Mifuko iwalipe mafao wastaafu kwa wakati

08Apr 2021
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Mifuko iwalipe mafao wastaafu kwa wakati

JUZI Rais Samia Suluhu Hassan, aliwafumbua macho Watanzania juu ya ya kifedha ya Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF), kuwa ni mbaya na ndiyo sababu hajateua Mkurugenzi Mkuu.

Aidha, alibainisha kuna kazi ya kufanya ili kuunusuru mfuko huo ili kujua nini la kufanya.

Hadi mwaka 2018 Tanzania ilikuwa na mifuko ya hifadhi ya jamii mitano Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) kwa ajili ya watumishi wa sekta binafsi, Mfuko wa Pensheni wa Mashirika ya Umma (PPF), Mfuko wa Pensheni kwa Watumishi wa Umma (PSPF), Mfuko wa Akiba wa Watumishi wa Serikali za Mitaa (LAPF) na Mfuko wa Mafao ya Kustaafu (GEPF).

Sheria ya Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa umma namba 2 iliyopitishwa na Bunge Januari 31 mwaka 2018 iliunganisha mifuko ya PPF, PSPF, LAPF na GEPF, kuunda mfuko wa PSSSF ambao unawajibu wa kuhudumia watumishi wa umma.

Sheria mpya ndiyo ilileta kikokotoo kipya ambacho kilitaka mstaafu kulipwa malipo ya mkupuo ya asilimia 25, huku asilimia 75 akilipwa kidogo kidogo, utekelezaji ambao kabla ulikuwa uko NSSF, huku mifuko mingine ikiwamo PSPF wakilipa asilimia 50.

Tunakumbuka aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii (SSRA), Dk. Irene Isaka, alivyokaririwa kuwa iwapo utaendelea utaratibu wa zamani, upo uwezekano wa PSPF kushindwa kujiendesha na kulipa wastaafu wake.

Tunafahamu kuwa hifadhi ya jamii ni muhimu sana, kwa kuwa ndiyo maisha ya baadaye ya wastaafu wengi, kwamba wamekatwa fedha zao na kama walikidhi vigezo vya kuchangia michango 180 kwa miaka 15, mfululizo wanastahili ya kulipwa mafao.

Mifuko hiyo baada ya kuunganishwa ilikuja na mafao mapya kutoka kwenye ile ya awali iliyokuwa ina mafao saba ambao ni pensheni ya uzeeni, fao la ulemavu, fao la walithi, fao la upotevu wa ajira, fao la ugonjwa, fao la uzazi na mkopo wa nyumba.

Yote haya ni namna ya kumfanya mstaafu aendelee kuishi maisha mazuri baada ya kumaliza utumishi wake, lakini kama mfuko unakuwa taabani maana yake kuna shida ambayo ni lazima hatua zichukuliwe.

Mbali na baada ya kustaafu hata mafao muhimu kama ya uzazi na mengine mtu hatayapata licha ya kila mwezi kukatwa fedha kwa mujibu wa sheria.

Kwa muda mrefu, kuna kilio cha wastaafu wengi wa kwa mujibu wa sheria yaani waliostaafu kwa hiyari kwa umri wa miaka 55 na wa lazima wa miaka 60, kunyimwa au kuzungushwa kulipwa mafao yao kwa sababu ambazo hazijawekwa hadharani kwa usahihi.

Aidha, kumekuwa na ucheleweshaji na uhakiki wa mara kwa mara wa wastaafu ambao wakati mwingine umekuwa ni usumbufu kwa wastaafu kusafiri umbali mrefu, huku wengi wakiwa ni wazee wanaojiuguza maradhi mbalimbali.

Hakuna ubishi kuwa kila mmoja ni mstaafu mtarajiwa, hivyo ni lazima stahiki za wastaafu zinatuzwa vizuri na siyo fedha kutumika kinyume na inapofika wakati wa kulipa inashindikana na wengi kutaabika.

Mathalani, mtu anapostaafu anatarajia ndani ya miezi mitatu awe amelipwa haki yake, lakini kwa sasa wapo wanaomaliza mwaka mzima bila kulipwa, huku wengine wakikimbilia kwenye vyobo vya habari.

Mbaya zaidi ni wale ambao hawakutimiza umri wa kulipwa mafao yaani nikuchangia mfululizo miezi 180 na sasa wanatakiwa kulipa michango yao walioyokuwa wamechangia kwenye mfuko, nao kumekuwa na shida kubwa ya kuwalipwa.

Tunaiomba serikali kulitizama suala hili kwa jicho la pekee kuhakikisha wastaafu wanaostaafu kila mwaka wanapata malipo ya mkupuo pamoja na ya kila mwezi kwa mujibu wa sheria, ili kuwa na ustaafu wenye hadhi na siyo kuhangaika wakati fedha zake zilikuwa zinakatwa kila mwezi kwenda kwenye mfuko husika.

Habari Kubwa