Maparachichi yahiaji soko

03Aug 2021
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Maparachichi yahiaji soko

SERIKALI mara kadhaa imekuwa ikihamasisha kilimo cha parachichi kwamba ni fursa kwa wakulima, na kwamba zao hilo linaweza kuwatoa kimaisha.

Zao hili linastawi kwa wingi katika mikoa yenye hali ya hewa ya baridi, ingawa wananchi wengi wa maeneo hayo hawajaiona fursa hiyo, pengine kutojua kuwa lina soko ndani na nje ya Tanzania. Takribani miaka miwili iliyopita, serikali ilianza kusisitiza kwa bidii uzalishaji wake pamoja na kuahidi kuwatafutia soko la ughaibuni wakulima, hususani mikoa ya Nyanda za Juu Kusini.

Sasa serikali inasema moja ya mikakati yake kwa wakulima wa maparachichi, ni kuendelea na mazungumzo na serikali ya Afrika Kusini ili kupata soko la matunda hayo yanayolimwa katika maeneo mbalimbali nchini.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, alisema juzi akiwa mkoani Mbeya kwamba, hatua hizo zinazoendelea kuchukuliwa na serikali zitasaidia kutatua kero ya wananchi kuingia hasara kwa kutupa matunda hayo baada ya kuoza, kutokana na kukosa soko.

Alisema hayo alipokuwa akizungumza na wananchi wa Wilaya ya Rungwe baada ya kutembelea mashamba ya kiwanda cha maparachichi cha Kampuni ya Kuza Afrika Ltd kilichopo katika Kijiji cha Ilolo, Kata ya Kiwira.

Pamoja na ufafanuzi huo, anawataka wananchi wa wilaya hiyo na maeneo mengine ambayo zao hilo linastawi, kuendelea kuzalisha kwa wingi kuwa soko hilo ni la uhakika na litapatikana.

Lakini alisema, Wizara ya Kilimo imepewa kazi ya kusimamia kilimo cha maparachichi na kuwatafutia wakulima mbegu bora, kutunza miche shambani na kutafuta masoko na kuwataka wakulima walime kwa nguvu.

Aidha, aliwaagiza maofisa kilimo kuanzia wa mkoa mpaka wilaya kuhakikisha wanawasaidia wakulima kulima kisasa zao hilo, huku wakurugenzi wakitakiwa kuwaondoa maofisa kilimo halmashauri wakafanye kazi kwa wakulima na kuanzisha mashamba darasa ya kufundishia wakulima.

Sisi tunaunga mkono juhudi hizo za serikali za kutaka kuwasaidia wakulima wa zao hilo kwa kuwatafutia soko nje ya nchi, kwani hatua hiyo itasaidia kuwafanya waondokane na hasara zinazotokana na ukosefu wa soko.

Hasara hizo ni pamoja na maparachichi kuoza, kwa sababu ya ukosefu wa soko, kutokana na ukweli kwamba, kuwapo kwa soko la uhakika kunasaidia  matunda yasioze na kuuza na kujipatia fedha kwa ajili ya maendeleo yao.

Lakini tunaona ingekuwa vyema zaidi iwapo serikali ingehamasisha pia ujenzi wa viwanda vingi zaidi vya kuchakata matunda nchini, ili wakulima wawe na sehemu badala ya kutegemea vichache vilivyopo.

Hatua hiyo inaweza kuongeza soko la ndani kuanzia kwenye maparachichi, machungwa, mananasi na matunda mengine, ambayo yamekuwa yakioza mashambani kutokana na ukosefu wa soko.

Pia kuwapo viwanda vingi vya kuchakata matunda, kutasaidia juhudi za serikali za kutaka Tanzania kuingia katika masoko ya kimataifa kwa kuuza bidhaa zinazotokana na matunda mbalimbali yanayopatikana nchini.

Tunatambua kuwa, lengo la serikali ni kufikia nchi ya viwanda, hivyo nchi ikiwa na viwanda vingi vya kuchakata maparachichi matunda, vitasaidia pia wakulima kuwa na kasi katika kilimo.

Uchache wa viwanda vidogo, kwa namna moja au nyingine, unachangia matunda mbalimbali kuoza mashambani au sokoni na kusababisha hasara kwa wakulima na wafanyabiashara.

Hivyo kwa mtazamo wetu ni kwamba, kuwapo kwa viwanda vingi vya kuchakata matunda nchini, linaweza kuwa suluhisho la hasara ya miaka nenda miaka rudi ambayo wakulima wa matunda wamekuwa wakikumbana nayo.

Tunaamini kwamba mamlaka husika zikiwamo Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji) na Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) zitalichukilia suala hili kwa uzito wake kwa kuwatafutia masoko wakulima wa maparachichi pamoja na kuwahamasisha wawekezaji kuanzisha viwanda vya kuyasindika.

Habari Kubwa