Maonyesho ya Kimataifa ya Biashara yawe fursa

29Jun 2022
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Maonyesho ya Kimataifa ya Biashara yawe fursa

WAKATI maonyesho ya Kimataifa ya Biashara (DITF) yakianza rasmi jijini Dar es Salaam, washiriki zaidi ya 3,000 kutoka nchini wanatarajiwa kuonyesha bidhaa zao.

Washiriki wengine kutoka nchi za nje 22 wanatarajiwa kuwa miongoni mwa kampuni 180 za nje zitakazoonyesha bidhaa na kuleta hamasa kwa watu watakaokwenda kutembelea mabanda yaliyoandaliwa kwa ajili hiyo.

Maonyesho hayo ambayo kwa jina maarufu hujulikana Sabasaba, huvuta mamia ya wakazi wa Jiji la Dar es Salaam kwenda kutembelea na kujionea bidhaa mbalimbali zinazoonyeshwa.

Fursa hiyo ya kufanyika maonyesho hayo kila mwaka haina budi kutumiwa na wajasiriamali kutangaza bidhaa wanazozitengeneza na vile vile kupata ujuzi kutoka kwa wenzao wa nje wanaokuja kushiriki.

Hata wananchi wanaokwenda kutembelea maonyesho hayo ni fursa kwao kwenda kujifunza kutoka kwa wenzao na kujitengenezea ajira.

Maonyesho hayo hayakuandaliwa kwa ajili ya watu kwenda kutembea na kununua bidhaa pekee, bali ni sehemu pia ya kubadilishana ujuzi kutoka kwa watu wanaotengeneza bidhaa zao mbalimbali ndani na nje ya nchi.

Kwa wajasiriamali na wafanyabiashara wa ndani kipindi hiki ni muhimu kwenu wa kutengeneza mtandao na wenzenu wa nje katika kukuza biashara zenu na kutafuta soko la nje.

Hakikisheni mnakuwa na vipeperushi vya kutangaza bidhaa zenu na pia kadi za mawasiliano hata mtakapotafutwa iwe rahisi kupatikana.

Kipindi hiki cha maonyesho ni lazima bidhaa mtakazozionyesha ziwe katika viwango vinavyokubalika kimataifa, kuanzia ubora wake na ufungaji utakaomvutia mteja.

Tanzania imebarikiwa kuwa na rasilimali nyingi na malighafi zinazoweza kutengenezwa bidhaa na kuleta utofauti na zile zinazotoka nje ya nchi.

Kwa mfano tumebarikiwa kuwa na aina tofauti za viungo vya asili vya chakula ambavyo pia hutumika kama dawa ya kutibu maradhi tofauti.

Nchi yetu ina mashamba yanayozalisha viungo hivyo, hasa kwa upande wa visiwani na kama vikitangazwa vizuri soko lake ni kubwa na watu kutoka mataifa mbalimbali hupenda kutumia viungo vyetu.

Wajasiriamali hasa wanawake wamekuwa na mwamko mkubwa wa kubuni vitu mbalimbali kuanzia bidhaa za chakula mpaka mavazi ambavyo wengine hushindwa hata kuamini kama vimebuniwa na kutengenezwa na Watanzania.

Fursa hii muhimu ya maonyesho haya itumike vizuri kuwatoa Watanzania kutoka hatua waliyopo kwenda mbele zaidi hadi kufikia ya kimataifa.

Tumeelezwa kuwa maonyesho ya Sabasaba yanatambuliwa na Umoja wa Taasisi zinazoandaa ulimwenguni, jambo ambalo linavuta nchi nyingi zilizopata mwamko kushiriki maonyesho hayo.

Uzuri wa maonyesho hayo hushirikisha wafanyabiashara wakubwa na wadogo hali inayotoa fursa ya wadogo kujifunza kwa wenzao na hatimaye wafikie malengo yao ya kuwa wafanyabiashara wakubwa baadaye.

Maonyesho hayo pia ni fursa kwa vijana kupata ajira za muda mfupi zikiwamo za kutangaza bidhaa za kampuni mbalimbali na pia ni sehemu ya kupata njia ya kuwasiliana na wenye kampuni, viwanda, ofisi kupata ajira za muda mrefu.

Itafurahisha kuona maonyesho hayo yanapomalizika wananchi wanaona faida ya kutangaza biashara zao na kutengeneza masoko ya nje.

Habari Kubwa