Miundombinu iboreshwe kuepusha mafuriko Dar

15May 2019
Mhariri
DAR ES SALAAM
Nipashe
Miundombinu iboreshwe kuepusha mafuriko Dar

Kwa takribani siku nane ambazo mvua za masika zimenyesha mfululizo katika Jiji la Dar es Salaam, athari zilitokea, vikiwamo vifo vya watoto wawili, hivyo funzo tunalolipata ni kuwa  mwarobaini ni kuboreshwa kwa miundombinu.  

Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa, tukio la kwanza lilitokea Mei 8, mwaka huu, saa 9:00 alasiri maeneo ya Goba wilayani Kinondoni, ambapo mtoto mmoja alifariki dunia, baada ya kutumbukia kwenye kisima cha futi 30 kilichokuwa wazi nyumbani kwao.

Kamanda Mambosasa alisema mtoto mwingine ambaye anakadiriwa kuwa na umri wa miaka (4-5), alifariki dunia Mei 12, maeneo ya Mongo la Ndege, kwamba mwili wake ulikutwa ukielea katika Mto Msimbazi bila kuwa na jeraha lolote.

Mbali na vifo hivyo, wakazi wa maeneo kadha ya Jiji la Dar es Salaam wameathirika kutokana na nyumba zao kuzingirwa na maji.

Kadhalika, mvua hizo zimesababisha usumbufu mkubwa kwa wakazi wa Jiji kutokana na maji kuathiri miundombinu hususan baadhi ya barabara, hivyo baadhi kufungwa kwa muda, huku baadhi wakikwama kupita kwenye baadhi ya maoeneo kwenda kwenye shughuli zao za ofisi, biashara na za kijamii.

Baadhi ya miundombini ya taasisi iliathirika. Kwa mfano, Kamanda Mambosasa alisema, mvua hizo zimesababisha uharibifu wa baadhi ya majengo ya Shule ya Msingi Mwale iliyopo Kiwalani, Majani ya Chai Kiwalani na Shule ya Sekondari Kibasila iliyopo Manispaa ya Temeke ambayo imejaa maji na kusababisha kushindwa kuendelea na masomo.

Kutokana na hali hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, ametoa tahadhari kwa wakazi wa jiji hilo waishio mabondeni kuhama maeneo yao.

Aliyataja maeneo yaliyofurika ni Jangwani, Magogoni Kigamboni, Ilala Kata ya Mchikichini, Kipunguni, Viwege, Majohe, Kata ya Tabata Madona na Temeke Shule ya Sekondari Kibasila.

Mengine ni Kinondoni Kata ya Kigogo, Tandale, Bunju eneo la Basihaya, Mwananyamala Mitaa ya Bwawani, Kambangwa, Msisiri ‘A’, Mbezi darajani na katikati ya Jiji.

Alisema Serikali inaendelea kuchukua hatua kurekebisha athari zilizojitokeza ili kuwaondolea adha wananchi kwa kuhakikisha mifereji iliyoziba inazibuliwa, kuweka madaraja ya muda pale madaraja yalipoharibiwa na maji, na kurekebisha barabara ili wananchi waendelee na shughuli zao.

Suala la kuboresha miundombimu lina umuhimu wa pekee katika kukabiliana na athari za mara kwa mara pale mvua zinapokuwa zinanyesha.

Hatua hizo zonaweza kuwa ujenzi wa madaraja ya muda katika maeneo ambayo yanakumbwa na mafuriko kama akivyosema Makonda, lakini pia ipo haja ya kujenga madaraja katika maeneo sugu kwa kuathiriwa na mafuriko kama Jangwani ili kurahisishia wananchi usafiri wakati wa mvua.

Tukio la Jumatatu lililowasababishia usumbufu wakazi kadhaa wa jiji na kulazimisha kulipa nauli ya Sh. 1,000 hadi 2,000 kutoka Jangwani hadi Posta na Kariakoo baada ya barabara kujaa maji na kufungwa kwa muda, linapaswa kuchukuliwa kama somo, ili kujengwa miundombimu ya uhakika.

Ushauri wetu ni kuwa pamoja na mamlaka zetu kuwataka wananchi kuondoka katika maeneo ya mabondeni, pia zijishughulishe na kujenga mitaro ya maji katika maeneo mengi yanayoathirika kwa maji na barabara kutokupitika wakati wa mvua, ingawa sio ya mabondeni.

Ni matumaini yetu kuwa hatua za dharura zinaweza kuchukuliwa sasa kutokana na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), kueleza kuwa mvua kubwa za masika zitaendelea kwa siku kadhaa.

Habari Kubwa