Mambo ya ukabila, udini yakemewe kwa nguvu zote

13Oct 2021
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Mambo ya ukabila, udini yakemewe kwa nguvu zote

JUZI Rais Samia Suluhu Hassan, aliwaonya wanaosambaza maneno kuwa anawajibisha na kuteua kwa kuangalia kabila la mtu, na kuweka bayana kuwa hafanyi kwa kigezo hicho bali kwa kadiri ya sifa muhimu na uwajibikaji wa mtu.

Aidha, kwa wanaoboronga wanachukuliwa hatua kwa kadri ya makosa yao na siyo kwa kuwa anatoka kabila gani, kwa kuwa Tanzania ni nchi yenye makabila zaidi ya 120, lakini utendaji kazi, ajira na vyeo havitolewi kwa kuangalia kabila wala ukanda anaotoka mtu.

Onyo la Rais Samia limekuja wakati muafaka ambao tuna elekea OKtoba 14 ya kumbukumbu ya miaka 22 tangu kifo cha baba wa taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere, ambaye aliunganisha Tanzania na kuhakikisha watu hawatambuliki kwa makabila, ukanda au sehemu wanazotoka.

Tanzania ni moja ya nchi za Afrika iliyofanikiwa kukomesha ukabila kwa kuwa watu wameoana na kuoleana kwa mchanganyiko wa makabila, tofauti na nchi nyingine ambazo ili upate kazi fulani sifa ya kwanza ni kabila unalotokea.
 
Hali hiyo imezifanya nchi hizo kushindwa kuwaunganisha watu wake kiasi kwamba katika kila jambo sifa ya kwanza ni muhusika anatokea kabila gani, kiasi cha siasa kutawaliwa na ukabila huku makabila madogo yakikosa uwakilishi.

Kwa Tanzania hali ni tofauti kwa kuwa mtu wa kabila lolote anaweza kuoana na yeyote na kuishi kokote, kuongoza kokote bila kuulizwa anatokea kabila gani, na ndilo lililotufanya wamoja siku zote.

Ndiyo maana leo hii mtu yeyote anaweza kugombea ubunge au udiwani katika eneo lolote, alimradi awe na nguvu ya ushawishi kwa jamii husika, lakini hata mtu yeyote anaweza kuwa Mkuu wa Mkoa, Wilaya au Mkurugenzi katika eneo lolote bila kuulizwa kabila lake.

Ni kawaida Watanzania kuishi, kusoma na kuwa marafiki bila kuulizana kabila wala ukanda wanaotokea, na hiyo imekuwa sifa ya muda mrefu ya kuigwa na wengine duniani kote.

Rais Samia amesisitiza hatumbui kwa sababu ya kabila la mtu bali mtu kafanya makosa ambayo kwa mujibu wa sheria, taratibu na kanuni za kazi zinastahili kuchukuliwa hatua, na hilo linapaswa kuendelea kubaki kuwa msingi.
 
Wanaozusha kuwa uteuzi au utumbuaji unafuata misingi ya kabila wameishiwa hoja na wanatakiwa kunyamazishwa mapema, ili kuepusha kuingiza nchi kwenye matatizo ya kubaguana kwa kadri ya makabila au dini.

Lakini ni muhimu kwa wenye mamlaka ya kuteua kuhakikisha suala la ukabila halipewi kipaumbele kiasi cha kuonekana kwa Watanzania kuwa wengi wa eneo fulani wamepewa nafasi zaidi ya wengine.

Pia ni muhimu kuhakikisha hakuna ukanda, ueneo au dini katika kutoa nafasi yoyote ila bali msingi uwe ni taaluma, uadilifu na uzoefu katika kazi.

Zipo nchi zimeingia kwenye machafuko ya wao kwa wao kutokana na ukabila na udini, hii ni saratani isiyo na tiba iwapo itaingia kwenye nchi yoyote, na ni lazima hatua madhubuti zichukuliwe kuhakikisha hakuna ubaguzi wa muundo huo.

Mathalani, kwenye vitabu vya dini imeandikwa, mwanadamu ameumbwa  kwa mfano wa Mungu, maana yake Mungu haangalia rangi, kabila na eneo unalotoka bali anakutambua kama mwanadamu.
 
Wasanii mbalimbali wameimba nyimbo kuwa sote ni ndugu watoto wa baba mmoja, na ndiyo maana ukiwaweka pamoja watoto wadogo wa makabila, rangi na dini tofauti watacheza na kushirikiana bila kubaguana, maana yake ni kuwa tunapokuwa wakubwa ndiyo tunabaguana, lakini Mungu hakuwahi kutubagua.
 
Ni muhimu jamii nzima kukemea kwa nguvu zote wanaoendekeza ukabila na udini, bali kusimama kwenye msingi ya umoja wa kitaifa, kufanya kazi kwa bidii, uadilifu na kufuata misingi iliyopo.