Mabango ya wananchi liwe funzo kwa viongozi

20Dec 2016
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Mabango ya wananchi liwe funzo kwa viongozi

ZIARA ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, mkoani Arusha imebainisha kitu ambacho viongozi wetu wa umma hawanabudi kujifunza.

Wakati akipita katika maeneo mbalimbali ya mkoa huo, Majaliwa alishtuka kuona wananchi wakibeba mabango yaliyokuwa yakieleza kero mbalimbali zinazowapata.

Waziri Mkuu kwa kutumia busara zake alibaini kuwa njia hiyo ya wananchi kutumia mabango kueleza kero zao inatokana na viongozi wao kutowasikiliza na kuwapa fursa ya kuwaeleza kero zao ili wazitafutie ufumbuzi.

Kutokana na matukio ya wananchi kutumia mabango kueleza changamoto mbalimbali zinazowakabili, Majaliwa alisema wananchi kutumia mabango kueleza kero zao ni ushahidi kwamba watendaji na madiwani hawawapi nafasi ya kueleza shida zao.

Majaliwa alisema kwa kutambua hawana nafasi ya kuuliza maswali, wananchi walitumia mabango katika kila mkutano aliohutubia ili kutoa waliyonayo moyoni.

Akizungumza katika mkutano wa kuhitimisha ziara yake mkoani Arusha, Waziri Mkuu alisema ni wazi kuwa viongozi wa serikali ngazi ya wilaya, kata na vijiji hawaandai mikutano na kuzungumza nao na kwamba kama wangekuwa wanaandaa mikutano ya hadhara, wananchi wasingeomba kujua lini watapata kiwanja cha kujenga kanisa lao mbele ya yake katika moja ya mikutano yake ya hadhara.

Baada ya kulibaini hilo, Waziri Mkuu alisema ni matarajio yake kuwa ziara yake itaamsha ari ya viongozi na watendaji wakiwamo madiwani kutenga muda wa kuzungumza na wananchi katika maeneo yao na kuzitafutia ufumbuzi kero zao.

Tumefurahishwa na wepesi wa Majaliwa kulibaini hilo kwa sababu kuna tabia iliyojengeka kwa muda mrefu kwa viongozi katika maeneo kadhaa nchini kufanya kazi kwa mazoea.

Viongozi wa aina hiyo wanajifungia ofisini badala ya kwenda kwa wananchi kusikiliza maoni yao pamoja na kero zinazowakabili. Aidha, viongozi wa aina hiyo wanapokwenda kuzungumza na wananchi wanakwenda na ajenda zao za kuwaeleza bila kutoa fursa kwao kueleza masuala yao.

Matumizi ya mabango ni njia mpya inayoonyesha kwamba jamii imebadilika kutokana na uelewa wa kudai haki zao, pale wanapoona viongozi wenye dhamana kwao hawatekelezi wajibu wao ipasavyo kwa kuwasikiliza na kuwatatulia kero.

Tunampongeza Majaliwa kwa kuonyesha mtazamo chanya kuhusiana na njia waliyoitumia wananchi kumueleza kero zao na kuwakumbusha viongozi wajibu wao wa kuwasikiliza.

Tunaamini kuwa mabango yatawafanya viongozi waliokuwa wamejisahau kutekeleza wajibu wao wa kushughulikia matatizo ya wananchi watarejea katika mstari ili wasiumbuke mbele ya viongozi wakuu wa nchi watakapofanya ziara katika maeneo yao na kukutana na mabango ya wananchi.

Tabia ya viongozi kutowatembelea wananchi na kupokea kero zao ndiyo iliyochangia kwa kiasi kikubwa changamoto mbalimbali ambazo zimekuwa zikiyakabili baadhi ya maeneo ya nchi yetu ikiwamo migogoro ya ardhi.

Mwamko wa wananchi na uelewa wa kudai haki zao umetokana na elimu ambayo imekuwa ikitolewa na asasi mbalimbali na tunapongeza mchango wao ulioleta mabadiliko chanya kwa jamii yetu.

Tunawashauri wananchi kutoogopa kuwaeleza viongozi kero zao na inapotokea baadhi wakawapuuza, watumie njia ya mabango kama walivyofanya wenzao wa Arusha na kufikisha ujumbe kwa Waziri Mkuu.

Habari Kubwa