Msako wa wezi wa fedha za mikopo usiishie HESLB

21Jul 2016
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Msako wa wezi wa fedha za mikopo usiishie HESLB

SERIKALI imesema kuwa imegundua madudu ya kutisha ya ufisadi wa mikopo ya wanafunzi wa vyuo vya elimu ya juu nchini, huku zaidi ya wanafunzi hewa 2,736 wakiwamo marehemu na waliofukuzwa vyuo kwa sababu mbaalimbali, wakiendelea kulipwa mikopo na Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB).

Hali hiyo imemfanya Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako, kutangaza kuwa Serikali kuanzia sasa imesitisha utoaji fedha za mafunzo kwa vitendo kwa wanafunzi wote nchini mpaka pale uhakiki wa wanafunzi wanaostahili kulipwa mikopo utakapomalizika nchi nzima.

Kadhalika, Serikali haitatoa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu, hadi hapo itakapojiridhisha na uhalali wa wanafunzi wanaostahili kupata mikopo.

Kwa mujibu wa Profesa Ndalichako, wanafunzi hao walibainika baada ya HESLB kuanza ukaguzi wa wanafunzi wote waliopatiwa mikopo kujua kama wanakidhi vigezo na kwamba waliobainika kupewa mikopo ni wale waliofariki na waliofukuzwa chuoni kwa sababu mbalimbali.

Hali hiyo imeendelea kudhihirisha kwamba bado kuna udhaifu mkubwa katika taasisi za Serikali kiasi kwamba baadhi ya watumishi wanajiamini na kuiba fedha za umama watakavyo bila kuogopa chochote.

Ni hali inayothibitisha kile ambacho Rais John Magufuli amekuwa akikisema mara kwa mara kwamba kuna watu wachache wanaishi kama malaika na kuwaacha wengi waliishi katika maisha ya shida na mahangaiko.

Kikubwa tunachokiona ni kwamba vitendo hivi vimekuwa vikifanyika kutokana na viongozi pamoja na watendaji waliopewa dhamana ya kusimamia fedha za HESLB kutokuwajibika.

Kinachoonekana ni kwamba mchezo huu ulikuwa unafanywa na mtandao mkubwa unaowashirikisha watumishi wa HESLB kwa kushirikiana na wenzao walioko katika vyuo vikuu kwa kutumia udhaifu wa wenye dhamana ya kusimamia fedha hizo.

Kwa hiyo ni wazi kuwa kuna mtandao mkubwa wa wezi hao, hivyo, Serikali isiwagang’anie watumishi na watendaji wa HESLB tu, bali pia iwasake wahusika walioko katika vyuo vikuu na kuwafikisha katika mkono wa sheria.

Siku zote Watanzania tumekuwa tukipiga kelele za kulalamikia kuporomoka kwa kiwango cha elimu, bila kuainisha baadhi ya mambo yanayochangia. Hili la ufisadi nalo ni kikwazo, kwa sababu fedha zinazoibwa na mafisadi wachache kupitia wanafunzi hewa zingeweza kutumika kusomesha wanafunzi wanaokosa mikopo, kujenga madarasa, kutengeneza madawati, kuajiri walimu na mahitaji mengine katika sekta ya elimu.

Kama tuna nia ya dhati ya kunusuru elimu yetu, sasa inatosha kusema inatosha na kuchukua hatua stahiki zikiwamo kufanya uhakiki wa kina na endelevu wa fedha zote zilizotolewa kwa wanafunzi wote wa vyuo vikuu kupitia HESLB na kujiridhisha kama zilikwenda kwa walengwa ama la. Wale wote watakaobainika kuhusika kuziiba wafikishwe katika Mahakama ya Mafisadi na washtakiwe kwa uhujumu uchumi na ikiwezekana wafilisiwe mali zao ili zitumike kusomesha wahitaji wengine.

Hilo litakuwa fundisho kwa watumishi na watendaji wengine wa umma ambao wamekuwa wakizichakachua fedha hizo na kuzitumia kwa maslahi yao binafsi ka kuipa hasara Serikali.

Tunashauri pia kwamba njia bora itakayodhibiti matukio kama haya ni kuzipatia meno taasisi zetu ikiwamo HESLB kujiendesha kwa uhuru bila kuingiliwa na wanasiasa, ambao uzoefu unaonyesha kuwa wanachangia kwa kiasi kikubwa kuzivuruga taasisi zetu.

Habari Kubwa