Mbeya City kujinasua mkiani 'dabi' ya Mbeya Jumamosi?

28Sep 2020
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Mbeya City kujinasua mkiani 'dabi' ya Mbeya Jumamosi?

LIGI Kuu ya Vodacom Tanzania Bara Msimu wa 2020/21 inayoshirikisha timu 18 imefikia mzunguko wa nne kwa kila timu kushuka dimbani mara nne.

Mbeya City ambayo ni miongoni mwa timu tatu za Mkoa wa Mbeya zinazoshiriki ligi hiyo pamoja na timu za Ihefu FC na Tanzania Prisons ambayo kwa sasa wamehamia mkoani Rukwa wakitumia Uwanja wa Nelson Mandela kama dimba lao la nyumbani.

Tangu msimu huu ulipoanza, Mbeya City ni timu ambayo imeonekana kuwa kibonde kuliko timu nyingine yoyote ambapo mpaka sasa imecheza michezo minne na kupoteza yote.

Mpaka sasa timu hiyo inaburuza mkia kwenye msimamo wa ligi hiyo ikiwa haina alama na ndiyo timu inayoongoza kwa kufungwa magoli mengi ambapo mpaka sasa nyavu zake zimetikiswa mara saba.

Mbali na kuongoza kufungwa magoli mengi, pia Mbeya City ni miongoni mwa timu tatu ambazo hazijafanikiwa kupata bao hata moja kwenye michezo yote minne iliyocheza.

Mechi ya kwanza Mbeya City walikubali kupokea kichapo kizito cha mabao 4-0 kutoka kwa watoza ushuru wa Manispaa ya Kinondoni timu ya KMC ya jijini Dar Es Salaam kwenye mchezo namba saba uliopigwa Uwanja wa Uhuru.

Baada ya hapo wagonga Nyundo hao wa Jiji la Mbeya walipokea kichapo kingine cha bao 1-0 kutoka kwa timu ya Wananchi, Yanga kwenye Uwanja wa Mkapa ambao ulikuwa mchezo wa pili wa timu hiyo kucheza ugenini.

Mtazamo wa wengi ulikuwa ni kwamba timu hiyo ilipoteza michezo hiyo kwa sababu ya kuwa ugenini na hivyo mashabiki na wapenzi wengi wa timu hiyo walitarajia mabadiliko kwenye michezo ya nyumbani.

Hata hivyo, mambo yalienda ndivyo sivyo baada ya Septemba 20 timu hiyo ikicheza mchezo wake wa kwanza nyumbani kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine dhidi ya 'Waokamikate' wa Chamazi, Azam FC walikubali kupokea kichapo cha bao 1-0.

Katika mechi hiyo ambayo ilikuwa ya kwanza kwa Mbeya City kucheza wakiwa nyumbani, walionyesha mchezo mzuri hali ambayo ilianza kufufua matumaini kwa mashabiki wake, lakini wakaghadhabishwa na baadhi ya maamuzi ya mwamuzi wa mchezo huo, Jackson Samwel kutoka mkoani Arusha wakidai alikuwa anaibeba Azam.

Moja ya matukio waliyokuwa wanayalalamikia mashabiki hao ni mshambuliaji wa timu yao, Kibu Denis, kutembezewa kiatu kwenye eneo la hatari wakiamini ilipaswa kutengwa mkwaju wa penalti, lakini mwamuzi aliamuru ipigwe kona.

Mashabiki hao walifanya vurugu ikiwamo kurusha chupa uwanjani wakati mchezo huo ukiendelea na baada ya mchezo huo kumalizika waliendelea kuwatafuta waamuzi ambapo Jeshi la Polisi likaingilia kati kwa kuwatorosha waamuzi hao.

Vurugu hizo zilisababisha timu hiyo ya Mbeya City, kupigwa faini ya Sh. 500,000 na Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi ya Bodi ya Ligi Kuu Tanzania Bara (TPLB).

Uwezo mzuri wa Mbeya City kwenye mchezo dhidi ya Azam, uliwavutia mashabiki wengi kujitokeza kwenye mechi yao ya Ijumaa dhidi ya 'Walimakorosho' kutoka Ruangwa mkoani Lindi, Namungo FC.

Pamoja na kujitokeza kwao kwa wingi, kama kawaida "la kuvunda huwa halina ubani", kwani wakati timu yao ilipokubali kipigo cha bao 1-0 kwenye uwanja wao wa nyumbani, wakatoka uwanjani hapo vichwa chini.

Baadhi ya mashabiki hao walijaribu kutaka kufanya tena fujo kwa kuingia uwanjani mchezo ukiwa unaendelea, lakini wakadhibitiwa na viongozi wa timu hiyo.

Baada ya vichapo hivyo, sasa mechi inayofuata nyumbani ni 'dabi ya Mbeya' dhidi ya mahasimu wao, Tanzania Prisons itakayopigwa Ijumaa wiki hii. Je, Kocha Mkuu wa Mbeya City, Amri Said, ataanza rasmi ligi kwa kuibuka na ushindi ama angalau sare katika dabi hiyo? Ni suala la kusubiri kuona.

Hata hivyo, Mbeya City inakwenda kukutana na Prisons ambayo msimu huu imeonyesha kandanda safi na la kuvutia licha ya kupoteza michezo yake miwili kati ya minne ambayo imeshacheza hadi sasa.

Prisons ambayo ipo nafasi ya 11 kwenye msimamo wa ligi hiyo ikiwa na alama nne, imeshinda mechi moja na kushinda mmoja, lakini imeruhusu nyavu zake kutingishwa mara nne tu huku washambuliaji wake wazifumania zile za wapinzani mara tatu, hakika itakuwa 'dabi' ya kibabe na ya kuvutia zaidi.

Habari Kubwa