Mfumo madhubuti muhimu udhibiti mapato utalii

06Dec 2017
Mhariri
Nipashe
Mfumo madhubuti muhimu udhibiti mapato utalii

JITIHADA kadhaa zimekuwa zikifanywa na serikali katika kusimamia sekta ya utalii, ili mapato zaidi yapatikane. 

Hata hivyo, pamoja na jitihada kubwa zinazofanywa na serikali ya awamu ya tano kudhibiti mianya ya upotevu wa mapato, bado inakosa mabilioni ya fedha kutokana na ufanisi duni wa ukusanyaji kwenye sekta ya utalii.

Ripoti maalum iliyochapishwa na gazeti hili toleo la juzi ilieleza kwa undani kuhusiana na udhaifu uliopo hususan wa kimfumo na kusababisha kupotea kwa mabilioni ya shilingi ya mapato hayo.

Pamoja na Wizara ya Maliasili na Utalii kukiri kuwapo kwa changamoto hiyo, imebainika azma ya serikali kuwa na watalii milioni nane na fedha za kigeni Dola za Marekani bilioni 20 (Sh. trilioni 43.7) kwa mwaka kufikia mwaka 2025, iko hatarini kutotimia kwa sababu ya kukosa mfumo madhubuti katika kufuatilia idadi ya watalii wanaolala kwenye hoteli na mabanda ya watalii.

Ripoti kadhaa za wizara hiyo na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) zinaonyeha udhaifu katika udhibiti wa mapato ya sekta hiyo inayochangia asilimia 25 ya fedha zote za kigeni nchini.

Ripoti ya CAG kuhusu Ukaguzi wa Mashirika ya Umma kwa mwaka wa fedha 2015/16, pia ilibainisha kuwa kukosekana kwa mfumo madhubuti wa kudhibiti malipo ya huduma za hoteli za kitalii ni moja ya changamoto zinazofifisha mchango wa sekta ya utalii kwenye uchumi.

Kutokana na hali hiyo, CAG alibainisha serikali inapoteza mapato kwenye mikataba ya upangishaji hoteli, nyumba za kupangisha na kambi za kulala watalii kwa kukosa chombo cha kufuatilia malipo ya wageni katika hoteli hizo.

CAG alieleza kwenye hoteli, nyumba za kupangisha na kambi za kulala watalii, wanapaswa kuilipa serikali kupitia Shirika la Hifadhi za Taifa (Tanapa) tozo ya kuendesha biashara ndani ya eneo la mamlaka hiyo.Ripoti yetu ilimkariri Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Japhet Hasunga, alikiri kuwapo kwa changamoto za kimfumo kudhibiti mapato ya serikali yatokanayo na malipo ya watalii wanaolala kwenye hoteli na kambi za watalii nchini.  

Alibainisha alitembelea maeneo mengi na kupewa taarifa kuwa Tanapa wana mfumo wa kufuatilia malipo ya watalii, lakini unatofautiana na unaotumika kwenye mamlaka nyingine.

Alisema serikali imeona kuna haja ya kuwa na mfumo mmoja ambao mtalii akiingia Uhamiaji, anaonekana mara moja kwa mamlaka zote zinazohusika na utalii, hivyo kuziwezesha kupeana taarifa na kujua hoteli anayolala na watahakikisha hoteli zote zinaunganishwa na mfumo huo.

Hata hivyo, Mkurugenzi Mkuu wa Tanapa, Allan Kijazi, alisema mfumo upo, lakini kudhibiti mapato ya utalii, ingawa alibainisha kuna kikosi kazi kimeundwa kusaka mbinu za kuitafutia ufumbuzi changamoto hiyo.

Ripoti maalum ya Nipashe ilieleza kwa kina jinsi kukosekana kwa mfumo madhubuti kunavyolipotezea Taifa fedha nyingi za mapato ya utalii kutokana na wajanja wachache kuutumia udhaifu huo kwa manufaa yao binafsi.

Suluhisho la changamoto hiyo ni kupatikana kwa mfumo madhubuti wa pamoja wa kudhibiti mapato yatokanayo na utalii ambao utazihusisha mamlaka mbalimbali kama Tanapa, Mamlaka ya Mapato (TRA), Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro na Uhamiaji ili mtalii anapoingia katika hoteli taarifa zake zionekane kila mamlaka. 

Ni matarajio yetu kuwa kikosi kazi kilichoundwa na serikali kitafanya kazi yake kwa umakini na weledi mkubwa na kukamilisha kazi kiliyopewa pamoja na kukabidhi taarifa yake kufikia mwezi ujao ili uamuzi ufanyike, ambao utadhibiti kupotea kwa mapato ya nchi. 

Habari Kubwa