Madeni ya NSSF na NHIF yalipwe mifuko ijiendeshe

22Feb 2022
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Madeni ya NSSF na NHIF yalipwe mifuko ijiendeshe

MWISHONI mwa wiki Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), iliitaka serikali kuweka mkakati madhubuti wa kulipa madeni ya Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), kwa kuwa yanaathiri utekelezaji wa majukumu yake.
 

Aidha, kamati hiyo ilisema hadi Juni 30, mwaka 2020 deni la NSSF lilifikia Sh. trilioni 1.174 ambalo lilipatikana kwa kuanzia mwaka 2007 hadi mwaka huo.
 
Kwa NHIF deni lilifikia Sh. bilioni 209.70, huku kamati ikisema kuwa pamoja na kupunguza ufanisi wa mifuko husika, lakini yanaharibu taratibu za mizania ya fedha kinyume na kanuni za kimataifa za uandaaji wa hesabu.
 
Kwa ujumla madeni hayo yamesababisha mifuko kushindwa kutimiza majukumu yake kisheria kwa ufanisi kwa wakati.
 
Kamati hiyo ilipongeza serikali kwa kuanza kulipa deni la Mfuko wa Pensheni kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) la Sh. bilioni731 ambalo hadi Juni mwaka 2021 zililipwa Sh. bilioni 500 na mwaka huu, wametoa hati fungani maalum isiyo taslimu yenye thamani ya zaidi ya Sh. trilioni 1.176.
 
Majukumu ya NSSF ni kutunza michango ya wanachama wa sekta binafsi na isiyo rasmi kama wavuvi, wafugaji, wajasiriamali, wachimbaji na wengineo.
 
Kwa mujibu wa Sheria ya NSSF na marekebisho ya mwaka 2018, mwanachama aliyetimiza matakwa ya kikanuni anapata pensheni ya uzeeni, pensheni ya urithi, pensheni ya ulemavu, fao la upotevu wa ajira, bima ya afya, mafao ya uzazi, msaada wa mazishi.
 
Ili mafao yote yaweze kutolewa kwa wakati ni lazima mfuko uwe na fedha, inapotokea sasa fedha nyingi ziko serikalini na nyingine zimewekezwa kwenye miradi ambayo baadhi inalalamikiwa kwa kuwa haijaweza kutimiza lengo la uanzishwaji wake, wanaoumia ni wanachama.
 
Mathalani, kumekuwa na malalamiko ya watu kuachishwa kazi na kutolipwa fao la ukosefu wa ajira, fao la uzazi na pensheni zao kwa wakati, wengine wakisotea miaka na miaka bila sababu kuelezwa.
 
Kwa upande wa NHIF, kazi yake ni kuhakikisha wanachama wanapata bima ya afya na matibabu pale wanapokwenda kwenye maeneo husika.
 
Kwa muda mrefu kumekuwa na kilio cha Bima ya Afya kwa wote, imekuwa ni ombi la wabunge kwa serikali ipeleke Muswada wa Sheria ya Bima ya Afya kwa wote na imesema iko katika hatua nzuri na utakapokamilika utapelekwa kwenye muhimili huo.
 
Ni muhimu serikali ikalipa madeni hayo kwa wakati, ili kurahisisha upatikanaji wa mafao kwa wanachama wa mifuko, bila kufanya hivyo ni kukwaza utendaji na wanaoumia ni wanachama wenyewe.
 
Kama ambavyo madeni ya PSSSF yameanza kulipwa basi utaratibu huo ufanyike kwa mifuko mingine, ili kusiwe na kusuasua kwa madai ya wanachama ambao kimsingi wanapaswa kunufaika na mifuko hiyo.

Kwa kufanya hivyo kutawafanya wanachama wa mifuko hiyo kuwa na imani nayo kwamba michango yao iko salama na kuwa na uhakika kupata mafao yao na pensheni kwa wakati mwafaka bila usumbufu wowote katika ufuatiliaji.

Ni matarajio yetu kwamba serikali itachukua hata haraka kuhakikisha madeni hayo yanalipwa ili mifuko hiyo ijiendeshe.
 

Habari Kubwa