Mashabiki Simba, Yanga wakiadhibiwa watakoma

03Oct 2016
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Mashabiki Simba, Yanga wakiadhibiwa watakoma

SERIKALI imezuia mapato ya mchezo wa jana kati ya Simba na Yanga uliochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam hadi hapo itakapopata gharama za uharibifu wa samani za uwanjani hapo zilizosababishwa na vurugu.

Pamoja na hayo, serikali imezizuia Simba na Yanga kutumia Uwanja wa Taifa hadi hapo itakapoamua vinginevyo.

Kauli hiyo ilitolewa na Waziri wa Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo, Nape Nnauye, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari katika Uwanja wa Taifa jana, baada ya kufanya ukaguzi wa uharibifu uliofanyika juzi katika mchezo baina ya timu hizo.

Mashabiki wa Simba juzi walifanya vurugu Uwanja wa Taifa baada ya Yanga kupata bao la kuongoza lililofungwa na mshambuliaji Mrundi Amissi Tambwe katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.

Tambwe alifunga bao lake dakika ya 26, akimalizia pasi ndefu ya beki Mbuyu Twite na kugeuka mbele ya beki wa Simba, Novat Lufunga kabla ya kufumua shuti lililomshinda kipa Vincent Angban.

Bao hilo lilizua kizaazaa, wachezaji wa Simba wakimvaa mwamuzi Martin Saanya wakidai mfungaji, Tambwe aliushika mpira kabla ya kufunga.

Katika vurugu hizo, Saanya alimtoa kwa kadi nyekundu Nahodha wa Simba SC, Jonas Mkude dakika ya 29 kwa sababu ndiye aliyekuwa mstari wa mbele kuongoza wenzake.

Mchezo ulisimama kwa takriban dakika tano baada ya mashabiki wa Simba kuanza kufanya vurugu waking’oa viti na kuvutupa uwanjani.

Polisi walitumia milipuko ya gesi za kutoa machozi kuwatuliza mashabiki hao na mchezo ukaendelea kisha Simba kusawazisha dakika ya 87 kwa bao la Shizza Kichuya.

Nape alisema uharibifu huo wa viti, pia mageti mawili ya kuingilia, moja la upande wa Yanga na lingine wa Simba yamevunjwa. Awali ya hapo, Kaimu Mkurugenzi wa Michezo, Alex Nkenyenge alisema zaidi ya viti 1,781 vilivunjwa juzi katika mchezo ambao kati ya Sh. milioni 350 na 400 zilikusanywa katika viingilio vya mashabiki walioingia kwa tiketi za elektroniki.

Nipashe tunaunga mkono hatua yoyote ya awali ya kinidhamu katika vurugu zilizotokea juzi, lakini tunapenda kuishauri serikali ihakikishe inatoa adhabu ambazo zitakuwa suluhusisho la matatizo kama hayo.

Haikuwa mara ya kwanza vurugu kutokea Uwanja wa Taifa, katika mechi ya watani, au mechi za Ligi Kuu, hiyo inamaana sasa imekuwa desturi na inahitaji kukomeshwa.

Njia nzuri ya kuifanya adhabu iwe na tija, ni kuhakikisha inawaumiza moja kwa moja mashabiki ambao ndiyo wafanya fujo na waleta athari zote ambazo hutokea, kama za jana.

Miongoni mwa adhabu hizo ni pamoja na kuizuia mashabiki wa klabu husika kuingia uwanjani timu yao inapocheza kama ambavyo tumekuwa tukiona sehemu mbalimbali duniani.

Nipashe hatupingi adhabu iliyochukuliwa, lakini tunaishauri serikali ikifikirie pia kutoa adhabu ambazo zitawakomesha mashabiki kufanya vurugu.

Habari Kubwa