Mfumo wa vyama vingi vya siasa uheshimiwe

10Dec 2019
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Mfumo wa vyama vingi vya siasa uheshimiwe

TANZANIA ilirejesha mfumo wa vyama vingi vya siasa mwaka 1992, baada ya kufutwa kwa mujibu wa sheria mwaka 1965.
Urejeshaji wa mfumo wa vyama vingi vya siasa ulirejeshwa kwa Sheria Namba 5 ya Julai Mosi, 1992.

Kwa maana hiyo, mfumo huu bado upo kisheria na vyama vya siasa vyenye usajili wa kudumu ni halali kwa kuwa vipo kisheria.

Vyama vyenye usajili wa kudumu zaidi ya 20 vilivyopo nchini ni halali kufanya shughuli zao za kisiasa kwa mujibu wa sheria, taratibu na kanuni ikiwamo kufanya mikutano, kushiriki uchaguzi, kupeperusha bendera, kwa kutaja baadhi.

Tumelikumbusha jambo hili ili kila mtu aelewe au kama amesahau akumbuke, kwa kuwa inawezekana halieleweki vizuri kwa baadhi ya watu au wanalipotosha.

Kwa mfano, baadhi ya vyombo vya habari jana vilichapisha habari iliyomkariri.

Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga mkoani Rukwa, Dk. Halfan Haule, akiwaagiza wenyeviti wa serikali za mitaa na vitongoji kwenye Manispaa ya Sumbawanga kuondoa bendera zote za vyama vya upinzani na kuziacha za Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa kuwa ndicho chama tawala.

Agizo hilo alilitoa mwishoni mwa wiki, baada ya wenyeviti hao kula kiapo kufuatia kushinda katika uchaguzi wa serikali za mitaa uliofanyika Novemba 24, mwaka huu.

Mkuu huyo wa wilaya aliwaagiza wenyeviti hao kuzing'oa bendera zote za vyama pinzani kwa madai kuwa zitakuwa zikiwachanganya wananchi.

Alisema CCM ndicho chama kilichoshinda uchaguzi huo kwa asilimia 100, hivyo hakuna sababu ya bendera za vyama vingine kupeperushwa, huku akiahidi kupita mitaani kukagua utekelezaji wa agizo lake.

Kwa mujibu wa Dk. Haule, utekelezaji wa agizo hilo ni mkakati wa kuhakikisha hata katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2020 hakuna diwani atakayeshinda kutoka chama cha upinzani.

Kwamba hataki kuziona zikipepea kwenye nyumba ya mtu yeyote, na atakayebisha atakamatwa na kumfungulia shtaka la kusababisha uchafu, na atakwenda jela mwezi mmoja au kulipa faini ya Sh. 50,000.

Kadhalika, aliwaagiza wenyeviti hao kuhakikisha hata kwenye mpango wa kusaidia kaya maskini unaotekelezwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (Tasaf) wanawaondoa wale wote ambao ni wanufaika wanaunga mkono vyama vya upinzani.

Katika hali ya kawaida, tunazichukulia kauli za DC huyo kuwa zinakiuka sheria na katiba ya nchi, kwa kuwa vyama vya siasa vinaruhusiwa kuwapo na kufanya shughuli zao kisheria.

Mazingira pekee yanayoweza kusababisha chama chochote kufutwa kwenye daftari la Msajili wa Vyama vya Siasa ni kile ambacho kitakwenda kinyume cha Sheria ya Vyama vya Siasa.

Ikumbukwe kuwa tangu kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vingi vya siasa nchini, ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa imeshavifuta baadhi ya vyama vikiwamo PONA, TPP, CHAUSTA, APPT-Maendeleo na Jahazi Asilia kwa kwenda kinyume cha sheria hiyo.

Kwa hiyo matamshi ya Mkuu huyo wa Wilaya yanaweza kutafsiriwa kuwa ni ya uongo, kibaguzi, yanaweza kusababisha uvunjifu wa amani na yanakwenda kinyume cha utawala bora.

Ni matarajio yetu kwamba Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi, atatoa tamko la kuweka jambo hili sawa, na ikiwezekana kutoa karipio dhidi ya matamshi ya aina hii yanayoweza kuhatarisha amani ya nchi.

Ni matumaini yetu pia kuwa mamlaka nyingine za juu zitachukua hatua kwa kuwapa maelekezo viongozi waliopewa dhamana kama wakuu wa wilaya kujiepusha kutenda mambo yanayokwenda kinyume cha utawala bora. Bado tunasisitiza kuwa mfumo wa vyama vingi vya siasa uendelee kuheshimiwa.

Habari Kubwa