Maridhiano yatawale mkutano wa Bunge

06Sep 2016
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Maridhiano yatawale mkutano wa Bunge

MKUTANO wa nne wa Bunge la 11 unaanza leo mjini Dodoma.

Mkutano huo utakuwa na shughuli mbalimbali zikiwamo kujadili ripoti za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na taarifa za kamati za kudumu za Bunge za Hesabu za Serikali (PAC) na Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC).

Aidha, mkutano huo utachambua miswada sita ya sheria ambayo imekwishasomwa kwa mara ya kwanza bungeni.

Miswada hiyo ni wa Sheria ya Upatikanaji wa Habari Na. 4 wa mwaka 2016, Sheria ya Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali Na. 8 wa mwaka 2016 na wa Sheria ya Wanataaluma ya Kemia wa mwaka 2016.

Mingine ni wa Sheria ya Uthamini na Usajili wa Wathamini Na. 5 wa mwaka 2016, Muswada wa Sheria ya Utafiti wa Kilimo Na. 2 ya mwaka 2016 na Muswada wa Sheria ya Utafiti wa Uvuvi Na. 3 wa mwaka 2016.

Hata hivyo, mpasuko uliojitokeza tangu Mei, mwaka huu kutokana na wabunge wa upinzani kususia vikao vya Bunge umeonyesha picha kwamba baadhi ya wananchi wamekosa uwakilishi unaostahili katika chombo hicho cha kutunga, kurekebisha sheria na kuisimamia serikali.

Wabunge wa upinzani wamekuwa wakisusa kushiriki vikao vyote vya kibunge vinavyoongozwa na Naibu Spika, Dk. Tulia Ackson, wakidai kutoridhishwa na mwenendo wa uendeshwaji wa chombo hicho wakati vikao vikiwa chini yake.

Mwafaka haukupatikana kwa muda wote kutokana na kila upande kushikilia msimamo wake huku wabunge zaidi ya 90 wakiweka saini za kutokuwa na imani na Naibu Spika na yeye kusisitiza kuwa ataendelea kuongoza Bunge kwa kufuata kanuni.

Hali hiyo imesababisha athari kwa kuwa hata mkutano wa tatu wa Bunge la bajeti wabunge wa upinzani hawakushiriki, hivyo kukosa fursa ya kueleza changamoto zinazowakabili wapigakura pamoja na kutoa ushauri kwa serikali kuhusiana na utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Kutokana na umuhinu wa kuwapo na maridhiano na hali ya utulivu bungeni, kuna taarifa kuwa viongozi wa dini walikutana na kuwashauri viongozi wa upinzani kuwarejesha wabunge wao bungeni kwa maslahi mapana ya taifa letu.

Ushauri wa viongozi wa dini ni wa kupongeza na sisi tunaungana nao kwa kushauri kwamba pande zote zifikie maridhiano na mkutano unaoanza leo wabunge wa upinzani washiriki ili kuwapa wapigakura wao haki yao ya kuwakilishwa katika chombo hicho.

Matarajio yetu ni kwamba pande hizo zitaweka kando mambo yote yaliyotokea katika mkutano uliopita na kufuangua ukurasa mpya kwa kuweka mbele maslahi ya taifa.

Bila shaka kuanzia leo tutawasikia wabunge wote wakizungumza lugha moja bungeni kuhusiana na masuala ya msingi hususani ya maendeleo ya nchi yetu.

Kuna mambo mengi ambayo sisi kama taifa tunapaswa kushirikiana kuyatekeleza. Kwa mfano, suala zima la maendeleo ya elimu pamoja na ushiriki wa kila mmoja kuifanya Tanzania iingie katika uchumi wa kati kupitia viwanda.

Haya na mengine yanahitaji umoja na mshikamano.

Kama wabunge wetu watashindwa kuridhiana kwa sababu za itikadi za kisiasa, hali hiyo haiwezi kuruhusu wananchi wakashikamana na kuwa wamoja.

Matumaini yetu ni kwamba kuanzia leo tutawasikia wabunge wakijadili mambo yote yaliyoko katika ratiba wakiwa wamoja na maridhiano yakiutawala mkutano huo.

Habari Kubwa