Madereva watii sheria kukwepa faini trafiki

03Nov 2017
Mhariri
Nipashe
Madereva watii sheria kukwepa faini trafiki

KATIKA siku za karibuni pamekuwapo na kilio cha wadau wa usafiri na usafirishaji kwamba kiasi kikubwa cha makusanyo ya faini kinachopatikana kwa Kikosi cha Usalama Barabarani ni mradi na kwamba askari wanapaswa kukazania utoaji elimu.

Makusanyo ya faini za barabarani katika mkoa wa Dar es Salaam yaliongezeka kutoka Sh. bilioni 7.3 kwa kipindi cha kati ya Januari-Mei, 2016, hadi kufikia Sh. bilioni 12.8 kwa kipindi kama hicho mwaka huu.

Akizungumza jijini juzi, Kamanda wa Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani nchini, Fortunatus Musilimu alisema malalamiko ya wadau kuwa askari wake wameweka mkazo katika makusanyo badala ya elimu, hayana msingi kwa kuwa dereva yeyote mwenye leseni alikwishaelimishwa chuoni.

Kamanda Musilimu alisema pia kuwa hatua ya polisi kikosi cha usalama barabarani kutoza faini madereva wasiofuata sheria, si tu kimefanya madereva wazembe kuwa makini barabarani bali pia ajali kupungua nchi nzima.

Tuchukue nafasi hii, Nipashe, kuunga mkono msimamo wa Kamanda Musilimu kwa sababu kama alivyoeleza katika taarifa yake, ajali nchi nzima zimepungua.

Lakini pia, tuchukue nafasi hii, Nipashe, kuunga mkono msimamo wa Kamanda Musilimu kwa sababu faini hizi za 'trafiki' zipo kwa mujibu wa Sheria ya Usalama Barabarani ya mwaka 1973.

Wadau wa usafiri na usafirishaji, wanaopinga faini hizo na kupendekeza elimu kwa madereva walioingia barabarani tayari ni lazima wafahamu kuwa madhara ya ajali kitaifa, ni makubwa kiuchumi na kijamii kuliko kiasi chochote cha fedha ambazo kinaweza kukusanywa kama faini za barabarani.

Tunaomba wadau wa usafiri na usafirishaji watafakari hili:

Kwa mujibu wa taarifa ya Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Masauni Yusuf Masauni ya Septemba mwaka jana, katika kipindi cha miaka iliyoishia Desemba , 2015 abiria 3,444 walipoteza maisha kutokana na ajali za barabarani zilizoacha pia majeruhi 20,181.

Aidha, katika kipindi hicho, Masauni alisema, watembea kwa miguu 3,328 walikufa kwa kugongwa na wengine 8,256 wakiachwa majeruhi barabarani.

Makundi mengine ya watumiaji wa barabara yaliyoathirika vibaya katika kipindi hicho, ilielezwa ni wapanda pikipiki 2,493 waliofariki na ajali zake kuacha majeruhi 10,702.

Palikuwa pia na vifo 1,071 vya waendesha baiskeli na majeruhi 2,060 katika kundi hilo, na wasukuma mikokoteni 81 waliofariki na 246 kujeruhiwa.

Bila shaka, takwimu hizo za wizara, zinapaswa kuwaamsha wote wanaopinga makusanyo makubwa ya faini kuona kwamba walipaswa kuacha Kamanda Musilimu na vijana wake kote nchini wafanye kazi yao kwa amani na utulivu zaidi.

Lakini kama bado kutakuwa na wadau wa usafiri na usafirishaji wanaoona kwamba 'trafiki' wanakosea kutoza faini, walinganishe idadi ya vifo vya abiria, watembea kwa miguu, waendesha mikokoteni na baiskeli katika miaka mitatu hiyo ya 2013-15, na jumla ya vifo 813 tu vya madereva katika kipindi hicho.

Badala ya 'kulia lia', madereva watii sheria kukwepa faini trafiki, Nipashe tunasema.

Habari Kubwa