Mabilioni ya TASAF yaonyeshe uhalisia maisha ya wanufaika

21Oct 2021
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Mabilioni ya TASAF yaonyeshe uhalisia maisha ya wanufaika

HIVI karibuni Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF), ulieleza umma kuwa umepokea Sh. bilioni 5.5 kama fedha za masharti nafuu kutoka Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) kwa ajili ya kutekeleza mpango wa maendeleo kwa ustawi wa taifa na mapambano dhidi ya UVIKO-19.

Wanufaika wa fedha hizo ni kaya 40,740 waliopo kwenye mpango wa kunusuru kaya maskini kwenye miji na majiji, ambao walipata athari ya UVIKO-19 katika shughuli zao.

Mradi wa kunusuru kaya maskini ni katika halmashauri 184 Tanzania Bara, Unguja na Pemba zenye kaya milioni 1.4 zenye watu milioni 10 wanaotoka kwenye mazingira magumu, wanaopatiwa ruzuku ya kujikimu, kufanya kazi kwenye miradi ya jamii na kulipwa ujira ambao unaziongezea kipato na kuunganishwa kwenye vikundi vya kujiwekea akiba.

TASAF imesema imejipanga kuhakikisha utekelezaji wa miradi ya ajira za muda kwa walengwa wa mpango unaanza haraka, na kutakuwa na ufuatiliaji wa karibu. Tunapongeza uamuzi wa kusaidia wananchi maskini ili kuwatoa kwenye umaskini na kupunguza idadi ya watu wanaoishi kwenye hali ngumu, ambao watamudu mahitaji ya familia zao na kuchangia uchumi wa nchi.
 
Tunatarajia fedha hizi zitatumika ipasavyo ili tathmini itakapofanyika ionyeshe namna gani mradi hiyo ilibadili maisha ya walengwa kama ilivyokuwa TASAF I na II, ambazo zilijenga vyumba vya madarasa, nyumba za walimu, zahanati, vituo vya afya na miundombinu ya barabara kulingana na kipaumbele cha wakazi wa eneo husika.

Kwenye miradi hiyo wananchi walichangia nguvu kazi ya asilimia 20 na TASAF ilitoa asilimia 80 ya fedha za mradi, na hadi sasa ipo kwenye vijiji mbalimbali na manufaa yake yanaonekana.

Ni muhimu fedha nyingi iwafikie walengwa na miradi ionekana na siyo kutumika kwenye shughuli za uendeshaji ambazo nyingi ni kulipa mishahara, posho na gharama nyingine kama za malazi na nauli.
 
Tunatambua kuna watu wanaowajibika wanapaswa kulipwa, lakini ni vyema itakapofanyika tathmini basi wanufaika waonekane kunufaika na mradi hiyo, na iwe imewavusha katika hali za maisha kutoka hali walizokuwa nazo awali. Ni muhimu Sh. bilioni 5.5 zikaonekana kwenye maisha ya watu na mabadiliko yaonekane kuliko familia hizo kuendelea kubaki katika hali ngumu.

Moja ya miradi wanayofanya wanufaika wengi ni ufugaji wa kuku, sawa ni mradi mzuri, lakini ni lini ufugaji wa kuku wawili au watatu utamchomoa mtu kwenye umaskini, akaweza kutimiza mahitaji ya familia yake?

Wengine wanaanzisha kuuza bidhaa mbalimbali ambazo kimsingi bado hazileti matokeo makubwa kwenye maisha yao, kwa kuwa wanatakiwa kutunza familia zao kwa mahitaji ya msingi kama kusomesha watoto na kulipia huduma nyingine.

Tunatarajia kuona wanufaika wanajivunia kiuhalisia mabadiliko ya maisha yao, kwamba mtu alikuwa hawezi kusomesha wanawe sasa analipa ada au anaweza kujilipia gharama za matibabu.
 
Ikiwa fedha nyingi kati ya hizo zitatumika kugharamia shughuli za uendeshaji, maana yake fedha kiduchi ndizo zitakwenda kwa walengwa, ambao wanapaswa kuonyesha mabadiliko na kuondoka kwenye mstari wa umaskini.

Habari Kubwa