Mauaji haya yanatia hofu kwenye jamii

13Jan 2022
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Mauaji haya yanatia hofu kwenye jamii

MATUKIO ya mauaji kutoka ndani ya familia yameendelea kutikisa katika kipindi cha miezi ya hivi karibuni na yanaendelea kutokea na kuleta taharuki kubwa.

Katika vyombo vya habari karibu kila siku kunaripotiwa taarifa za mauaji yakiwamo ya wivu wa mapenzi na mengine ya kutaka kurithi mali kwa nguvu.

Binadamu wamekosa utu na kudiriki kufanya vitendo ambavyo hata wanyama ni vigumu kuvifanya.

Taarifa mbalimbali za watu kuua binadamu wenzao kwa kuwachinja, kujinyonga au kunyonga, kumwagiana petroli na kuchomana moto, havikosi kusikika masikioni na machoni mwa watu.

Katika matukio hayo kunaripotiwa visa mbalimbali vya wanandoa kuuana au kujiua kwa sababu ya wivu wa kimapenzi.

Matukio mengine ni ya watoto kuua wazazi wao kwa tamaa ya kumiliki mali. Ukiangalia visa vyote hivyo vinatokana na watu wa karibu ndani ya familia.

Hali hii inasikitisha na inatisha na kama hatua za haraka hazitachukuliwa familia nyingi zitaendelea kuteketea.

Ni vizuri wataalamu wa mambo ya saikolojia na watu wa ustawi wa jamii wakaingilia kati kudhibiti hali hii isiendelee kuangamiza familia.

Suala hili pia linahitaji nguvu ya pamoja na shirikishi kutoka kwenye familia pale inapoonekana dalili ya kutokea kwa vitendo hivyo.

Kuna baadhi ya wanaodhamiria kufanya vitendo hivyo kwa kumtamkia wazi mtu anayetamka kumdhuru, basi inapotokea hivyo ni vizuri kuripoti mapema kwa ndugu wa karibu au kwa wataalamu wa saikolojia ili liweze kudhibitiwa.

Katika ngazi ya familia wapo wanaoshuhudia dalili hizo mapema pengine kwa watoto kushinikiza wazazi wao kutaka kurithishwa mali mapema badala ya kusubiri mpaka wazazi waage dunia. Kwa kweli hali inatisha na hii yote inasababishwa na tamaa ya kuiga maisha ya watu wengine wenye uwezo na kutaka kufanana nao.

Hao waliofanikiwa walivitafuta kwa kufanyakazi mpaka vikapatikana, hakuna kitu kinachopatikana kirahisi bila kukitolea jasho. Na hili la tamaa ya mali linafanyika sana kwa vijana kwa kuiga maisha ya watu wanaojiposti kwenye mitandao.

Na mara nyingi mauaji hayo yanapofanyika, huyo aliyetekeleza huishia mikononi mwa dola na hiyo mali akiiacha ikiteketea.

Elimu kubwa inahitajika hasa kwa viongozi wa dini kwenye nyumba za ibada kuwasihi watu kumwogopa Mungu.

Mauaji yote yanayofanyika mwisho wake wanaoyatekeleza huishia gerezani au kuharibikiwa kabisa kimaisha.

Kwa wale wanaowaua wenzi wao kwa sababu ya wivu wa mapenzi, ni bora mtu anapoona mwenzake anakwenda kinyume, kukaa kifamilia na kuyazungumza na kama ikishindikana kila mtu atafute njia yake badala ya kutoana uhai. Siku zote hasira ni hasara.

Kila familia ina jukumu la kufuatilia kinachoendelea kwenye familia yao ili kuepusha hali hii inayoendelea kutokea kila kukicha na kuleta taharuki kubwa. Inasababisha hata mzazi kumwogopa mtoto wake aliyemzaa.

Dalili zinapoanza kujitokeza ni vizuri kudhibiti mapema. Moja ya dalili hizo ni mtu kupenda kujitenga peke yake, kutamka maneno ya kuua au kujiua, kuwa mkimya bila sababu, zote hizo zikionekana ziripotiwe na kudhibitiwa.

Ushirikiano ukitolewa vitendo hivyo vya mauaji vitadhibitiwa kwa watu kupewa ushauri nasaha.

Habari Kubwa