Mahakama isafishwe

05Jan 2017
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Mahakama isafishwe

KATIKA toleo letu la jana tulichapisha habari iliyoeleza kuhusu hatua mbalimbali zinazochukuliwa na serikali kurejesha maadili ya watumishi wa Mahakama.

Kwamba utumbuaji wa majipu katika serikali ya awamu ya tano umeikumba pia Mahakama ya Tanzania.

Kwamba katika Mahakama mahakimu zaidi ya 60 wamejikuta wakifikishwa kortini kukabiliana na makosa mbalimbali huku wengine wakitimuliwa kazini.

Waziri wa Sheria na Katiba, Dk. Harrison Mwakyembe, alilieleza gazeti hili kuwa hatua hizo zilichukuliwa takribani miezi 14 iliyopita baada ya kuingia madarakani kwa serikali ya awamu ya tano na kwamba kuanzia Januari hadi Desemba, 2016, mahakimu 62 walifikishwa mahakamani kukabiliana na mashtaka mbalimbali yakiwamo ya rushwa na jinai.

Aidha, mahakimu 11 wamefutwa kazi, wakiwa ni sehemu ya watumishi 34 wa mahakama za mwanzo hadi juu waliokumbana na adhabu hiyo baada ya kukutwa na hatia kutokana na tuhuma mbalimbali za ukiukaji wa maadili ya kazi zao na utovu wa nidhamu.

Alisema mahakimu na watumishi wengine wa mahakama walifutwa kazi baada ya hatua zote kufuatwa, ikiwa ni pamoja na Tume ya Utumishi wa Mahakama kujiridhisha pasi na shaka kuwa walihusika katika vitendo viovu vinavyokwenda kinyume cha sheria za utumishi.


Kuhusu mahakimu 62 waliofikishwa kortini, Dk. alisema 30 kati yao walituhumiwa kujihusisha na makosa ya rushwa huku wengine 32 wakituhumiwa kwa makosa mengine mbalimbali yakiwamo ya jinai. Hata hivyo, alisema mahakimu hao wote 62 walishinda kesi, sababu ikiwa ni changamoto ya kuwafikisha wahusika mbele ya wenzao ili kuhukumiwa, hivyo baadhi yao kushinda kirahisi.

Makosa yaliyowaponza mahakimu waliofutwa kazi pamoja na watumishi wengine wa mahakama, alisema kuna aliyebainika kumsaidia mtu kufungua kesi moja kwenye mahakama mbili tofauti na mwingine alifungua shauri la mirathi bila kuwapo hati ya kifo.
Aliongeza kuwa mahakimu 30 walioshtakiwa mahakamani kwa tuhuma za rushwa na kushinda kesi zao, sasa hatima ya ajira zao ipo mikononi mwa Kamati ya Maadili na Nidhamu ya Mahakama.

Tunaipongeza serikali kwa kuchukua hatua hizo kwa kuwa mahakama ni chombo nyeti cha utoaji wa haki kwa wananchi, hivyo inapotokea watumishi wake kukosa maadili kunachangia kuwanyima watu haki.

Mhimili huo unahitaji watumishi ambao ni wasafi wanaotekeleza majukumu yao kwa uaminifu, uadilifu na weledi.


Tunakubaliana na Waziri Mwakyembe kwamba Kamati ya Maadili na Nidhamu ya Mahakama inaweza kuwarejesha kazini baadhi ya waliopelekwa huko, lakini kwa maoni yake haitakuwa sahihi kufanya hivyo kwa kuwa walishinda kesi mbele ya mahakimu wenzao, ikitiliwa maanani kuwa mtu hawezi kuwa jaji katika suala ambalo ana maslahi nalo.

Sababu ya pili ya kutowarejesha ni kuwa Mahakimu na majaji wameaminiwa na Katiba kubeba uamuzi wa mwisho kuhusu haki, uhuru na hata maisha ya watu. Hivyo hakimu au jaji hategemewi siyo tu kupokea rushwa, bali vilevile hata kufikiriwa tu, kuhisiwa na kutuhumiwa kuwa mla rushwa.

Tunaunga mkono hatua zilizochukuliwa za kuisafisha Mahakama na tunashauri kuchukuliwa kwa hatua zaidi ili mhimili huo urejee katika misingi yake ya kutoa haki kwa wote.

Tunasema hivyo kwa kuwa baadhi ya tuhuma zilizowagusa baadhi ya mahakimu, ikiwamo kusaidia mtu kufungua kesi ya mirathi bila hati ya kifo, ni dhahiri kuwa ni rushwa ya wazi ambayo mwishowe inawanyima haki baadhi ya wahusika.


Habari Kubwa