Maofisa mikopo wa benki wadhibitiwe

17Jan 2020
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Maofisa mikopo wa benki wadhibitiwe

JUZI Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, aliwaonya baadhi ya maofisa mikopo wa benki mbalimbali nchini, ambao wamekuwa wakishirikiana na madalali kuuza mali za wananchi waliochukua mikopo.

Alikwenda mbali zaidi na kutoa mfano wa ofisa mikopo mmoja ambaye alijimilikisha nyumba tano za wananchi walikuwa na mikopo wakashindwa kuilipa.

Nyumba hizo alizipata kilaghai kwa kuwa wakopaji husika hawakupewa nafasi ya kujitetea au kuwa na mazungumzo na benki husika bali moja kwa moja ulifanyika mpango wa kuuza mali zao na mnunuzi akawa ofisa mikopo.

Waziri huyo alieleza kuwa maofisa mikopo wanapotoa mikopo kwa wateja husubiri mwaka mmoja kisha wanawafuata madalali, ambao hupewa kazi ya kwenda kupiga mnada mali iliyowekwa dhamana kwa madai ya mhusika kukiuka masharti ya mikopo.

Waziri anarudia kauli hiyo ambayo amekuwa akiisema mara kwa mara kwa kuwa lilikuwa tatizo kubwa ambalo linaendelea kwisha taratibu.

Mara ya kwanza aliwaonya madalali wanaokula njama na benki ili kuuza mali za wakopaji wanyonge kinyume cha sheria.

Kwa mujibu wa Waziri huyo, mwaka 2016 alipokea malalamiki zaidi ya 80 ya kesi za watu walioonewa na madalali hao na kati ya kesi hizo zaidi ya asilimia 75 ni wanawake.

Alisema madalali hao wanachokifanya, wanakwenda siku ya Jumamosi Sinza wananadi nyumba kwa Sh. milioni 4 , na kwamba haiwezekani nyumba kuuzwa chini ya asilimia 25 ya thamani, huku akiwataka kufanyakazi hiyo kwa sura ya ubinadamu na si kuangalia fedha.

Tunafahamu katika kutafuta suluhisho la utakaokuwa na ulaghai huu, Waziri Lukuvi aliweka masharti kwamba bei wanayotaka kuuzia nyumba husika mthamini wa ardhi ni lazima ajue, hatua zilizofikiwa hadi kuuza nyumba ziandikwe na ziwe wazi ili kujua thamani halisi ya nyumba husika kulingana na bei ya soko.

Kinachotakiwa kufanyika ni mtathmini wa ardhi atafuatili kujua bei iliyouzwa kama ndiyo bei ya soko na kama haki imetendeka kabla ya kuhamisha umiliki wa nyumba.

Sambamba na hilo, Benki Kuu ya Tanzania (BoT), ilisema na kanuni za sheria ya fedha ambazo zitazibana taasisi za kifedha kuwa na utaratibu wa kuwasikiliza na kujadiliana na wateja ambao wameshindwa kulipa mikopo kutokana na kuporomoka kiuchumi.

Alichokisema Waziri Lukuvi ndiyo uhalisia kutokana na vilio ni vingi na wengine wamepata maradhi ya shinikizo la damu kutokana na kupoteza mali zao katika mazingira ambayo wangeweza kuokoa mali zao na kulipa deni la benki.

Tunaona lipo tatizo la msingi ambalo benki zinapaswa kulishughulikia kabla ya kufanya mnada wa mali ya mteja wao, kama alivyoelekeza Waziri lazima kujiridhisha na mambo mengi ikiwamo mthamini wa ardhi kushirikishwa ili nyumba husika iuzwe kwa bei halisi na siyo kwa lengo jingine.

Tunaamini iwapo kutakuwa na mazunguzo na wateja kabla ya kufikia uamuzi wa kuuza mali husika, basi kutakuwa na maelewano na hatua za kisheria zitafuatwa na kila upande kuridhika kabla ya kuingia kwenye mvutano au uonevu wowote.

Lakini, benki zinapaswa kujisafisha juu ya lawama hizi kwa kuchukua hatua kwa wote ambao wameonekana kunufaika na mali za wakopaji ambazo zimepatikana kwa njia za dhuluma na ujanja unaoacha maumivu kwa wateja.

Tunazishauri benki kuweka utaratibu wa kuwafuatilia maofisa wake kimaadili kwa kuwa kuna mambo mengi yasiyofaa ambayo baadhi yao wamekuwa wakiyafanya likiwamo kuwaomba au kuwalazimisha wawape fedha wateja waliopata mikopo kwenye benki zao kwa madai kuwa wamewasaidia kuwezesha mchakato wa kukopeshwa.

Habari Kubwa