Magereza isikilizwe wito kupunguza msongamano

02Jul 2021
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Magereza isikilizwe wito kupunguza msongamano

JESHI la Magereza limesema limeanza ujenzi wa magereza mapya na ngome kwenye magereza ya zamani, ili kukabiliana na msongamano wa mahabusu na wafungwa katika maeneo hayo.

Aidha, limesema kuna upungufu wa magereza katika wilaya 46 na tayari wamepata maeneo katika wilaya 26 kuwa na maeneo ya kuhifadhi watu hao.
 
Kwa mujibu wa Kamishna wa Jeshi la Magereza nchini, Seleman Mzee, fedha za kazi hiyo ipo ingawa hakutaja kiasi, na wataendelea kuimarisha ili kuhakikisha wanaondokana na msongamano.
 
Alidokeza kuwa jitihada za Rais katika kutoa msamaha kwa wafungwa kumesaidia kupunguza idadi ya wafungwa, na sasa anaziomba mamlaka nyingine kama Polisi, Mahakama na Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), kutimiza wajibu wao kikamilifu ili kupunguza msongamano.
 
Tatizo la msongamano wa wafungwa ni kubwa na limezungumzwa mara nyingi na aliyekuwa Rais wa awamu wa tano, Hayati John Magufuli, mara kadhaa alieleza nia ya kupunguza msongamano kwenye magereza.
 
Jambo hili ni tatizo kubwa hadi sasa na kuna jitihada zinafanywa na Ofisi ya DPP kwa kumaliza kesi kwa kufuta au kuondoa nia ya kuendelea na shauri husika, jambo ambalo linapunguza mahabusu.
 
Lakini wito wa Kamishna huyo ni muhimu kuzingatiwa na mamlaka nyingine ili kusaidia kuanzia polisi kufanya upelelezi kikamilifu, ili wanaofikishwa kwa DPP kwa ajili ya kupelekwa mahakamani wawe ni wahusika.
 
Vivyo hivyo, DPP naye afanye kazi yake kikamilifu kuangalia kama kuna kesi ya kujibu na kama ushahidi upo wa kutosha, ili kuepusha kuwa na watu wenye kesi za kawaida wanaosota ndani kwa muda mrefu na kuongeza mahabusu.
 
Ikiwa kutakuwa na ushirikiano au kila mamlaka kuwajibika ni wazi msongamano utapungua na magereza yatapumua, kutakuwa na hali bora maeneo hayo.
 
Uwapo wa mahabusu ni gharama kwa nchi kwa kuwa wafanyakazi wanaowalinda wanalipwa mishahara, marupurupu na mahitaji mengine, kulipa ankara mbalimbali za maji, umeme na majitaka pia kuwalisha, mavazi na viatu.
 
Licha ya magereza kutakiwa kujitegemea kwa maana ya chakula na mahitaji mengine kwa wafungwa kufanyakazi za uzalishaji bado hawajaweza kwa asilimia 100, na wamejikuta wanategemea fedha za serikali.
 
Lakini kwa mujibu wa sheria, mahabusu hawaruhusiwi kufanyakazi na hata wakifanya wanalindwa sana, jambo ambalo ni gharama sana, maana yake unakuwa na idadi kubwa ya watu wanaogharamiwa na kodi za Watanzania.
 
Lazima kuwe na mkakati wa kupunguza mahabusu kuanzia ngazi ya jamii, viongozi wa dini na mamlaka nyinginezo, vinginevyo ni kuendelea kubeba mzigo mkubwa wa kuhifadhi watu hao.

Pia ni vyema kasi ya ujenzi wa magereza ikaongezeka kwa kuzingatia kuwa kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi kuna Watanzania zaidi ya milioni 55, na mwakani itakapofanyika sensa nyingine kuna uwezekano mkubwa wa idadi hiyo kuongezeka zaidi.
 
Jitihada za pamoja zinahitajika katika kuhakikisha msongamano kwenye magereza nchini unapungua na wale ambao ni wafungwa wakatumika kwenye uzalishaji kwa ajili ya kuliwezesha jeshi hilo kujiendesha kwa gharama zake zenyewe.

Habari Kubwa