Mikakati zaidi inahitajika sasa kumaliza changamoto za maji

19Jul 2016
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Mikakati zaidi inahitajika sasa kumaliza changamoto za maji

JANA maadhimisho ya sita ya Wiki ya Maji barani Afrika yalifunguliwa rasmi jijini Dar es Salaam, sambamba na Mkutano wa 10 wa Baraza la Mawaziri wa Maji wa nchi za Afrika.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, aliufungua mkutano huo ambao unaambatana na maonyesho ya shughuli za wadau wa sekta ya maji na umwagiliaji na kusema kuwa pamoja na mipango ya nchi hizo kukabiliana na tatizo la maji, lakini hazijafanikiwa kusambaza maji hususani maeneo ya vijijini.

Alisema ingawa Tanzania imepiga hatua, lakini nchi nyingi hazijafanikiwa na kutoa wito kwa watatafiti, mawaziri, watunga sera na wadau wengine waliohudhuria mkutano huo kuwa kujadili changamoto hiyo na kuondoka na jawabu ili kila nchi iende kutumia vyanzo vyake vya maji kuondokana na tatizo la upatikanaji wa maji.

Pamoja na Serikali kwa sasa angalau kuonyesha jitihada za kukabiliana na uhaba wa maji hususan katika baadhi ya maeneo likiwamo Jiji la Dar es Salaam, lakini katika maeneo mengi nchini wananchi wanakabiliwa na uhaba wa maji. Kinamama wa vijijini wanatembea umbari mrefu kusaka maji na wengine wakiwa na watoto migongoni.

Kupotea kwa maji kutokana na hujuma ikiwamo kujiunganishia maji kienyeji na kukata mabomba pamoja na baadhi ya watu kutojali imeendelea kuwa changamoto kubwa, ambayo inahitaji kufanyiwa kazi zaidi.

Lakini pia mabadiliko ya tabianchi limeendelea kuwa tatizo kubwa na kuathiri sana upatikanaji wa maji ya uhakika kutokana na vyanzo vingi kukauka. Pia kuna watu kadhaa ambao wanategemea sana uvunaji wa maji ya mvua na baadhi huyavuna na kuyatumia kwa muda mrefu, hivyo kukosekana kwa mvua ya uhakika kunakwamisha uvunaji wa maji.

Tunaamini kuwa kupitia mkutano huo, nchi za Afrika zitapeana uzoefu na kupanga mikakati ya pamoja ya kukabiliana kwa na changamoto zilizopo. Kwa kuwa suala la maji linamgusa kila binadamu, bila shaka nchi za Afrika zitaunganisha nguvu ikiwamo kutekeleza kwa pamoka miradi mikubwa ya maji.

Kwa upande wa Tanzania ni wakati mwafaka sasa kwa serikali kuanzisha miradi mipya ya maji sambamba na kutekeleza iliyopo ili kila mwananchi apate maji. Nchi yetu ina mamlaka za maji zaidi ya 80, lakini idadi hiyo haiendani na huduma za maji ambazo wananchi wanatakiwa kuzipata, hivyo kuna haja kubwa kwa serikali kuzipa msukumo mamlaka hizo ambazo zinawalenga wananchi moja kwa moja ikiwamo kuziwezesha kifedha na kuzisimamia kwa karibu ili utendaji wake uwe wa tija na ufanisi.

Kwa kuwa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2015-2020 pamoja na mambo mengine, inasema kuwa serikali yake itaendelea na juhudi za kuimarisha huduma za kijamii ikiwamo maji, matarajio yetu ni kuwa ahadi hiyo itatekelezwa kutokana na Serikali ya Awamu ya Tano kuonyesha kwa vitendo kuwa imedhamiria kutekeleza ahadi zake.

Tunashauri kwamba Serikali iwekeze zaidi katika maji kwa kuanzishaji wa miradi kadhaa kama uchimbaji wa visima hususani maeneo ya vijijini, uchimbaji wa mabwawa na kutumia maji ya maziwa na mito yatakayotumika kwa umwagiliaji.

Tukumbuke kuwa maji ni uhai na bila kuwa na maji ya uhakika safari yetu ya kuwa na viwanda kuelekea uchumi wa kati itakuwa ngumu. Kutokana na umuhimu wa maji, kuna msemo kuwa ‘Vita ya Tatu ya Dunia itatokana na maji’.

Habari Kubwa