Maono ya Nyerere yafuatwe kwa vitendo

14Oct 2021
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Maono ya Nyerere yafuatwe kwa vitendo

BABA wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere, wakati wa uhai wake hususan akiwa Rais wa Taanganyika na baadaye Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, alianzisha na kutekeleza mipango mingi, ambayo iliiwezesha nchi yetu kusimama kama taifa.

Baada ya nchi kupata Uhuru wa bendera mwaka 1961, alibaini kuwa bado kulikuwapo na kazi zaidi ya kufanya kutokana na mfumo wa uchumi tuliourithi kutoka kwa wakoloni kutoonyesha dalili kama ungewapa matunda wananchi.

Hiyo ni kutokana na njia zote kuu za uchumi kama ardhi, viwanda, migodi, shule, hospitali na za usafirishaji kuendelea kuwa chini ya umiliki wa watu wachache. Kadhalika, ajira zilikuwa ni shida kwa wazalendo.

Aliamua kutaifisha mali hizo zote na kuziweka chini ya umiliki wa serikali, lengo likiwa ni kuwawezesha Watanzania wote kunufaika na kupata maendeleo. Mbali na utaifishaji, Mwalimu Nyerere pia aliunda mashirika ya umma takribani 500 ambayo pamoja na kufanya shughuli za uzalishaji na kuingiza fedha za ndani na za kigeni, yalisaidia sana kuwapa ajira wananchi wengi wakiwamo hata ambao hawakuwa na elimu kubwa.

Hatua nyingine alizochukua ni kutoa bure huduma za kijamii kwa wananchi kama elimu, matibabu, maji na nyinginezo. Katika kuhakikisha kwamba huduma hizo zinawafikia wananchi wengi, alianzisha ‘operesheni vijiji’ mapema miaka ya sabini, ambapo wananchi walikusanywa na kupelekwa kwenye vijiji maalum vilivyowekewa huduma hizo.

Mwalimu Nyerere aliona njia ambayo ingeifikisha Tanzania katika maendeleo ni kufuata itikadi ya Ujamaa na Kujitegemea akiamini kuwa ni itikadi ambayo haina matabaka na inayoweza kuwafanya watu wote kunufaika na keki ya taifa, lakini kumfanya kila mmoja aishi kwa kufanya kazi kupitia kilimo.

Kwa kuamini kuwa asilimia kubwa ya wananchi waliishi kwa kutegemea kilimo, serikali iliweka msukumo mkubwa kwa sekta hiyo ikiwamo kugawa pembejeo bure, kupeleka maofisa ugani vijijini na kuyatafutia masoko mazao yote ya biashara.

Maazimio kadhaa yalitangazwa ikiwa ni njia ya kutekeleza kwa vitendo sera ya Ujamaa na Kujitegemea yakiwamo la Arusha la mwaka 1967 ambalo lililitumika kuweka njia zote za uchumi kwa umma; la Musoma Elimu kwa Wote 1974 na la Iringa Siasa ni Kilimo mwaka 1972.

Leo tunapofanya kumbukizi ya miaka 22 ya kifo cha Mwalimu Nyerere tunaona mchango wake mkubwa na alivyojitoa katika historia na maendeleo ya nchi yetu.

Kuna mengi ya kumkumbuka Nyerere, lakini safu hii haiwezi kuyabeba yote ila baadhi ya mengine ni utaratibu wake na viongozi wenzake kwenda vijijini kila mara kuhimiza kilimo pamoja na kuwaunganisha Watanzania kuwa wamoja bila kuegemea kwenye ukabila, ukanda na udini.

Maisha ya Mwalimu Nyerere yanapaswa kuwa kioo kwetu, hivyo hatunabudi kuendeleza yote mazuri aliyotuachia.

Tunaelewa kuwa mfumo wa uchumi umebadilika kutokana na kutawaliwa na utandawazi, lakini hilo halitafuta kabisa maono aliyokuwa nayo Nyerere. Kama wakati wake alijielekeza kwenye kilimo, kwa nini sasa viongozi wetu wakaweka nguvu kubwa katika ujenzi wa viwanda kukabiliana na tatizo la sasa la ajira kwa vijana wanaohitimu vyuo vikuu?

Tunaona pia kuwapo kwa umakini mkubwa katika kubinafsisha baadhi ya mashirika ya umma kuepuka makosa yaliyofanyika miaka iliyopita, hivyo kuisababishia nchi hasara.

Wakati nchi yetu inapata Uhuru, Mwalimu Nyerere aliwataja maadui watatu kwa taifa letu ni umaskini, ujinga na maradhi. Hata hivyo wanazuoni kwa sasa wameongeza adui mwingine kuwa ni ufisadi.

Tunawashauri viongozi wetu kwamba mawazo mengi ya Nyerere hayajafa, hivyo katika kuwaletea maendeleo wananchi, hawanabudi kuendelea kuyafuata. Msisitizo uwe wa kupambana na maadui hao ukwamo wizi na matumizi mabaya ya fedha za umma.

Licha ya serikali kuacha kutoa huduma bure za kijamii kutokana na masharti ya wakubwa wa dunia mwanzoni mwa miaka ya tisini, ni jambo la kujivunia kuona serikali imefuta gharama za elimu ya msingi hadi kidato cha nne.