Muhimbili iheshimu sera ya matibabu bure

07Oct 2016
Mhariri
Nipashe
Muhimbili iheshimu sera ya matibabu bure

JANA tulichapisha habari ndefu ya uchunguzi ikieleza jinsi kinamama wanaokwenda kujifungua wanavyopata mahangaiko katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.

Ni kwamba, tofauti na agizo la Serikali litokanalo na utekelezaji wa Sera ya Afya ya Mwaka 2007 inayosisitiza kwamba wajawazito wapate huduma bure, hali iko tofauti kwenye hospitali hiyo.

Wajawazito wanaofikishwa Muhimbili baada ya kuhamishwa kutoka katika hospitali nyingine za rufani hulazimishwa kulipa walau jumla ya Sh. 200,000 na kuendelea kulingana na matatizo yanayowafikisha hapo.

Aidha, zipo taarifa kuwa kutokana na gharama hizo kuwa za juu kwa wananchi wengi wa kawaida ambao huaminishwa kuwa huduma kwa wajawazito ni miongoni mwa Watanzania wanaosamehewa hospitali, baadhi yao hutelekeza vichanga ili kukimbia madeni.

Uchunguzi umebaini kuwa baadhi yao hulazimika kuendelea kukaa katika wodi kutokana na tishio la kuzuiwa kuondoka hadi wanapomaliza madeni yao.

Nipashe imebaini kuwa wazazi hao hutakiwa walipe gharama kadhaa zikiwamo za mchakato wa kuzalishwa, dawa, vifaa na pia gharama za kuwezesha watoto wao kutolewa kutoka katika wodi ambayo huhifadhiwa baada ya kuzaliwa.

Baadhi ya ankara, zinaonyesha kuwa kila kichanga hutozwa Sh. 3,000 kutokana na kile kinachoitwa kuwa ni “IP settlement Bill”, kwa kinamama wanaolazwa kama “gharama za kumkomboa mtoto”.

Nyingine ni Sh. 250,000 za huduma inayohusiana moja kwa moja na uzazi na dawa nyingine ambazo hutozwa kulingana na mazingira ya huduma kwa mzazi husika. Pia kuwa kinamama wanaojifungua kwa upasuaji, hasa wanaojifungua mapacha, hukumbana na gharama kubwa zaidi zikiwamo pia zile zinazohusiana na damu.

Kimsingi, gharama hizi ni kubwa sana na zinatozwa kwa kundi ambalo Serikali ilishabaini kuwa linahitaji huduma bure za afya, kutokana na kutambua wananchi wengi ni maskini, ndiyo maana serikali iliamua kutunga sera ya matibabu ya bure kwa wajawazito, watoto chini ya miaka mitano na wazee.

Baada ya utekelezaji wake kuanza, watoa huduma katika zahanati, vituo vya afya na hospitali walitakiwa kutoa huduma bure kwa makundi hayo. Kuwatoza fedha ni ukaidi wa sheria, kanuni na taratibu za serikali na vile vile ni kutojali utu.

Moja ya malengo ya millennia ni kupunguza idadi ya vifo vya wajawazito na watoto na ndiyo maana serikali imekuwa ikitenga fedha kwa ajili ya kulipatia kundi hilo huduma za matibabu. Katika bajeti ya 2016/17, Serikali imepanga kutumia Sh. bilioni 251 kugharimia dawa na vifaa tiba. Kati ya fedha hizo, Sh. bilioni 18 ni kwa ajili ya kugharimia uzazi wa mpango na afya ya mama na mtoto.

Tunampongeza Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, ambaye baada ya kusoma habari hiyo, ameiagiza Bodi ya Muhimbili kueleza sababu za kutoza fedha hizo wakati sera ya afya inatamka wazi kuwa huduma za afya kwa wajawazito ni bure.

Ummy amesema anashangaa kwa kuwa mishahara ya madaktari inalipwa na serikali kwa kodi za walipakodi wakati serikali ndiyo inayopeleka dawa na vifaa tiba hospitalini.

Mbali na kumpongeza Waziri Ummy kwa hatua hiyo, tunamshauri achukue hatua stahiki na za haraka dhidi ya wanaokaidi maagizo na maelekezo ya serikali kuhusu matibabu ya bure kwa makundi husika.

Habari Kubwa