Mafanikio yapo kwenye uadilifu

11Jun 2019
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Mafanikio yapo kwenye uadilifu

TUNAWAPONGEZA  Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Dk. Edwin  Nhende na Waziri wa Viwanda na Biashara, Innocent Bashungwa, kwa kupewa dhamana hizo za kuwatumikia Watanzania.

Wosia wetu kwenu ni kuwa na uadilifu na kusimamia kwa bidii zote watumishi ili wawe waadilifu.

Tunatoa wosia wa uadilifu kwa kuwa ndiyo msingi mkuu wa uongozi. Uadilifu ambao ndani yake kuna uaminifu mkubwa, uzalendo, hekima na hofu ya Mungu, ndiyo mambo yakuambatana nayo katika kufanyakazi.

Uadilifu tunaouzungumzia unamaanisha kusema na kuishi ukweli hata kama kufanya hivyo kutawaumiza.

Tunapenda kuwaambia kuwa mnasimamia taasisi nyeti za serikali, hivyo ni vyema kuwa waaminifu kulinda maslahi ya nchi kuliko kuhadaa na kudanganya ili kumnufaisha asiye na haki wala maslahi na taifa.

Tunawakumbusha kuwa hakuna kufanikiwa kwa mipango yoyote kama hakuna uadilifu. Mikakati ya kuondoa umaskini, kufikia Tanzania ya viwanda na yenye uchumi imara haitakamilika kama hakuna viongozi waadilifu.

Kama viongozi wa wizara nyeti yenye kushughulikia vitega uchumi, uwekezaji na biashara na kukuza uchumi wa nchi kwa upande wa Bashungwa na taasisi muhimu ya kusimamia mapato ya taifa ya TRA simamieni kila mnachokiamini ili mambo yafanyike kwa uadilifu, uzalendo na hofu ya Mungu.

Tunajifunza kuwa uadilifu na uzalendo, ndiyo unayoyafanya mataifa ya wenzetu hasa ya Asia kwa mfano Japan na China kuendelea kwa viwango vikubwa kwenye sekta zote, kung’ara kwenye sayansi na teknolojia kutokana na uchapaji kazi wa hali ya juu.

Tunajifunza kuwa Japan inasifika kwa falsafa yake ya Samurai, ambayo inahamasisha jitihada katika kazi, heshima na kuthaminiana, ushindani, uzalendo na uadilifu mkubwa yote hayo yameliwezesha taifa hilo kuwa la mfano.

Ni nchi iliyoendelea na inayoheshimika tena ni ya mfano kwenye uchapaji kazi na mafanikio kiuchumi, kisiasa na kiteknolojia.

Inasifika kwenye utengenezaji magari ya kila aina na mitambo ya kila aina, inaunda vifaa vya usafiri kwa teknolojia ya kisasa zikiwamo meli.

Si Wajapani pekee hata Wachina wanajulikana duniani kwenye uchapaji kazi, kujituma, utiifu, uadilifu, heshima na uzalendo kupitia falsafa ya Confucius.

Mataifa hayo yana maendeleo na yanajitahidi kuongeza ushindani na ufanyakazi kwa bidii na kujiepusha na kutekwa na hisia za ufisadi.

Maeneo mnayoyaongoza ni kama moyo wa taifa kama Rais John Magufuli, alivyowaagiza simamieni utendaji kazi.

Ondoeni kulindani, kubebana na kulea mafisadi wanaokwamisha maendeleo ya taifa.

Dokta Nhede, kama ambavyo umepewa rungu na Rais kwa kusisitiza kuongeza mapato na kusimamia utendaji kazi wenye tija ili kukusanya kodi, huku ukilinda vyanzo vya kodi, usikubali kurubuniwa na wachache ambao wanaifanya mamlaka hiyo kuonekana kama eneo la mafisadi.

Mara nyingi katika vikao vya Rais na wafanyabiashara TRA imekuwa ni eneo linalolalamikiwa mno.

Ni wakati wa kushirikisha wadau na kufanya utafiti ili kufahamu chanzo cha tatizo, namna ya kulirekebisha na mbinu za kutumia ili kurudisha heshima kwa taasisi hiyo.

Tunapomtakia Bashungwa kazi njema ya kuiongoza Wizara ya Viwanda na Biashara, tunamshauri kushirikisha wadau na kufanya tafiti zitakazosaidia kujua chanzo cha udhaifu na namna ya kuurekebisha.

Tunawakumbusha tena kuishi na kuuendeleza uzalendo na uadilifu ili mfanikiwe.

Habari Kubwa