Mapatano yalindwe SUK idumu Zanzibar

11Aug 2021
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Mapatano yalindwe SUK idumu Zanzibar

BAADA ya kumalizika kwa Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar wa mwaka 2020 vyama vya siasa vya CCM na ACT-Wazalendo viliafikiana kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK).

Kuundwa kwa serikali hiyo kulifikiwa baada ya kuwapo kwa mgogoro wa kisiasa uliotokana na uchaguzi huo, hivyo pande husika zikaona umuhimu wa kufanya hiyo ili kudumisha amani, mshikamano, umoja na maridhiano miongoni mwa Wazanzibari.

Katika makubaliano hayo, aliyekuwa Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo ambaye alikuwa mgombea urais wake, Hayati Maalim Seif Sharif Hamad, alijumuishwa katika SUK na Rais Hussein Mwinyi, kwa kumteua kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais.

Itakumbukwa kwamba hiyo haikuwa mara ya kwanza kuwapo kwa SUK Zanzibar. Mara ya kwanza iliundwa mwaka 2010 baada ya Katiba ya Zanzibar kufanyiwa marekebisho, hufuatia mazungumzo kati ya aliyekuwa Rais wa Zanzibar, Amani Abeid Karume na aliyekuwa Katibu Mkuu wa CUf, Hayati Maalim Seif Shaarif Hamad.

Pamoja na nia njema na uzalendo ulioonyeshwa na Rais Mwinyi kurejesha SUK, hivi karibuni zimeonekana dalili ambazo zinatishia uhai wa serikali hiyo.

Baadhi ya matukio yaliyotokea kwenye uchaguzi mdogo wa ubunge Jimbo la Konde kisiwani Pemba wa Julai mwaka huu yametia doa uhai wa SUK, kutokana na viongozi wa ACT-Wazalendo kuyalalamikia kuwa yaliutia dosari uchaguzi huo.

Tusingetaka kuyarejea mambo yanayolalamikiwa, lakini viongozi wa ACT-Wazalendo wametoa masharti ya kushiriki tena kwenye uchaguzi huo, baada ya mshindi katika uchaguzi unaolalamikiwa kupitia CCM kutangaza kujiuzulu.

Juzi viongozi wa chama hicho cha upinzani wakiwa katika ziara kisiwani Pemba walisema hakitashiriki uchaguzi mdogo wa Jimbo la Konde hadi watumishi wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), waliohusika katika uchaguzi uliopita watakapowajibishwa.

Kiongozi Mkuu wa Chama hicho, Zitto Kabwe, akisoma maazimio, alisema chama hicho hakitashiriki uchaguzi huo hadi watumishi wa ZEC wawajibishwe. ACT inasema wananchi ambao waliumizwa na kuteswa kwenye uchaguzi walipwe fidia, ili wapate haki yao.

Pia inataka kuundwa kwa kamati ya kisheria ya kuratibu maridhiano ya kijamii, ili ZEC ionyeshe mwelekeo nini kifanyike ili maridhiano yazidi kukua. Pia kuitaka Serikali ya Zanzibar na ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuzifanyia marekebisho sheria zote za uchaguzi kabla ya mwaka 2025, ili uchaguzi mkuu ujao uwe sawa katika kushindania nafasi za uongozi.

Hata hivyo, kwa kuona athari zinazoweza kuhatarisha uhai wa SUK, baadhi ya hatua zimechukuliwa kuinusuru kama alivyoeleza Mjumbe wa Kamati Kuu ya ACT ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar, Othman Masoud Othman, kwamba kilichomfanya mbunge mteule wa Konde kutoka CCM kuachia ngazi ni mazungumzo.

Kutokana na matukio kadhaa ambayo yaliwahi kutokea Zanzibar na kutishia umoja wa Wazanzibari, tunaona kwamba kuna kila sababu kwa viongozi wenye mamlaka pamoja na vyama vya siasa vinavyoinda SUK kuchukua hatua ili kuinusuru.

Jambo la msingi ni kuweka utaratibu mzuri wa mawasiliano na majadiliano ya kila mara hususan pale inapoonekana kuna mambo au matukio unayoweza kuleta mgawanyiko.

Tusingependa kuona matukio ya nyuma, yakiwamo yaliyovunja SUK ya mwanzo yakijirudia, hivyo tunawasihi waliopewa dhama kutanguliza mbele maslahi ya vyama na Zanzibar badala ya maslahi ya kwao binafsi.

Habari Kubwa