Malalamiko ya uchaguzi S/mitaa yapatiwe suluhu

11Nov 2019
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Malalamiko ya uchaguzi S/mitaa yapatiwe suluhu

KUNA malalamiko mengi kutoka kwa vyama vya upinzani kuhusiana na mchakato wa uchukuaji na urejeshaji wa fomu za uchaguzi wa serikali za mitaa, ambao unatarajiwa kufanyika nchini kote Novemba 24, mwaka huu.

Malalamiko hayo yanahusu wagombea katika maeneo kadhaa kunyimwa fomu za kugombea na mengine yanahusu kukataliwa na watendaji wa ngazi husika kuzipokea fomu hizo hadi juzi ambayo ilikuwa siku ya mwisho, huku jana ikiwa siku ya mchakato wa uteuzi.

Kimsingi, kulikuwapo na malalamiko ya wagombea kadhaa kuchaniwa fomu, baadhi kutekwa, kupigwa na mengine ambayo yanahusu vitendo vya kihalifu, ambavyo havipaswi kupewa nafasi katika nchi yetu ambayo wananchi wake wameishi katika misingi ya umoja wa kutaifa na amani kwa miaka yote tangu Uhuru kutoka kwa wakoloni.

Katika maeneo kadha, watendaji ambao ndio maofisa wasimamizi wa uchaguzi huo wametoa majibu kuhusiana na malalamiko hayo, lakini majibu mengi hayatoshelezi na yanaacha shaka.

Matumaini yetu ni kuwa kwa kila mmoja wetu kama taifa, Tanzanua ni muhimu na ya kwanza na uchaguzi ni baadaye uwe wa serikali za mitaa au uchaguzi mkuu. Tunalisema hili na kuweka msisitizo huu kwa kuwa uchaguzi utapita na Tanzania itaendelea kuwapo milele.

Hatuoni sababu za kuwapo ugomvi, vitisho, malumbano na kila aina ya matukio yanayoashiria kuwa jamii yetu haithamini umuhimu wa amani na umoja wa kitaifa, badala yake kuthamini itikadi za vyama vya kisiasa, ambazo hazina tija katika afya ya taifa letu.

Kila mmoja anapaswa kuelewa kuwa uchaguzi sio vita bali ni kushindana kwa kujenga hoja pamoja na washindani kujenga utamaduni wa ustaarabu na kuvumiliana kwa kuwa wote tunajenga taifa moja.

Hayo ndiyo waliyoyasisitiza na kuyahimiza waasisi wa taifa letu kwa miaka yote waliyoishi duniani, ikiwamo baada ya kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vingi vya siasa mapema miaka ya tisini.

Kwa kuwa kuna malalamiko mengi, ni vizuri kushughulikiwa na serikali kwa kuwa ndiye msimamizi wa uchaguzi huo kupitia Waziri mwenye dhamana ya Tamisemi, Selemani Jafo.

Kuna njia nyingi za kuchukua kwa ajili ya kuyapatia ufumbuzi. Kubwa ni kukutana na viongozi wa vyama vyote vya siasa ambavyo vimesimamisha wagombea, ambavyo vinadai kuwa wagombea wao wamefanyiwa rafu ili kama kuna ukweli haki itendeke, hivyo muafaka kupatikana.

Pili maeneo ambayo yatabainika kuwa wagombea wa vyama hivyo hawakutendewa haki muda uongezwe ili warejeshe fomu zao ili wasimamishe wagombea katika vijiji, mitaa na vitongoji.

Mambo hayo yakifanyika, yataondoa dhana iliyojengeka kuwa wagombea wa upinzani wanafanyiwa rafu kwa lengo la kukibeba chama tawala, hivyo kutoa picha kuwa mambo hayo yatajirudia tena mwakani katika uchaguzi mkuu na kusababisha usiwe huru na haki.

Ikiwa vyama havitarudishwa na hatua zitakazochukuliwa na Waziri Jafo, baada ya kumpelekea malalamiko, hatua nyingine vinavyoweza kuchukua katika kudai haki ni kwenda mahakamani.

Tunaendelea kuhimiza uwajibikaji wa wadau wote wa uchaguzi huu ili uwe huru na haki, hivyo kuweka mazingira mazuri ya uchaguzi mkuu wa mwakani.

Tukijenga utamaduni wa kufanya uchaguzi wa ushindani katika mazingira ya haki na usawa, ni dhahiri kuwa amani, utulivu na umoja vitadumu katika taifa letu na hakika tutakuwa tunawaenzi kwa vitendo waasisi wetu.

Habari Kubwa