Mawaziri chapeni kazi

15Sep 2021
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Mawaziri chapeni kazi

JUMAPILI, Rais Samia Suluhu Hassan, alifanya mabadiliko madogo ya mawaziri, huku akifanya mabadiliko ya kimuundo kwa kuiondoa Idara ya Habari (Maelezo) kutoka Wizara ya Habari na kuipeleka Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia.

Kwa mawaziri watatu ambao wameteuliwa na kurejea kwenye uwaziri January Makamba (Nishati), Prof. Makame Mbarawa (Ujenzi na Uchukuzi) na Ashatu Kijaji (Habari, Teknolojia na Mawasiliano), wanakabiliwa na mtihani mgumu katika utekelezaji wa majukumu yao.

Rais Samia alisema hajaweka nukta bali ameweka koma kwa kuwa bado anaendelea na mabadiliko ya watendaji mbalimbali, ambao wako chini ya mamlaka yake ya uteuzi, ikiwa ni namna ya kutuma salamu kwa wateule kufanyakazi kwa bidii na kufikia malengo tarajiwa ya kuhudumia umma.

Alisema wateule wasitarajie kwa maumbile na malezi yake wamuone akifoka, na kwamba hatafanya hivyo kwa kuwa anafanyakazi na watu wazima wanaojua jema na baya na ni imani yake wanapozungumza wanaelewana na kila mmoja anajua wajibu wake, na pale itakapomlazimu kufoka atafoka kwa kalamu.

Aidha, alisema amejichagulia njia yake mwenyewe na anachokitaka ni serikali kuendeshwa kwa matendo makali kwa kutoa huduma muhimu kwa wananchi.

Pia, rais aligusia suala la machinga ambalo ni tatizo kubwa kwa miji na majiji , huku akiwaelekeza wakuu wa mikoa na wilaya kuwapanga badala ya kuwabughudhi.

Ni muhimu wateule wakatekeleza wajibu wao kwa kuhudumia wananchi kwa kuwa msingi wa yote ni kuwatumikia walipakodi pamoja na utatuzi wa kero zao.

Tunampongeza Rais kwa kusikia kilio cha vyombo vya habari nchini kwa kuunganisha vyombo vya magazeti, redio, TV na digital kusimamiwa na wizara moja, tofauti na awali.

Tasnia ya habari tuna matarajio makubwa kwa Waziri Dk. Kijaji, kwa kuwa maumivu ya kufungiwa kwa chombo cha habari ni makubwa na haiathiri chombo husika bali waajiriwa na wategemezi wao na uchumi wa nchi kwa kuwa hawataweza kulipa kodi stahiki.

Malalamiko ya wadau ni kukosekana kwa meza au kusikiliza madai yanayotolewa dhidi ya chombo husika kabla ya hukumu, au wakati mwingine hukumu kutoka bila kugusa utetezi wa waliotuhumiwa, na matokeo yake inaleta taswira mbaya kwa nchi katika uhuru wa kujieleza na upatikanaji wa taarifa.

Pia wadau wa habari wana malalamiko dhidi ya Sheria ya Huduma za Habari ya mwaka 2016 na kanuni za utangazaji, hivyo tunaamini kwa kuwa chini ya waziri mmoja sasa changamoto nyingi zitatuliwa na kuondoa malalamiko.

Kwenye Wizara ya Nishati, Makamba, anakabiliwa na kibarua cha kuhakikisha wananchi wanaunganishiwa umeme hasa vijijini, kasi ya kubadili nguzo za mbao kwenda za zege, usambazaji wa gesi kwenye makazi ya watu na viwandani pamoja na kuhakikisha bei ya mafuta haizidi kupaa kwa sababu za ndani.

Kwa upande wa Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa, kibarua ni kizito zaidi kwa kuwa kuna mradi mingi ya ujenzi ambayo inapaswa kukamilika ikiwamo reli ya kisasa na ianze kutumika kwa kadri ya muda wa mradi, ujenzi wa vivuko/ meli, ujenzi wa kiwanja cha ndege cha Msalato, Dodoma, madaraja na barabara za miji na majiji. Pia ununuzi wa meli kwenye maziwa.

Miradi hii yote inahitaji usimamizi wa karibu kwa kuwa inatumia mabilioni ya fedha, ambazo ni za Watanzania, lakini kukamilika kwake ni neema kwa kuwa huduma za usafiri zitakuwa rahisi na haraka, pamoja na maendeleo ya kiuchumi kwa taifa.

Tunafikiri ni muhimu kwa kila kiongozi kuwajibika kwa kuwa hakuna sababu kwa nchi tajiri kwa rasilimali kama Tanzania kuwa na watu maskini, au tatizo la ajira kuendelea kukua kiasi cha kuzalisha machinga wengi kuliko wafanyabiashara wengi, ambao wataajiri wengine na kulipa kodi sahihi.