Maji ya Ziwa Victoria iwe fursa kwa wakazi wa Mkoa wa Tabora

18Mar 2020
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Maji ya Ziwa Victoria iwe fursa kwa wakazi wa Mkoa wa Tabora

MIKOA kadhaa nchini hususani ya kanda za magharibi, ziwa na kati imekuwa ikikabiliwa na changamoto ya upatikanaji wa majisafi na salama.

Kutokana na hali hiyo, wakati wa uongozi wa serikali ya awamu ya tatu chini ya Rais Benjamin Mkapa ulianzisha na kutekeleza mradi mkubwa wa maji kutoka Ziwa Victoria kwa ajili ya kuchukua maji kutoka ziwa hilo na kupelekwa kwenye mikoa ambayo ilikuwa inakabiliwa na tatizo la maji.

Mbali na changamoto zilizokuwapo wakati wa kuanza utekelezaji, lakini Mkoa wa Shinyanga kwa mikoa ya Kanda ya Ziwa ambao ulikuwa unakabiliwa na changamoto hiyo, uliweza kufikiwa na maji ya mradi huo na wakazi wake wakaanza kunufaika kwa kuondokana na kero hiyo.

Wilaya ya Kahama iliyoko mkoani humo baadaye nayo ilifikiwa na mradi huo na kuwa mkombozi kwa wakazi wake ambao awali walikuwa wakipata ufumbufu mkubwa wa maji.

Sasa habari za kufurahisha ni kwamba sasa mradi huo umeingia katika Mkoa wa Tabora katika wilaya za Igunga na Nzega, na serikali inasema tayari wakazi wake wameshaanza kunufaika na huduma hiyo.

Mradi huo unagharimu Sh. bilioni 600 na utanufanisha wakazi milioni 1.8 katika vijiji zaidi ya 90 katika maeneo yote ya mradi kuanzia kanda ya ziwa hadi Tabora Mjini, Igunga na Nzega.

Msemaji Mkuu wa Serikali, Dk. Hassan Abbas, alisema mwishoni mwa wiki kuwa mradi huo unapita zaidi ya kilometa 300.
Dk. Abbas ambaye ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, alisema kazi inayofanyika kwa sasa ni kupeleka maji hayo kwenye vijiji hivyo.

Hii bila shaka ni fursa muhimu kwa wakazi wa maeneo husika kwa kufanya shughuli mbalimbali za kijamii na kiuchumi kwa lengo la kujiongezea kipato. Sasa wakazi wake wanaweza kufuga, kulima na shughuli nyingine ambazo zinategemea maji.

Kutokuwapo kwa uhakika wa maji kulikuwa kikwazo kwa shughuli mbalimbali za kiuchumi na kijamii, hivyo tunaamini kuwa wakazi wa maeneo husika wataichangamkia fursa hiyo kwa ajili ya maendeleo yao.

Tunasema hivyo kwa kuwa maendeleo yameshuhudiwa katika maeneo kadhaa ya Mkoa wa Shinyanga ambayo kabla ya kufikiwa na mradi huo yalikuwa yakikabiliwa na vikwazo vingi.

Kufikiwa na fursa hiyo hakunabudi kuwaamsha wananchi kuchangamka kwa kuanza kuomba kuunganishiwa huduma ya maji kwa kuwa wameshafikiwa kwenye maeneo yao.

Mradi huo kwa kufika mkoani Tabora ni ishara kuwa mikoa mingine hususan ya Kanda ya Kati ya Singida na Dodoma, wenye changamoto hiyo inaweza kufikiwa na kunufaika.

Utekelezaji wa mradi huo inatia matumaini kuwa nchi yetu inaweza kunufaika kwa rasilimali zilizopo yakiwamo maji, ikiwa kutakuwa na ubunifu katika kuzitumia kwa maendeleo ya taifa na wananchi wake.

Ziwa Victoria liwe mfano kwamba rasilimali nyingine za maji zilizoko zitumike vizuri kuiendeleza nchi yetu. Kwa mfano Tanzania ina maziwa mengine na mito mikubwa, ambayo inapaswa kutumika kupeleka maji katika maeneo ambayo yanakabiliwa na uhaba wa maji.

Kwa kuzitumia rasilimali hizi kupitia utekelezaji wa miradi mikubwa, bila shaka Watanzania wengi watafikiwa na huduma za maji ya uhakika, huku lengo la serikali likiwa ni kuwa hadi kufikia mwishoni mwa mwaka huu, tutakuwa tumefikia azma ya kufikia lengo la asilimia 85 vijijini na mijini asilimia 95.

Habari Kubwa