Mtoto wa kike alindwe dhidhi ya ukeketaji, mimba za utotoni

11Oct 2018
Mhariri
DAR ES SALAAM
Nipashe
Mtoto wa kike alindwe dhidhi ya ukeketaji, mimba za utotoni

OKTOBA 11 kila mwaka ni siku ya maadhimisho ya mtoto wa kike duniani. Kitaifa maadhimisho hayo  yamepewa umuhimu wa pekee kwa kuanza kuadhimishwa-

mapema kwa kuendesha midahalo katika taasisi mbalimbali zinazotetea haki za mtoto wa kike dhidi ya vitendo vya ukatili ukiwamo wa ukeketaji na ndoa za utotoni.

Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia idadi ya watu (Unfpa), imeendesha midahalo hiyo kwa kuwashirikisha pia watoto ambao wanakumbwa na tatizo hilo.

Wadau wanaotetea haki za watoto wameshiriki katika midahalo hiyo ili kuhakikisha mtoto wa kike analindwa dhidi ya vitendo vya kikatili.

Madhumuni ya midahalo hiyo ni kusaidia kupata michango, mawazo na maoni mbalimbali kutoka kwa wadau ambayo itawezesha kutokomeza vitendo vya ukeketaji kwa watoto wa kike nchini.

Maadhimisho hayo yamelenga kuelimisha na kuhamasisha jamii namna ya kuwalinda watoto wa kike ili wasiweze kufanyiwa vitendo hivyo ambavyo katika baadhi ya mikoa nchini vimeendelea kushamiri na takwimu za vitendo hivyo kuwa juu.

Kadhalika midahalo inayofanyika inalenga kumsaidia mtoto wa kike kujitambua, kujithamini na kujilinda dhidi ya vitendo hivyo.

Kaulimbiu ya mwaka huu ni ‘Imarisha uwezo wa mtoto wa kike: Tokomeza ukeketaji, mimba na ndoa za utotoni’.

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Faustine Ndugulile akinukuu takwimu za utafiti wa idadi ya watu, anaeleza kuwa Mkoa wa Manyara unaongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya watoto wa kike waliokeketwa kwa asilimia 58.

Imeelezwa kuwa katika kipindi cha miaka 10 ijayo wasichana milioni moja watakuwa wameolewa wakiwa chini ya umri wa miaka 18 nchini.

Kwa sasa mikoa inayoongoza kwa ndoa za utotoni ni Shinganya kwa asilimia 69, Tabora (58), Mara (55), Dodoma (51), Lindi (48) na Mbeya (41).

Kadhalika kwa sasa nchini asilimia 27 ya watoto walio na umri kati ya miaka 15 na 16 wanapata ujauzito.

Aidha, kwa mujibu wa takwimu za Ofisi ya Takwimu ya Taifa (NSB), katika kipindi cha mwaka 2017, matukio 41,000 ya ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake na watoto yaliripotiwa na kati ya hayo ya watoto pekee yalikuwa 13,000.

Sababu ya kuendelea kushamiri kwa matukio hayo imeelezwa kuwa ni mila na desturi potofu na umaskini unaochochea watoto wa kike kuolewa chini ya miaka 18.

Katika kukabiliana na tatizo hilo serikali imepanga mkakati wa kupunguza vitendo hivyo kwa asilimia 50 ifikapo mwaka 2021 – 2022. Mkakati mwingine ni kukusanya takwimu za vitendo hivyo ili kubaini hali halisi na kuweza kukabiliana nayo.

Serikali pia imedhamiria kuanzisha madawati ya jinsia katika shule zote nchini kwa walimu kujengewa uwezo wa kushughulikia suala hilo.

Vile vile kuwa na `One Stop Center’ ambayo itajumuisha madawati ya Jeshi la Polisi, huduma za afya na ushauri nasaha, vitakavyopatikana sehemu moja na kuondoa usumbufu kwa waathirika.

Pia kuhakikisha mashauri ya ukatili wa kijinsia kwa watoto yanapewa kipaumbele na kuisha kwa wakati.

Takwimu za dunia zinaonyesha kuwa wasichana na wanawake wapatao milioni 200 wamepitia tatizo la ukatili wa kijinsia. Kwa Tanzania Mkoa wa Manyara unaongoza kwa vitendo hivyo kwa asilimia 58.

Habari Kubwa