Matukio ya moto shuleni yanahitaji ufumbuzi sasa

16Sep 2020
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Matukio ya moto shuleni yanahitaji ufumbuzi sasa

JUZI wanafunzi 10 wa Shule ya Msingi ya Kiislamu Byamungu, iliyoko Kata ya Kyerwa wilayani Kyerwa mkoani Kagera, waliteketea kwa moto kiasi cha miili yao kutofahamika, huku wengine sita wakijeruhiwa baadhi vibaya, kutokana na bweni walilokuwa wamelala kuungua moto ambao chanzo chake hakijajulikana.

Tukio hili ni la tano kutokea kwa shule za sekondari na msingi za kiislam nchini ikiwa ni matukio mawili kwenye shule hiyo ambayo hayakusababisha madhara yoyote.

Mengine ni kwa Shule ya sekondari ya Ilala Islamic iliyoungua mwezi Julai, mwaka huu na kusababisha vifo vya wanafunzi wawili pamoja na shule ya Mivumoni Islamic iliyopo Msikiti wa Myambani Kinondoni mkoani Dar es Salaam, ambako mali ziliteketea kwa moto.

Baada ya matukio hayo ya mfululizo kwa Jiji la Dar es Salaam, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, aliagiza Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, kuunda kamati ya kuchunguza tukio hilo.

Aidha, baada ya kutokea tukio la shule ya Byamungu, Mkuu wa mkoa wa Kagera, Brigedia Jenerali Marco Gaguti, alitangaza kuundwa kwa kamati ya kuchunguza chanzo cha matukio ya moto kwenye shule hiyo ili kuchukua hatua zaidi.

Licha ya kamati zote kutotangaza walichobaini mbele ya umma, lakini bado yapo maswali mengi na magumu ya kujiuliza juu ya hiki kinachotokea ambacho kinaendelea kusambaa na sasa madhara yamekuwa makubwa.

Maswali haya ni je, shule hizi zinachomwa moto au zinaungua ikiwa ni majanga kama majanga mengine, je, ni matukio ya kawaida kabisa au yana ajenda nyuma ya pazia, je, ni kwanini shule zinazoungua ni za Jumuiya moja pekee? Je, kamati zimebaini nini na hatua gani zimechukuliwa ili kupeusha, Je, ni miundombinu ya muda mrefu?

Lakini kubwa tunajiuliza ni kwa namna gani ofisa elimu na wakaguzi wa elimu waliridhika na majengo hayo na kuruhusu yaendele kutumiwa na wanafunzi 74.

Ni lazima maswahi haya yajibiwe kupitia kamati zilizoundwa, na kubwa zaidi lipatikane jibu ni kwanini shule zinazoungua ni hizi na kwanini hali iko hivyo?

Matukio haya yanatoa taswira kuwa lipo tatizo la msingi sana katika miundombinu ya shule hizi, na badala ya kufanya jambo kwa zima moto wa kundana na upepo uliopo ni wakati wa kuhakikisha shule zinakaguliwa mara kwa maa na ndiyo maana kuna wakaguzi wa elimu.

Katika moja ya mahojiano, Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, IGP Simon Sirro, alisikika akishangaa jinsi miundombinu ya shule hiyo ilivyokuwa dhaifu, huku akihoji ilikuwaje wakaguzi na ofisa elimu kuruhusu shule hiyo kuwa na wanafunzi.

Maswali anayojiuliza ndiyo wanayojiuliza Watanzania kwamba shule yenye miundombinu dhaifu kiasi hicho inaruhusiwaje kuendelea kuhifadhi wanafunzi, na kama ukaguzi ungefanyika inavyotakiwa maana yake hatua zingeeshachukuliwa.

Kuna wakati ilitokea tukio la ajali ya gari kwa wanafunzi wa Shule ya Msingi Lucky Vincent jijini Arusha, na kusababisha vifo vya wanafunzi 32, hatua zilizochukuliwa kwa haraka ambazo kwa sasa hazisimamiwi na baadhi ya shule ni kuelekeza magari ya kupakwa rangi ya njano.

Kwa sasa baadhi ya magari yanabeba wanafunzi, lakini hayana vigezo vya kisheria vya kufanya hivyo, jambo hili likiachwa maana yake yakitokea maafa mengine ndiyo utakuja mkakati mwingine.

Tunasema suala hili la matukio ya moto kwenye hizi shule lifanyiwe uchunguzi wa kina, hatua zichukuliwe kwa uzembe wowote uliojitokeza, kuwapo na uwajibikaji kuanzia mmiliki wa shule hadi watumishi wa shule na mamlaka za serikali.

Hatuoni tija kwa kufumbia udhaifu unaosababisha matukio haya, badala yake kuanza kutafuta ‘mchawi’ kila majanga ya moto kwenye shule.

Habari Kubwa