Magufuli aungwe mkono kusafisha chama tawala

14Aug 2016
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe Jumapili
Magufuli aungwe mkono kusafisha chama tawala

MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais John Magufuli ametangaza vita kali ndani ya chama chake. Ni vita ya kukikwamua chama hicho kikubwa zaidi nchini kutoka kwenye mikono ya wabadhirifu wa mali zake.

Lengo la mpango huo wa Rais Magufuli ni kuona kuwa chama chake kinanufaika na rasilimali tele zilizotapakaa nchini kote ili mwishowe kiepukane na aibu ya kubembeleza wafadhili ili wapate fedha za kufanikisha program zao, hasa wakati wa uchaguzi.

Kwa maelezo ya Rais Magufuli, ambaye alipokelewa kwa kishindo aliporipoti kwa mara ya kwanza kwenye Ofisi Ndogo ya Makao Makuu ya CCM jijini Dar es Salaam juzi, ni kwamba kuna watu wachache ndani ya jumuiya mbalimbali za chama hicho ndiyo hunufaika kutokana na fedha zinazoingia kila uchao. Wanaitumia CCM kujinufaisha huku wakikikondesha chama chao kiuchumi.

Akitolea mfano, Magufuli alizungumzia majengo makubwa ya maghorofa yanayomilikiwa na jumuiya zake na kunufaisha zaidi watu wachache badala ya CCM. Alitaja pia mfano wa ubadhirifu kwenye fremu za maduka katika viwanja vyake vya soka vilivyopo mikoa ya Mwanza na Ruvuma.

Aligusia pia viwanja zaidi ya 400 vinavyomilikiwa na CCM nchini lakini vyote hivyo vikinufaisha zaidi watu wachache na kukiacha chama hicho kikiwa ombaomba.

Magufuli aliahidi kuwa atapitia mikataba yote inayohusiana na mali za CCM, tena nukta kwa nukta ili kukomesha hali hiyo.

Sisi tunaona kuwa hatua zote alizozitangaza Magufuli katika kusafisha chama chake kutoka makucha ya ufisadi ni sahihi na zinapaswa kuungwa mkono na kila Mtanzania.

Sababu ya kusisitiza uungwaji mkono huo zipo nyingi, muhimu zaidi ikiwa ni kuhakikisha kuwa vita dhidi ya ufisadi inafanikiwa na kuiweka nchi mbali na athari za vitendo hivyo.

Ni imani yetu kuwa uadilifu unapotwaa nafasi ndani ya CCM, utasambaa pia katika maeneo mengine ya nchi. CCM ni chama tawala na hivyo, ni wazi kwamba taifa linaweza kuangukia mikononi mwa mafisadi ikiwa chama hicho kitaingia ubia wa aina yoyote ile na watu wenye sifa hizo.

Kwa mfano, ikiwa CCM itaendeleza desturi ya aibu anayoipinga Magufuli ya kuwaangukia wafadhili kufanikisha mambo yao, maana yake ikitokea mfanyabiashara wanayemfuata akawa si mwaminifu, atakuwa na jeuri kubwa ya kufanikisha maovu yake.

Ni kwa sababu mfanyabiashara asiye mwaminifu atajua fika kuwa hakuna ofisa wa Serikali atakayekuwa na ujasiri wa kumhoji.

Katika mazingira hayo, ni wazi kwamba miongoni mwa wafadhili wenye nia ovu ya kufanikisha miradi yao ovu, wanaweza kutumia mwanya huo kuifilisi nchi kwa namna mbalimbali.

Wafadhili wenye hulka za kifisadi, wanaweza kutumia kivuli cha misaada yao kwa chama tawala kufanikisha mbinu za ukwepaji kodi, kujihusisha na ujangili, dawa za kulevya na hata kuongoza makundi ya kihalifu.

Bila shaka, Rais Magufuli na vyombo vyake wanaijua hatari hiyo na ndiyo maana amepania kukiwezesha chama chake kusimamia rasilimali nyingi walizo nazo kwa maslahi ya CCM na siyo kikundi cha watu wachache.

Vinginevyo, endapo CCM itabaki kuwa ombaomba na kujikuta ikipata ufadhili wa watu wabaya, ni wazi kwamba madhara yake kwa taifa yatakuwa makubwa. Makusanyo ya kodi yatapungua na mwishowe Serikali itashindwa kutimiza malengo iliyojiwekea katika kusambaza huduma za kijamii kama afya, elimu na maji. Hapo, wakaoathirika siyo CCM peke yao bali Watanzania wote.

Shime, Rais Magufuli aungwe mkono katika mpango wake wa kuzuia ubadhirifu wa mali za chama tawala -- CCM.

Habari Kubwa