Maazimio ya mawaziri 8 yatekelezwe kwa vitendo

01Jul 2021
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Maazimio ya mawaziri 8 yatekelezwe kwa vitendo

JUZI mawaziri wanane waliweka bayana mkakati wa pamoja katika kukabiliana na kelele nyumba za ibada na maeneo ya starehe, huku wakiweka adhabu kali, ikiwamo kufunga biashara au eneo husika ambalo ni kero kwa waliolalamika.

Adhabu iliyopo kwenye Sheria ya Mazingira ni kifungo cha miezi sita jela na kufungiwa biashara kwa watu watakaobainika kusababisha kelele na mitetemo kwenye makazi ya watu hasa kwenye nyumba za ibada na starehe.

Mawaziri hao ni kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira); Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI); Ofisi ya Waziri Mkuu (UWEKEZAJI); Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto;

Wizara ya Viwanda na Biashara; Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia; Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makazi na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.

Waziri wa Mazingira, Selemani Jafo, alieleza mikakati mitano yenye lengo la kuondokana na hali hiyo, ikiwamo kutilia mkazo utekelezaji wa Kanuni za Usimamizi wa Mazingira za mwaka 2015.

Pia wamewataka wenye nyumba za ibada na maeneo ya starehe kuhakikisha shughuli zake hazisababishi kelele na mitetemo na sauti ziwe kwa kiwango kinachokubaliwa kisheria.

Hii ni habari njema sana kwa wananchi wengi wa maeneo ya mjini, ambao wameishi kwa mateso na usumbufu kwa muda mrefu, huku baadhi ya mamlaka zikitumia kama sehemu ya kujipatia fedha kwa kupokea rushwa hasa kwa wamiliki wa maeneo ya starehe.

Licha ya sheria kutaka kuwa inapofika saa sita usiku maeneo ya starehe kushusha sauti, lakini inakuwa kinyume kwa kuwa badala yake huzidisha.

Eneo gumu sana ambalo limekuwa kero, lakini viongozi wanaogopa kuligusa ni nyumba za ibada ambazo zinaanzishwa kila uchao kwenye makazi ya watu, na mara nyingi wanakuwa na mitetemo mikubwa kiasi cha kulazimu waliopo jirani kutolala usiku kucha.

Kwa sasa watu wanabadili makazi yao na kuanzisha makanisa kwa ajili ya kumwabudu Mungu. Ni jambo jema, lakini katika ibada hizo isiwe kero kwa wengine, ni lazima kusheshimu wengine kwa kuwa hata Mungu ameagiza binadamu kuheshimu wengine na kuishi kwa upendo.

Ni muhimu mkakati huu wa mawaziri wanane ukawa kwa vitendo na ufuatiliaji usiwe wa kueleza umma tu na kumaliza, kwa kuwa hakuna ubishi kelele ni kero kubwa sana hasa nyakati za usiku katika maeneo ya watu. Kutoa taarifa halafu mamlaka kukaa kimya, ni jambo linaloonyesha kuna rushwa.

Mathalani, wakazi wa Banana Wilaya ya Ilala, Dar es Salaam wanaishi kwa taabu kwa kuwa kuna baa tatu sugu na nyumba za ibada kwa kupiga muziki na ibada hadi asubuhi, na mbaya zaidi mamlaka za serikali zinajua, lakini hatua hazichukuliwi. Hawa ni mfano kati ya wengi.

Ni muhimu hatua mahususi zikachukuliwa kwamba mtu kabla hajapewa kibali cha kuanzisha nyumba ya ibada au eneo la starehe, awe amekidhi vigezo vyote na afuatiliwe kwa karibu kwa kutumia mamlaka za serikali za mitaa na Polisi, kuhakikisha anafuata masharti ya leseni au kibali chake.

Ikiwa hali itaachwa hivi, kuna hatari kubwa ya kujikuta uchumi unatikiswa na watu kushindwa kufanyakazi, mzigo wa matibabu kwa watu ambao hawapumziki.

Hata kama watu hawa wana haki ya kikatiba ya kuabudu, lakini ni vizuri wafanye hayo bila kuwa kero kwa wengine, hata kama nchi inataka kodi kutokana na biashara, lakini wasikwaze walipakodi wengine.

Tunapaswa kujifunza kwa nchi zilizoendelea, ambazo huwezi kukuta baa na nyumba za ibada ni kero kwa watu, kwa kuwa zimejengwa kwa muundo wa kuhakikisha sauti inabaki ndani kwa ndani.

Ikiwa mamlaka za serikali zitashirikiana kikamilifu maana yake kero hii itaondoka, lakini Wizara ya Mambo ya Ndani inapaswa kufuatilia kwa karibu.

Pia Wizara ya Ardhi wanaotoa vibali vya kubadili matumizi ya eneo husika ni muhimu kufuatilia kwa kina kabla ya kufanya uamuzi.

Hata Mungu alisema asiyefanyakazi asile na anataka watu wafanyekazi ili wapate fedha walipe kodi. Na ndiyo maana kwenye Biblia inaelezwa kuwa ya Kaisari mpe Kaisari na ya Mungu mpe Mungu.

Habari Kubwa