inajipanga vizuri.

Tayari Mkwasa ambaye aliacha ajira yake Yanga na kujiunga na Taifa Stars ameshatangaza nia yake ya kuachana na timu hiyo mkataba wake utakapomalizika Machi 31 mwakani, hapo ndipo TFF inapotakiwa kujipanga kwa kufahamu itaanzaje 'safari' mpya ya AFCON 2019.

Hatua hiyo itasaidia kumpa nafasi Mkwasa kama ataendelea kuinoa timu hiyo au kocha mpya kuanza kusuka upya kikosi kuelekea mashindano hayo.

Sio mbaya kama TFF ikameza 'matapishi' yake kwa kumrejesha Kim Poulsen ambaye naye alikuwa na programu ya kusuka sura mpya kama ambazo zimemsaidia Mserbia, Sredojovi Milutin 'Micho' kuipeleka Uganda kwenye fainali za AFCON mwakani.

Kim aliaminika kuwa anaweza kutimiza ndoto za Watanzania, lakini yaliyotokea yametokea, huu ni wakati wa kufikiria kutekeleza programu za maendeleo kwa kuhakikisha Taifa Stars inashiriki fainali hizo.

Huku TFF ikijipanga kusaka njia ya kwenda AFOCN 2019, pia wadau wa soka wajitokeze kuisaidia timu ya vijana ya umri chini ya miaka 17 (Serengeti Boys) iliyobakisha mechi mbili dhidi ya Congo Brazzaville ili kufuzu.

Habari Kubwa