Mkoa wa kipolisi Rufiji umekuja wakati mwafaka

11May 2017
Mhariri
Nipashe
Mkoa wa kipolisi Rufiji umekuja wakati mwafaka

MATUKIO ya uhalifu wa kutisha ambao umesababisha hofu kubwa ya usalama wa wananchi katika wilaya za Rufiji, Kibiti na Mkuranga mkoani Pwani, umeifanya serikali ichukue uamuzi wenye lengo la kukabiliana na hali hiyo, lengo likiwa ni kulinda usalama wa raia na mali zao.

Katika kukabiliana na kudhibiti matukio hayo yakiwamo ya mauaji, serikali imetangaza kuwa itaanzisha mkoa mpya wa kipolisi wa Rufiji ili kuimarisha ulinzi na usalama wa wananchi na mali zao na kurejesha amani na utulivu katika eneo hilo na maeneo ya jirani.

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba, alitangaza uamuzi huo bungeni mjini Dodoma juzi wakati akiwasilisha hotuba ya bajeti ya wizara yake kwa mwaka ujao wa fedha 2017/18.

Waziri Mwigulu alisema uanzishwaji wa mkoa huo wa kipolisi utasogeza huduma ya polisi karibu zaidi na wananchi na kurejesha amani na utulivu katika maeneo hayo ambayo yamekuwa tishio kwa usalama nchini.

Alisema mkoa huo utajumuisha wilaya hizo ambazo zimekuwa zikikumbwa na matukio makubwa ya kihalifu ambayo yamekuwa yakisababisha mauaji ya raia na askari.

Kwa mujibu wa Mwigulu, Wilaya ya Mafia nayo itakuwa ndani ya mkoa huo mpya.

Tunakubaliana na uamuzi huo wa serikali kwa kuwa ni sahihi kabisa na umefanyika wakati mwafaka kutokana na matukio ya kihalifu ya kutisha na kusababisha wananchi kuishi katika hofu kubwa.

Itakumbukwa kwamba Aprili 13, mwaka huu, askari polisi nane waliuawa kikatili na watu wasiojulikana katika eneo la Jaribu wilayani Kibiti, huku wauaji hao wakipora bunduki nne aina ya SMG na Long Range tatu.

Aidha tukio hilo lilikuwa ni mwendelezo wa matukio mengine ya mauaji ya viongozi kadhaa wa vijiji na vitongoji. Vile vile, kuna matukio yaliyowahi kutokea katika vituo vya polisi, malindo na baadhi ya benki.

Uamuzi kama huo wa kuanzishwa kwa mkoa wa kipolisi wa Rufiji uliwahi kufanywa na serikali kwa kuanzisha mkoa wa kipolisi wa Tarime/Rorya mkoani Mara kutokana na kukithiri kwa matukio ya uhalifu, yaliwamo mauaji na wizi wa mifugo.

Tunaipongeza hatua hiyo ya serikali kwa kuwa imefanyika kwa kuangalia hali halisi ya usalama katika maeneo hayo ambayo yamezungukwa na misitu mikubwa, hivyo kuwa rahisi kutumiwa na wahalifu kutekeleza malengo yao na kujihifadhi humo.

Pamoja na uamuzi huo, bado kuna haja kwa vyombo vya usalama kuendelea na msako mkali dhidi ya wahalifu wote waliohusika katika matukio ya mauaji ya raia na askari.

Tunaamini kuwa hilo litafanyika kutokana na ahadi ya Mwigulu kwamba serikali kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama, itaendelea kuwabaini wale wote wanaojihusisha na vitendo hivyo haramu pamoja na washirika wao ili kuwachukulia hatua stahiki za kisheria.

Kadhalika, serikali ihakikishe inapeleka askari wa kutosha kutokana na mkoa huo wa kipolisi kuwa na maeneo makubwa sambamba na vifaa muhimu ili iwe rahisi kudhibiti hali ya usalama na kurejesha utulivu.

Kwa upande wao, viongozi wa serikali wa ngazi zote na wananchi hawanabudi kutoa ushirikiano wa kutosha kwa vyombo vya ulinzi na usalama kwa kutoa taarifa mbalimbali za wahalifu na uhalifu zitakazowezesha kuwakamata wahusika wote na kuwafikisha mbele ya sheria.

Tunaishauri serikali isisite kuanzisha mikoa mingine ya kipolisi pale itakapobaini kushamiri kwa vitendo vya uhalifu vinavyohatarisha usalama wa maisha ya raia na mali zao. Vinginevyo tunasisitiza kuwa mkoa wa kipolisi wa Rufiji umeanzishwa wakati mwafaka.