Madudu haya yataiweka elimu ya Tanzania kitanzini

27May 2016
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Madudu haya yataiweka elimu ya Tanzania kitanzini

MOJA ya changamoto ambazo zinazoikabili nchi yetu kwa sasa ni kushuka kwa kiwango cha elimu.

Zimekuwa zikitajwa sababu nyingi, lakini kuna mambo ambayo yamekuwa yakiibuliwa na kuonekana kuwa sababu kubwa zinazochangia kuporomoka kwa elimu nchini kuanzia msingi hadi vyuo vikuu.

Suala lililoibuliwa na hivi karibuni ni wanafunzi wa kidato cha nne waliofeli na kukosa sifa hata za kuendelea na elimu kwa ngazi ya cheti, kudahiliwa kusoma vyuo vikuu shahada ya kwanza ya ualimu.

Mbali na wanafunzi hao kutokuwa na sifa za kujiunga na elimu ya juu, pia walipewa mkopo wengi ikiwa ni wa asilimia 100, jambo lililoipa serikali hasara ya takriban Sh. milioni 700. Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia na Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako, ajuzi alisema kuwa Rais Dk. John Magufuli amemwagiza kuwasimamisha kazi watendaji wa Tume ya Vyuo Vikuu nchini (TCU) waliohusika na suala hilo.

Profesa Ndalichako alitangaza kumsimamisha kazi Profesa Yunus Mgaya, Katibu Mtendaji wa TCU; Dk. Savinus Maronga, Mkurugenzi wa Ithibati na Uthibiti Ubora; Rose Kiishweko, Mkurugenzi wa Udahili na Nyaraka na Kimboka Stambuli, Ofisa Msimamizi Mkuu wa Taarifa.

Alisema, wizara ilibaini kuwa wanafunzi 489 walidahiliwa katika matawi ya Songea na Arusha ya Chuo cha St. Joseph bila sifa za kusoma programu za chuo kikuu. Kwamba wanafunzi hao walidahiliwa kuchukua programu za chuo kikuu wakati hawajasoma Kidato cha Tano na Sita na hawakufaulu katika mitihani yao ya Kidato cha Nne.

Inashangaza kuona watu wasiokuwa na sifa za kujiunga na vyuo vikuu wakati kuna TCU ambayo jukumu lake la msingi ni kusimamia udahili wa wanafunzi katika vyuo vikuu vyote. Tukio hili ni ishara kwamba kuna madudu mengine mengi yanayofanyika na pengine kuwa sababu zaidi zinazosababisha elimu yetu iendelee kuporomoka kwa kasi kubwa.

Kama waliopewa dhamana ya kusimamia taasisi za serikali za kusimamia elimu wanashindwa kuwajibika katika utekelezaji wa majukumu yao na kusababisha watu wasio na sifa kujiunga na vyuo vikuu pamoja na kuisababishia hasara, basi tuna safari ndefu katika kufufua elimu na kutimiza malengo ya huko tuendako.

Tunasema hivyo kutokana na visheni ya Serikali ya Awamu ya Tano ya kutaka kuipeleka Tanzania katika uchumi wa kati kupitia viwanda. Hatuwezi kufika huko bila kuwa na wataalamu wa sayansi, taaluma inayohitaji wanasayansi wenye viwango vya ubora.

Dunia ya leo ni ya sayansi na teknolojia, hivyo, inashangaza kusikia kuna wanafunzi waliodahiliwa na TCU kusoma masomo ya sayansi, lakini walisoma masomo ya biashara katika shule za sekondari. Madudu hayo ndiyo yanayozua shaka kama tutafika katika nchi ya viwanda.

Kwa ujumla, yaliyobainishwa na Profesa Ndalichako ni aibu na fedheha kubwa kwa nchi yetu kwani tafsiri yake ni kwamba tunaelekea kutengeneza taifa la wajinga bila kujali kuwa ushindani miongoni mwa mataifa ni mkubwa na taifa litakaloshindwa kuhimili, halitasonga mbele.

Kwa mfano, ushindani katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), unawafanya Watanzania wawalalamikie Waganda na Wakenya wasiruhusiwe kuja kufanya kazi nchini. Hofu hiyo inatokana na kutokuwa na elimu ya kutosha kushindana nao.

Tunachotakiwa kufanya kama taifa, ni kutokubali kuruhusu madudu kama hayo yatokee pamoja na kuweka mifumo mizuri ya elmu na kuhakikisha wanaopewa dhamana ya kusimamia taasisi za elimu wawe watu weledi, wenye uwezo na uadilifu wa kutosha. Vinginevyo, tutaiweka elimu ya Tanzania kitanzini.

Habari Kubwa