Mgawanyo wa keki ya taifa  ulenge kwenye maendeleo

11Jun 2021
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Mgawanyo wa keki ya taifa  ulenge kwenye maendeleo

JANA bajeti ya serikali imesomwa ambayo imeonyesha mgawanyo wa keki ya taifa ya Sh. tilioni 36.26 kuhakikisha kila Mtanzania ananufaika, ili kutambua umuhimu wa kutunza na kulinda rasilimali za madini, maliasili na nyinginezo.

Kabla ya kufanyika kwa mgao huo, sekta mbalimbali kupitia wizara zao waliwasilisha makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka 2021/22, ambazo zilipitishwa na bunge baada ya mijadala ya kina.
 
Watanzania wanataka kuona namna keki ya taifa inagawanywa na kiasi kikubwa kitekeleze miradi ya maendeleo kama elimu, afya, kilimo, mifugo na uvuvi, maji na miundombinu ambayo inagusa maisha ya watu moja kwa moja.
 
Mathalani, katika makadirio ya mapato na matumizi kwa wizara za kilimo, ujenzi na uchukuzi, maji, afya, ilionyesha utekelezaji wa bajeti iliyopita siyo wa kuridhisha kwa kuwa fedha zilizotengwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo hazikutolewa.
 
Katika kitabu cha kamati ya Bajeti ilielezwa kuwa katika mafungu saba yaliyo chini ya Wizara ya Fedha na Mipango hadi Aprili mwaka huu, utekelezaji wa bajeti ni asilimia 68.4, ikiwa ni matumizi ya kawaida asilimia 71.6 na matumizi ya fedha za maendeleo asilimia 1.4.
 
Hiyo ni wizara moja, huku zile zinazogusa maisha ya wananchi kwa asilimia 100 zikipata fedha kiduchu, huku fedha nyingi ikielekezwa kwenye matumizi ya kawaida.
 
Wabunge mara kadhaa walitishia kuondoa shilingi kwenye mshahara wa Waziri, lakini serikali iliwahakikishia kutekeleza bajeti kwa muundo wa kugusa maisha ya watu na ndiyo maana walikubali kupitisha.
 
Kila wizara ilieeleza kushindwa kutekeleza miradi ya maendeleo kutokana na ukosefu wa fedha, wabunge walipaza sauti zao kuhusu kusuasua kwa miradi ya barabara ambayo athari yake inaonekana kwenye afya kwa kuwa watu watashindwa kuzifikia huduma za afya, kumtua mama ndoo kichwani na mingine inayogusa maisha ya watu moja kwa moja.
 
Pia, miradi ya afya ya ujenzi wa zahanati, vituo vya afya na hospitali pamoja na vifaa tiba nayo ilionekana ni kikwazo hata maboresho ya jumla ya huduma za afya, kiasi cha wengi kushindwa kupata huduma sahihi kwenye maeneo ya huduma ya umma.
 
Ni wazi kuwa bado mgawanyo wa keki ya taifa haufanyika kwa kutoa kipaumbele kwa miradi ya maendeleo, ambayo hugusa maisha ya wananchi moja kwa moja, bali fedha nyingi kutumika kulipa watendaji.
 
Ili bajeti iwe na maana kwa mwananchi wa kawaida, ni lazima aone inagusa maisha yake moja kwa moja kupitia huduma za kijamii kama afya, maji, miundombinu na elimu.
 
Tunaamini kuwa fedha nyingi za bajeti zitaelekezwa kwenye maendeleo, kutokana na alivyoeleza jana Waziri wa Fedha na Mipango, Mwigulu Nchemba, alipokuwa akiwasilisha bungeni jana asubuhi Taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa kwa mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2021/22 kabla ya kusoma bajeti wakati wa jioni, kwamba miradi itagusa maisha ya watu.

Habari Kubwa