Maradhi na uchafu huu vimeshindikana?

05Jun 2019
Mhariri
DAR
Nipashe
Maradhi na uchafu huu vimeshindikana?

MATATIZO ya uhaba wa mifumo na miundombinu ya kusafirisha majitaka, madampo ya kutupa taka pia tabia za wananchi kuendelea kuishi kwenye mazingira machafu kumesababisha Dar es Salaam kuwa na magonjwa ya fedheha kama kipindupindu.

Mbali na kipindupindu ambacho kinasababishwa na kula kinyesi kibichi, mji umejaa maradhi kama dengue na magonjwa ya kuharisha yanayochochewa na tabia za kula uchafu unaoweza kusambazwa na taka za vyooni.

Uchafu huo unasababishwa na kutapisha vyoo unaofanywa na wakazi wa jiji msimu wa mvua.

Taarifa za kulipuka kipindupindu Dar zilianza tangu mwezi uliopita, lakini hadi sasa mamalishe wanaendelea kupika na kuhudumia wateja kwenye maeneo yenye mitaro inayopitisha kinyesi kibichi.

Mbali na mamalishe kuchangia kueneza magonjwa Dar, mienendo iliyozoeleka wala isiyokemewa ya kufungua vyoo wakati wa mvua na kuvitapisha ni chanzo cha kusambaza kinyesi mji mzima hali inayosababisha kila mahali kujaa uchafu wa vyooni.

Ni dhahiri kuwa Dar es Salaam inasifika kwa uchafu ikilinganishwa na miji kama Moshi, Arusha na Iringa, tatizo ni kwamba hakuna miundombinu wala mipango ya uzoaji taka inayoeleweka na wakazi wake wana hulka za uchafu.

Mambo hayo na mengine mengi yanachangia Dar kuwa chafu na yenye magonjwa kama dengue, malaria, kuhara na kipindupindu kama hali ilivyo leo.

Wakati hayo yanatokea kuna maofisa afya na zipo sheria ndogondogo za jiji na za manispaa ambazo hazitumiki ipasavyo ili kulinda afya za walaji kwa kuhakikisha biashara za vyakula kuanzia migahawa, hadi vile vinavyopikwa ovyo mitaani vinadhibitiwa.

Aidha kuna sharia za usafiri wa mazingira ambazo kama zingetumiwa zingedhibiti kuzibua vyoo na kuacha kinyesi kusambaa mitaani kila wakati wa msimu wa mvua.

Huu si wakati wa kulaumiana lakini ni muda wa kukumbushana kuwa ni vyema kupanga upya na kuiweka Dar kwenye mazingira safi na salama yasiyo na magonjwa kama yanavyotokea sasa.

Maofisa afya na wanamgambo wa jiji watumie sheria ndogondogo na mamlaka waliyo nayo kudhibiti maradhi hasa dengue na kipindupindu.

Kwa vile kuna Sheria ya Mazingira ya mwaka 2004 ni wakati wa kuitumia kudhibiti kutapisha vyoo, mambo yanayofanywa wakati wa misimu ya mvua ambayo kiasi miaka inavyokwenda yanazidi kuzoelekea na kukubalika.

Pamoja na maofisa wa afya wa kata na wilaya , tunatarajia pia kuona maofisa wa Baraza la Taifa la Uhifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) na Mamlaka ya Chakula Dawa (TFDA), wakisimamia pamoja usafi wa jiji, wa vyakula na mazingira kwani tatizo la kipindupindu linahitaji wadau mtambuka kulishughulikia.

Tunaamini kuwa NEMC inalielewa kikamilifu suala la ujenzi unaoziba mitaro na kusababisha mafuriko kuharibu mazingira nyakati za mvua ni vyema ikalivalia njuga ili kuondoa magonjwa.

Tunatarajia kuona kamati za afya za jiji zikishirikiana na NEMC, TFDA na wadau wengine wa mazingira kuzungumzia na kusimamia uzibuaji wa mitaro ya maji taka na ikibidi kuondoa majengo yaliyojengwa juu ya miundombinu hiyo.

Dar es Salaam pamoja na kuwapo na mipango ya kuondoa maji taka, kuwapa wananchi maji salama na pia kuweka mikakati ya kusafisha maneno yamekuwa mengi kuliko utekelezaji.

Tunaamini kuwa wadau wakishirikiana Dar itakuwa salama tena isiyo na magonjwa kila mmoja akitimiza wajibu wake. Ikumbukwe taifa linahitaji kuwekeza kwenye maendeleo endelevu na si kutibu maradhi yanayoepukika kama kipindupindu.

Habari Kubwa