Moto wa Kariakoo umetuachia funzo

14Jul 2021
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Moto wa Kariakoo umetuachia funzo

JUMAMOSI soko la kihistoria la Kariakoo liliteketea moto katika mazingira yenye utata, huku Jeshi la Zimamoto na Uokoaji likishindwa kukabili moto huo, kutokana na sababu nyingi zilizoelezwa, ikiwamo kukosekana kwa miundombinu ya maji na maji katika eneo hilo.

Hasara iliyopatikana ni kubwa katika soko hilo ambalo bado lilikuwa na madeni makubwa ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na mwanahisa mmoja ambaye ni Jiji la Dar es Salaam, huku ikiwa zimepita siku chache tangu Rais Samia Suluhu Hassan, atembelee na kuwasimamisha kazi viongozi wa soko na kuunda tume ya uchunguzi.

Moto huo ulizuka majira ya saa 2 usiku na ilishindikana kuukabili, kutokana na kukosekana kwa maji ya kuzima, wakati makao makuu ya Zimamoto yakiwa ni Upanga, umbali wa kilomita moja.

Ni jambo la kushangaza kwamba katika eneo la Kariakoo sokoni na kwenye mitaa yenye maduka ya bidhaa za kila aina ambazo huleta wafanyabiashara kutoka nchi za Zimbabwe, Uganda, Malawi na Zambia na DRC, kwa kutaja baadhi kuna majengo mengi ya ghorofa ambayo mwonekano wake ukiwa angani ni kivutio tosha kinachopendezesha Jiji, hakuna miundombinu ya maji ya kuwezesha kujaza gari la zimamoto!

Inaelezwa walilazimika kwenda umbali mrefu kutafuta maji ya kujaza kwenye magari ndipo wauzime, jambo ambalo siyo sahihi kwa kuwa kuwa sehemu kubwa ya kodi kwenye biashara inakusanywa kutoka Kariakoo.

Kingine ni vifaa vya kupanda kwenye jengo hilo kuwa tatizo, jambo linaloonyesha wanapaswa kufanya kazi ya ziada ya namna ya kukabili matukio hayo.

Huu ni ujumbe tosha kwa serikali kwamba inatakiwa kujipanga upya hasa kwa kuwa na miundombinu ya maji katika maeneo yote muhimu, na kujiandaa kwa ajili ya kukabiliana na majanga kama hili h na mengine.

Leo tunazungumza hasara kubwa iliyowapata wafanyabiashara zaidi ya 1,662, huku waliokuwa wanalipa pango wakiwa ni 224, ambao kila mmoja mtaji wake umeteketea na sasa wamerudi sifuri, kama walikuwa wamekopa benki maana yake watashindwa kurudisha.

Lakini wamiliki wa biashara hizo hawakuwa wanafanya wenyewe bali waliajiri Watanzania wengine, ambao walijipatia kipato na kuchangia uchumi wa nchi, na sasa wanashindwa kupata kipato chochote kutokana na hasara hiyo.

Pia, wamiliki na waliokuwa wameajiriwa wana wategemezi kwa maana ya watoto wa kusomesha au wanatakiwa kulipa kodi ya nyumba, kugharamia matibabu yao na ndugu wengine. Na huenda asilimia kubwa hawakuwa wamekata bima ya biashara zao na sasa wanarudi nyuma kimaisha, hii siyo hali njema kwao binafsi na uchumi kwa ujumla.

Kushindwa kudhibiti matukio ya moto imekuwa ni kilio cha muda mrefu kwa wanaokumbwa na majanga hayo, kwa kuwa ni kawaida kwa gari la zimamoto kufika bila maji au kufika eneo la tukio na kuondoka kwenda kuyatafuta mbali.

Ni muhimu Jeshi la Zimamoto na Uokoaji wakajifunza na kubadilika ili kukabili matukio ya moto kwa kuhakikisha magari yana maji na wanatumia mbinu zote kufanyakazi kwa ubora, vinginevyo watu wanapoteza imani na uwezo wao wa kukabili majanga.

Habari Kubwa