Mahakama imewezeshwa kwa fedha, tunatarajia kuona kazi

10Feb 2016
Mhariri
Nipashe
Mahakama imewezeshwa kwa fedha, tunatarajia kuona kazi

SABABU kubwa ambayo imekuwa ikitolewa kwa miaka mingi na Mahakama ya Tanzania kuwa ni kikwazo cha kutokamilisha mashauri kwa wakati, ni ufinyu wa bajeti.

SABABU kubwa ambayo imekuwa ikitolewa kwa miaka mingi na Mahakama ya Tanzania kuwa ni kikwazo cha kutokamilisha mashauri kwa wakati, ni ufinyu wa bajeti.

Mahakama imekuwa ikilalamikia miundombinu mibovu kama majengo ya mahakama, ukosefu wa vifaa na fedha kwa ajili ya kuwasafirisha pamoja na posho majaji na mahakimu kutoka eneo moja kwenda lingine kwa ajili ya kusikiliza mashauri na kuyatolea uamuzi.

Athari za ufinyu wa bajeti kwa mhimili huo zimekuwa zikiwapata na kuwaumiza wananchi wenye mashauri katika mahakama mbalimbali kuanzia za mwanzo hadi Mahakama ya Rufani.

Wanaoathirika na hali hiyo ni pamoja na mahabusu, hususani wanaokabiliwa na kesi kubwa zikiwano za mauaji kutokana na kukaa miaka mingi magerezani bila kesi zao kusikilizwa.

Serikali imekuwa ikitoa ahadi kwamba itaongeza bajeti kwa ajili ya mahakama, lakini ahadi hiyo imekuwa ikishindikana kutekelezwa kutokana na uhaba wa fedha.

Ingawa serikali ya awamu ya nne ilijitahidi kuiwezesha mahakama kwa kuongeza idadi ya mahakimu na majaji, lakini hatua hiyo haikusaidia kupunguza tatizo la ucheleweshaji wa mashauri katika mahakama zetu.

Moja ya athari zinazotokana ucheleweshaji wa kesi ni vishawishi vya rushwa, kwa kuwa hali hiyo inasababisha baadhi ya wenye kesi kuona njia rahisi ya kesi zao kumalizika ni kutoa rushwa.

Katika kudhihirisha kuwa kero hiyo inapatiwa ufumbuzi, serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais John Magufuli, imetoa Sh. bilioni 12.3 kwa ajili ya kusaidia kukamilisha kesi pamoja maendeleo ya mahakama.

Fedha hizo zilikadhidhiwa juzi na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango, kwa Mtendaji Mkuu wa Mahakama, Hussein Katanga, ukiwa ni utekelezaji wa ahadi ya Rais Magufuli aliyoitoa Alhamisi iliyopita kwa Jaji Mkuu, Mohamed Othman Chande, kwamba angewapatia kiasi hicho ndani ya siku tano ili zisaidie kumaliza kesi zikiwamo 442 za wakwepa kodi.
Rais Magufuli alitoa ahadi hiyo alipokuwa akihutubia wadau wa sheria wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Sheria na kusema kwamba mahakama ilikuwa inapewa bajeti ya Sh. bilioni 41, lakini mwaka 2015/2016 ilishuka hadi Sh. bilioni 12 ambazo hadi sasa haijapewa, huku akiahidi kuwa mhimili huo utaendelea kutengewa bajeti kubwa zaidi.

Serikali inastahili pongezi kwa kutekeleza ahadi ya kutoa fedha hizo kwa wakati mwafaka licha kukabiliwa na changamoto nyingine nyingi kwa sasa zinazohitaji fedha nyingi, ikiwamo utoaji wa elimu ya bure ya msingi na sekondari.

Baada ya kupewa fedha hizo, wananchi sasa wanatarajia kuona utendaji wa mahakama ukiboreka na wenye tija na ufanisi. Kubwa zaidi ni kuona kasi kubwa ya kukamilika kwa kesi mbalimbali zilizoko mahakamani na zingine zitakazopelekwa bila kuwapo kisingizio cha ufinyu wa bajeti.

Wananchi wanatarajia pia kuona zinajengwa mahakama mpya katika maeneo kadhaa ambayo hayakuwa na mahakama sambamba na kukarabati majengo ya mahakama ambayo yako katika hali mbaya pamoja na ununuzi wa vifaa.

Kauli ya Mtendaji wa Mahakama , Katanga kuwa fedha hizo zitasaidia mahakama katika miradi yake mbalimbali ikiwamo ya ujenzi wa mahakama, ndiyo inayotutia matumaini kwamba mahakama imewezeshwa kwa fedha na kilichobakia ni kuona inachapa kazi.

Habari Kubwa