Mapambano ya rushwa ya ngono yahusishe wote

23Jun 2020
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Mapambano ya rushwa ya ngono yahusishe wote

WAHADHIRI wa vyuo vikuu wamepinga vikali madai ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), kuwa wanashawishi rushwa ya ngono vyuoni kwa wanafunzi wa kike.

Madai hayo yalitolewa wakati kampeni maalum ya kupinga rushwa ya ngono vyuoni iliyofanyika katika Chuo cha Uhasibu (TIA) tawi la Mbeya, na kujumuisha wahadhiri wa vyuo mbalimbali.

Mmoja wa wahadhiri alitetea wenzake kwa kueleza jinsi wanafunzi wa kike wanavyochangia kasi ya rushwa ya ngono.

Alisema wanafunzi hao kuvaa mavazi ya kutega na kufanya matendo ya kuwashawishi wakati nao ni binadamu na wanaweza kuingia majaribuni.

TAKUKURU ilidai kuwa rushwa hiyo hutokea zaidi kwa ahadi ya kuwapa alama nzuri kwenye mitihani na kupanga maeneo ya kufanya mafunzo kwa vitendo na kama wahadhiri wangekuwa imara, rushwa hiyo isingekuwa inajitokeza mara kwa mara.

Tatizo la rushwa ya ngono limeonekana kuwaathiri zaidi watoto wa kike na wapo ambao hutumia nafasi zao kuwanyanyasa au kuwabania katika jambo fulani ili akubali matakwa ya wahadhiri wao.

Athari ya kuwa na rushwa ya ngono kwanza ni kunyanyasa wanafunzi kisaikolojia, kuwaumiza kimwili kwa kuwa wanashiriki tendo la ndoa kwa kupata kitu fulani (alama za ufaulu).

Nyingine ni kuambukizwa maradhi ikiwamo Ukimwi na wapo waliojikuta kwenye maisha hayo na sasa wamepoteza tumaini la maisha yao, ilhali walikwenda chuoni kwa ajili ya kusoma kwa ajili ya maisha yao ya baadaye.

Pia, athari nyingine ni kuzalisha wataalamu ambao hawajaiva kabisa kwa kuwa walifaulu si kwa kusoma na kuelewa bali kusubiri majibu ya mitihani au alama za bure, na kuonekana ni wenye vyeti vyenye ufaulu wa juu lakini kiuhalisia hawastahili.

Wapo wahadhiri wanaostahili lawama hizi kwa kuwa wamedhamiria kutenda hayo, lakini wapo ambao wamejikuta kwenye mitego ya wanafunzi wa kike na kwa matamanio ya kibinadamu wamejikuta kwenye mtego.

Baadhi ya wanafunzi wa kike hawasomi na badala yake wanajihusisha ma starehe, kutoingia darasani na hawafanyi mazoezi yanayotolewa ambayo hutengeneza alama za kumwezesha mwanafunzi kufanya mtihani wa muhula.

Mwanafunzi wa aina hii maana yake atafanya kila awezalo kuwa karibu na mwalimu wake na anapopata upenyo anaonyesha anachotaka kwa kumtega mwalimu, naye bila ya kujua anaingia kwenye mtego wa kuwa na uhusiano wa kimapenzi na kuwa na mzigo mzito wa kumbeba kimasomo katika hali isiyo ya kweli.

Baadhi ya vyuo hakuna zuio la mavazi ya kuvaa mathalani vyuo vya umma, mwanafunzi anaruhusiwa kuvaa anachoona ni sawa.

Wanafunzi wengine kwa kujua au kutojua huvaa mavazi yenye kuonyesha maumbile yao ambayo huwa ni mtego kwa wahadhiri, nao bila kujijua wanaingia kwenye mtego.

Hivyo, suala la rushwa ya ngono linapaswa kuangaliwa kwa jicho la pekee kwa kuwa wakati mwingine husababishwa na pande zote.

Kutokana na tamaduni zetu ni ngumu sana kwa mwanaume kuripoti tukio la mwanaume kumtaka kwa nguvu, na wakati mwingine huona ni ufahari kutembea naye kuliko achekwe kwa kukataa vishawishi.

Pia, lipo tatizo la wahadhiri wa kike kuwataka wanafunzi wa kiume na wakati mwingine wanafunzi hushawishiwa wahadhiri, nalo si jambo la kufumbiwa macho kwa kuwa madhara yake ni makubwa.

Tunaona ni vyema pande zote zikashiriki kukomesha rushwa ya ngono kwa kuhakikisha kila mmoja anatimiza wajibu wake, na inapokuwa kinyume chake hatua za kisheria zichukuliwe.

Taifa linahitaji wataalamu waliopikwa na kuiva wawapo masomoni na siyo waliopewa majibu au kutoa rushwa ya ngono na kupata alama.

Tunaipongeza TAKUKURU kuanza kutoa elimu ya rushwa ya ngono vyuoni ili kusikia yanayoelezwa na wanafunzi pamoja na wahadhiri.

Tunaamini kuwa elimu hiyo itawezesha pande zote kujua upungufu wa kila upande na athari zinazoweza kuwapata. Tunatarajia kuwa baada ya kupata elimu hiyo tatizo hilo litapungua kama si kumalizika kabisa.

Habari Kubwa