Muafaka upatikane upakaji rangi mabasi ya wanafunzi

30Aug 2017
Mhariri
Nipashe
Muafaka upatikane upakaji rangi mabasi ya wanafunzi

INAONEKANA kuwa agizo lililotolewa na serikali kuzitaka shule binafsi kupaka rangi ya njano mabasi yanayobeba wanafunzi, utekelezaji wake ni mgumu, kutokana na wadau kukwama kufikia makubaliano.

Hali hiyo inatokana na wamiliki wa shule kueleza kuwa kama agizo hilo watalitekeleza, itabidi wapandishe ada ya wanafunzi, lengo likiwa ni kumudu gharama ya kununua magari mapya.

Kwamba watalazimika kununua magari mapya kwa kuwa kwa sasa magari wanayoyatumia kubeba wanafunzi wanayakodi.

Mamlaka ya Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra), imetoa muda hadi kesho kwa magari ya shule binafsi yanayobeba wanafunzi kupakwa rangi ya njano na ya shule 11 za umma ambazo wazazi wanachangia ifikapo 30 Septemba, mwaka huu yawe yamekamilika.

Kimsingi, hatua ya kuyapaka rangi magari ya wanafunzi ina mantiki na faida kuwa kwa kuwa ni utaratibu wa dunia na vile vile unasaidia watoto kuwahi shuleni na kutumia muda mfupi kurejea nyumbani kwa kuwa watasaidiwa na askari wa kikosi cha usalama barabarani. Aidha, ni rahisi kutambulika na wanafunzi kupata msaada kwa urahisi pale linapotokea tatizo.

Jambo la kufurahisha ni kuwa hata wazazi wa wanafunzi wa shule binafsi wanaunga mkono agizo hilo la serikali kutokana na kuwaondolea kero. Kinachowakwaza ni mzigo wa kutupiwa gharama zaidi ya karo ili wamiliki wa shule wagharimie ununuzi wa mabasi mapya yanayotakiwa kupakwa rangi.

Mwenyekiti wa Umoja wa Mameneja na Wamiliki wa Shule Binafsi na Vyuo (TAMONGSCO), Charles Totera, anasema magari mengi yanayotumika ni ya kukodishwa kwa muda ambayo hutumika nyakati za asubuhi na jioni, hivyo wakiamua kununua magari yao ni dhahiri wataongeza gharama za usafiri ambazo zitarudi kwa wazazi.

Suala hili bado ni changamoto kutokana na wahusika kutokufikia muafaka hadi sasa wakati siku ya mwisho waliyopewa na Sumatra ni kesho.

Kwa kuwa wadau muhimu wa suala hilo wameshirikishwa katika kikao cha kujadili suala hilo kama ambavyo inasema TAMONGSCO, ingawa wanasema wameweka tahadhari kuwa shughuli zisisimame bali magari ya shule yaendelee kupakwa rangi, huku ya kukodishwa yaendelea kubaki hivyo hadi mwishoni mwa mwaka huu.

Kauli hii inaonyesha wazi kuwa shule binafsi zinakubaliana na agizo la serikali la kupaka magari rangi, isipokuwa muda zaidi utolewe ili magari yanayokodishwa yawe yamepakwa rangi kufikia mwisho wa mwaka huu.

Ushauri ni kwamba Sumatra iwe na uvumilivu ili wadau wafikie makubaliano ili agizo hilo liweze kutekelezwa katika mazingira mazuri yenye mwafaka.

Miongoni mwa athari zinazoweza kutokea kama mamlaka hiyo itakosa uvumilivu na kuharakisha utekelezaji, ni kupanda kwa karo ya shule ikiwa njia ya shule binafsi kufidia gharama za kununua mabasi mapya ili kuyapaka rangi.

Hatua ya kupandisha ada ni dhahiri itawaathiri wazazi, hivyo kuwa kikwazo kwa baadhi ya wanafunzi ambao wazazi na walezi wao watakosa kumudu kulipa nyongeza hiyo.

Kwa kuwa shule zitaanza kufungwa kuanzia mwishoni mwa wiki hii kwa ajili ya likizo fupi, ni bora utekelezaji wa agizo la kuyapaka rangi magari ya wanafunzi tarehe ya mwisho ikasogezwa mbele, kuepuka uwezekano wa kuwaongezea mzigo wa ada siku chache baada ya shule kufunguliwa.

Tunasisitiza pande husika kuendelea na majadiliano na kulimaliza suala hilo na utekelezaji wake uanze kwa kuzingatia kuwa agizo hilo lina manufaa zaidi kwa wazazi kutokana na ahadi ya polisi kuwa wakiwa na magari yenye kutambulika kwa rangi ni rahisi kuruhusiwa kupita hata barabara za kando, ili kuwawahisha wanafunzi shuleni na nyumbani.

 

Habari Kubwa