Matokeo Simba, Yanga yasichafue upepo klabuni

06Jan 2020
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Matokeo Simba, Yanga yasichafue upepo klabuni

BAADA ya tambo zilizodumu tangu kuanza kwa msimu huu wa 2019/2020 wa Ligi Kuu Tanzania Bara, hatimaye miamba ya soka nchini, Simba na Yanga imekutana katika Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam juzi.

Mechi hiyo ya watani wa jadi ilikuwa 'dabi' ya 100 tangu zianze kukutana na Yanga ilishuka dimbani ikiwa imeshinda mara 36 wakati Simba ikishinda mara 28 huku zikitoka sare mara 35.

Hivyo, kwa matokeo ya sare ya mabao 2-2 zilizoyapata juzi, yanaifanya miamba hiyo sasa kutoka sare mara 36 na Yanga ikiendelea kushikilia rekodi ya kushinda mara nyingi zaidi.

Hakika matokeo hayo yanaweza kuwa yasiyotarajiwa hasa kutokana na jinsi kila upande ulivyokuwa ukijinasibu kuibuka na ushindi kabla ya mechi kupigwa.

Simba ambayo ipo kileleni mwa msimamo wa ligi hiyo ilikuwa ikijivunia muunganiko mzuri wa kikosi chake pamoja na ubora wa mchezaji mmoja mmoja.

Kwa upande wa Yanga inayoshika nafasi ya nne kwenye msimamo wa ligi hiyo, bado ilikuwa haijawa na muunganiko mzuri katika kikosi chake, lakini mbali na ubora wa mchezaji mmoja mmoja ilikuwa ikijivunia zaidi namna ilivyokiboresha katika dirisha hili dogo la usajili.

Hata hivyo, pamoja na kila timu kuamini ingeweza kuibuka na pointi tatu muhimu, matokeo yamekuwa tofauti na miamba hiyo imejikuta ikiambulia alama moja moja.

Tunatambua wapo mashabiki waliokwenda uwanjani wakiwa na matokeo yao mkononi kutokana na kuamini usajili walioufanya na ubora wa wachezaji wao.

Hata hivyo, hawana budi kuyapokea matokeo yaliyopatikana na kuganga mbele kwa kuwa mchezo wa soka una matokeo matatu, kushinda, kushindwa ama sare.

Kadhalika, mashabiki wa Simba na Yanga hawana budi kutambua timu hizo ndiyo kwanza zipo mikononi mwa makocha wapya hivyo hawana budi kuwapa muda zaidi.

Simba ipo mikononi mwa Sven Vandenbroeck aliyerithi mikoba ya Mbelgiji mwenzake Patrick Aussems mwezi uliopita wakati Boniface Mkwasa akikaimu mikoba ya Mwinyi Zahera mwezi mmoja na wiki kadhaa sasa.

Hivyo, ni makocha wanaohitaji muda zaidi ili kuweza kuzijenga timu zao na wachezaji kuzoea mifumo na mbinu kutoka kwao.
Tunasema hivyo kutokana na kufahamu chokochoko zinazoweza kujitokeza kutokana na mashabiki ambao huenda uwanjani na matokeo yao, kwani hawa huwa hawakawii kwa kutaka makocha watimuliwe.

Matarajio yetu ni kuona Vandenbroeck na Mkwasa wakipewa muda zaidi kuzijenga timu zao ili zitakapokutana mzunguko wa pili ziweze kutoa burudani nzuri zaidi kwa kuwa kila mmoja atakuwa amepata muda wa kutosha wa kukiimarisha kikosi chake.

Habari Kubwa