Mahakama inastahili pongezi kwa hukumu hii

29May 2019
Mhariri
DAR
Nipashe
Mahakama inastahili pongezi kwa hukumu hii

MAMLAKA zote husika zina jukumu la kuhakikisha vitendo vya ukatili hasa ubakaji kwa watoto vinakomeshwa, ili kuwafanya waishi maisha ya furaha na amani.

Miongoni mwa mamlaka hizo ni pamoja na wizara mbalimbali, Jeshi la Polisi, Ustawi wa Jamii, Mahakama na taasisi nyinginezo zinazohusika katika kusimamia masuala ya haki na malezi ya watoto.

Tunatambua kuwa vitendo vya ukatili kwa watoto vinaathiri kwa namna nyingi ikiwamo kiakili, kimwili na kisaikolojia hali ambayo ni wazi isipodhibitiwa inaweza kuathiri ustawi wa jamii kwa ujumla.

Hivi karibuni Mpango Kazi wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto 2017 -2022, ulizinduliwa na Waziri wa Afya, Maendeleo Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu.

Alikaririwa na vyombo vya habari akibainisha kuwa ukatili dhidi ya watoto unafanywa katika nyumba wanazoishi na shuleni, hivyo kila shule ya msingi na sekondari kutaundwa timu za ulinzi pamoja na kila kata kuwa na timu ya ulinzi.

Kwa mujibu wa takwimu kutoka Jeshi la Polisi, vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto vilivyoripotiwa 2015 vilifikia 22,876 kati ya hivyo vitendo vya ubakaji vilikuwa 3,444, shambulio, kujeruhi na matusi vilikuwa 14,561.

Jambo linalotia moyo ni kwamba baadhi ya mamlaka zimejitokeza kuonyesha umakini wa hali ya juu katika kuhakikisha zinakomesha vitendo hivyo viovu.

Tumepata taarifa kuwa Mahakama ya Wilaya Mkoa wa Kigoma imemhukumu mkazi wa Burega, Manispaa ya Kigoma/Ujiji, Sadock Amani (21), kifungo cha maisha jela kwa kosa la kumbaka mtoto mwenye umri wa miaka mitano.

Hukumu hiyo ilitolewa Mei 27, mwaka huu na Hakimu Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Kenneth Mutembei, baada ya upande wa mashtaka kuthibitisha kosa hilo bila kuacha shaka.

Tunampongeza Hakimu Mutembei kwa kuwa amekaririwa na vyombo vya habari akieleza kuwa mahakama hiyo inatoa adhabu kali dhidi ya mshtakiwa ili liwe fundisho kwake na kwa vijana wengine wenye tabia ya kikatili kama yake.

Pia tunapongeza upande wa mashtaka kwa kuwa umefanikisha kutolewa kwa hukumu hiyo kali, kwa sababu uliwezesha ushahidi usio na shaka kutolewa na mashahidi watano pamoja na kielelezo kimoja cha PF3 ambavyo vilithibitisha kuwa mshtakiwa huyo alimbaka mtoto huyo.

Makahama hiyo ilielezwa kuwa mshtakiwa huyo na mama wa mtoto wamepanga nyumba moja maeneo ya Burega, Manispaa ya Kigoma/Ujiji.

Mahakama haikuwa na wasiwasi na ushahidi uliotolewa na daktari pamoja na mtoto huyo, ambapo alimbaini mshtakiwa kuwa ni jirani yake, ndiye aliyembaka kwa sababu walikuwa na mazoea ya kuitana anko.

Pia mtoto huyo aliyefanyiwa ukatili imeelezwa kuwa alikuwa na uelewa mkubwa wa kueleza, hivyo kufanya Mahakama hiyo kuamini kuwa mshtakiwa huyo alimbaka mtoto huyo.

Upande wa mashtaka umethibitisha kosa bila kuacha shaka yoyote, hivyo Mahakama inamtia mshtakiwa hatiani kwa kosa aliloshtakiwa.

Awali akisoma hati ya mashtaka, Wakili wa Serikali, Benedict Kivuma, alidai kuwa Januari 5, 2018 majira ya mchana eneo la Burega, mkoani Kigoma, mshtakiwa alimbaka mtoto huyo na kumsababishia maumivu makali.

Tunasisitiza kuwa hatua kali za kisheria zinaweza kusaidia kukomesha vitendo hivi vya kikatili, lakini pia wanajamii hasa wazazi wanapaswa kuongeza umakini katika kufuatilia nyendo za watoto pamoja na kuzungumza nao ili kuwaelimisha wasiogope kujieleza wanapotendewa ukatili.

Habari Kubwa